Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Eng. Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nipende kutoa shukrani zangu na pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maono yake makubwa katika sekta hii ya mawasiliano kwa kufungua milango ya uwekezaji. Ambapo sisi sekta ya mawasiliano tunaiona na katika kuwekeza, katika miundombinu na mifumo ya mawasiliano na pia kwa utayari wake ili kurejea Sera na Sheria ambazo haziendani na wakati wa sasa, ambapo tuna teknolojia zinazoibukia hivyo basi Mheshimiwa Rais yuko tayari.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuridhia mchakato wa uundwaji wa satellite yetu. Ambapo anaenda kuweka alama kubwa sana katika sekta ya mawasiliano na katika ulinzi wa nchi yetu hivyo tunampongeza sana kwa kutekeleza mfumo wa anuani ya makazi kwa asilimia 100 kabla hata ya kufikia mwaka 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini na kwa kuakikisha kwamba leo hii nasimama katika bajeti ya tatu ya Wizara hii nikiwa namshukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maelezo yake, kwa ushauri wake wa kuhakikisha kwamba sisi wasaidizi wake tunaendelea kufanya kazi kwa weledi mkubwa. Nimshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Nape Moses Nnauye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa uongozi wake mzuri, maelekezo yake na kwa malezi yake yenye lengo la kuinua Sekta ya Habari na Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Katibu Mkuu, Mheshimiwa Mohammed Khamis Abdulla pamoja na Naibu Katibu Mkuu na Wakurugenzi wote wa Taasisi ambazo ziko chini ya Wizara yetu. Niwapongeze na kuwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Bariadi kwa kuendelea kunipatia ushirikiano katika majukumu yangu ndani ya jimbo na wakati napotekeleza majukumu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kutumia fursa hii kumshukuru sana mke wangu Grace ambaye kwa kweli ananipatia utulivu na kuhakikisha kwamba nawajibika vizuri katika majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru wewe pamoja na Mheshimiwa Spika, kwa kuendelea kuongoza Bunge hili kwa viwango vya kimataifa. Baada ya kusema hayo sasa naomba nirejee hoja za Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, kwanza tunaishukuru sana Kamati yetu ya Kudumu ya Miundombinu pamoja na michango yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wamejaribu kugusia. Niseme jambo moja Wizara hii champion wake ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania akisaidiwa na kaka yangu, Mheshimiwa Waziri, Nape Moses Nnauye, pamoja na Taasisi zetu ambazo ziko chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumebaini kuna changamoto katika mgawanyo wa minara ambapo Waheshimiwa Wabunge wamejaribu kugusia na mgawanyo huu tuliangalia kwa kuangalia wilaya kwa wilaya. Lakini baada ya kugawa kwa wilaya tukagundua kwamba kuna majimbo mawili kwenye baadhi ya wilaya hatimaye tukajikuta kwamba kuna baadhi ya majimbo yanapata minara mingi na majimbo mengine yanapata minara michache, hivyo tumeishaliona hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nitumie fursa hii katika Bunge lako tukufu kusema kwamba Mheshimiwa Rais, amesaini mikataba ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika Kata 713 kwa ujenzi wa minara 758. Hiyo ni mvua ambayo haijawahi kushuhudiwa sasa tunakuja na mvua nyingine ya kuleta minara 1,600. Ambapo Mheshimiwa Rais tayari ameisharidhia na ameishatafuta fedha na tutaanza na minara 600, ambayo kufikia Desemba nafikiri fedha zitakuwa zimeishapatikana tayari mchakato utakuwa umeishaanza wa kutafuta wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo Waheshimiwa Wabunge niwatoe hofu na Watanzania kwa ujumla mvua hii itakapokatika itaanza mvua nyingine ya minara. Kwa hiyo, tutahakikisha nchi yetu inafikishiwa huduma ya mawasiliano kwa mujibu wa utekelezaji wa Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wameligusia kwamba Wizara yetu mpaka sasa tumepokea fedha kidogo katika miradi ya maendeleo. Miradi yetu yetu inatekelezwa kwa ujenzi na wakandarasi, mkandarasi anapopatikana hatuwezi kumlipa fedha zote mpaka pale atakapokuwa anatoa certificate na miradi hii mingine inakamilika kwa miezi sita, mwaka mmoja. Hivyo tunatarajia kila anapokamilisha hatua moja na anapo raise certificate na ndipo tunapoweza kufanya malipo. Kwa hiyo, fedha zipo na tuna uwakikia watakapoleta certificate watalipwa na miradi itakamilika bila kuwa na changamoto yoyote ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna baadhi ya Waheshimiwa wameshauri na kuna baadhi ya changamoto nipende kusema kwamba baadhi ya changamoto zao tumezipokea, ushauri wenu tumeuzingatia, maoni yenu tunayazingatia na tutahakikisha kwamba tunaenda kuyafanyia kazi kwani nyinyi mko hapa kwa niaba ya Watanzania milioni 63 hivyo Serikali hii ya Mama Samia Suluhu Hassan ni sikivu na sisi wasaidizi wake tutahakikisha kwamba tunafanyia kazi mambo yote hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee jambo moja la mkomazi Mheshimiwa Zuena Athumani Mbunge kutoka Kilimanjaro aliongelea kuhusu usikivu wa TBC. Usikivu wa TBC tulikuwa na mtambo wetu pale Rombo Tarakea ule mtambo uko chini na sasa tunaenda kufunga mtambo mwingine pale Rombo DC. Hivyo tutakuwa tumetatua kabisa changamoto ya maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile umeongelea kuhusu hifadhi ya Mkomazi, katika hifadhi hiyo tayari kuna mawasilino tunapeleka katika eneo la Kata ya Kilia, Kwakoa, Toloha pamoja na Mgagawa ambazo ziko pembezoni mwa nchi yetu ambapo baada ya kuweka hiyo minara itaweza kufikisha huduma ya mawasiliano katika lango la hifadhi ya Mkomazi. Kwa suala kama hili naamini kwamba Mheshimiwa Mbunge awe na subira na Serikali iko kazini kuhakikisha kwamba changamoto hii inatatuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimeshuhudia Waheshimiwa Wabunge wakiishukuru Serikali na sisi hatuta bweteka kwa shukurani zao. Sisi tutaendelea kuhakikisha kwamba katika maeneo ambayo bado hayajafikishiwa huduma na mawasiliano na katika changamoto zile ambazo wamekuja kuzisema kwa niaba ya wananchi wao sisi tunazichukua na tutaenda kuzifanyia kazi kwa weledi, maarifa yote kwani tunazingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nikushukuru sana na niombe kusema kwamba niwashawishi Waheshimiwa Wabunge, tuiunge Bajeti yetu hii kwa asilimia mia moja kwani ni bajeti shirikishi na ni bajeti ya wananchi…

NAIBU SPIKA: Ahsante, ahsante kwa mchango mzuri.

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.