Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia katika hoja hii ya bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Mheshimiwa MNami napenda kuungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dokta Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anafanya mageuzi makubwa ya teknolojia na maendeleo ya kidijitali hapa nchini kwetu, ikiwemo pia kuhakikisha kwamba Serikali inaboresha namna ambavyo inafanya kazi kwa kutumia TEHAMA.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Nape Nnauye na Viongozi wote wa Wizara hii kwa mageuzi makubwa ambayo anaendeleea kuleta katika sekta hii muhimu. Kipekee ningependa pia kumpongeza sana Dada yangu Justina Mkurugenzi Mtendaji wa UCSAF kwa kazi kubwa ambayo anafanya, siyo tu ya kupeleka minara lakini ya kuhakikisha ya kwamba shule zetu zinaunganishwa na mtandao ili watoto wetu waanze kukua kupata elimu ya kidijitali na stadi zingine tokea wakiwa kwenye umri mdogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo awali kulikuwa hakuna Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na badala yake masuala yote yanayohusiana na TEHAMA yalikuwa yamegawanywa ama yametapakaa sehemu mbalimbali kwa maana ya Serikali, taasisi na maeneo mengine ya Serikali. Kwa utashi wa Mheshimiwa Rais Dokta Samia Suluhu Hassan mwaka 2021 aliamua kuunda Wizara hii mahsusi ambayo itakuwa na mamlaka na dhamana ya kusimamia na kuunganisha na kuratibu masuala yote yanayohusu na TEHAMA na ninampongeza sana Mheshimiwa Rasi kwa jambo hilo kwa sababu limeongeza tija ambayo wengi wetu tunaisifia hapa leo Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya badiliko hilo, moja ya vitu ambavyo vilifanyika ni kuhamisha Data Center ambayo ilikuwa iko chini ya Ofisi ya Rais na ikahamishiwa ikaletwa kwenye Wizara hii. Lengo zima ni kutimiza lengo la Serikali kuwa na sehemu moja ya kukusanya data na ilionekana kwa kuwa sasa tuna Wizara hii mahsusi, basi jukumu hilo liletwe kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi katika mchango wangu wa siku ya leo nitajikita katika e-GA (E-government Agency). E-government Agency hivi sasa iko chini ya Ofisi ya Rais, Utumishi na ninatambua kwamba chini ya e-GA kuna sehemu mbili. Sehemu moja ni platform, sehemu nyingine ni masuala ya utumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupendekeza ya kwamba suala la utumishi libaki kwenye Ofisi ya Rais, Utumishi lakini suala la e-GA platform lihamishwe liletwe kwenye Wizara hii ambayo ndiyo ina dhamana na mamlaka ya usimamizi wa masuala yote ya TEHAMA.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu hivi sasa ijapokuwa tunayo e-GA lakini kutokana na pale ambapo ipo, hivi sasa kuna mifumo mingi ambayo haisomani. Nitatoa mfano mdogo, Walimu wetu ambao wako chini ya TAMISEMI wanatumia mifano mingi kuingiza taarifa na mifano hiyo haisomani.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu tukija kwenye sekta ya afya. Leo hii mimi naweza kufanya kipimo cha CT scan Hospitali yetu ya Benjamin Mkapa hapa Dodoma lakini nikilazimika kufanya CT scan Muhimbili Dar es Salaam, inabidi nifanye CT scan tena kwa sababu mifumo haisomani na viko vipimo hivi vya afya ambavyo huruhusiwi kufanya mara kwa mara.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba tumepongeza maeneo mengi yamepata minara lakini kwa masikitiko makubwa kwa Wilaya ya Nyang’hwale hakuna mnara hata mmoja na taarifa tulizileta kwamba kuna tatizo la usikivu. Kwa hiyo, nataka nikupe taarifa kwamba tunapongeza lakini Wananyang’hwale tuna masikitiko makubwa. Ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Amar umesimama hiyo ndiyo hoja aliyokuwa anazungumza Mbunge kweli? Mheshimiwa endelea.

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba utanilindia muda wangu. Kama nilivyokuwa nasema kuna umuhimu mkubwa wa mifumo hii kusomana kwa sababu pasipo kusomana inawaongezea gharama kubwa sana Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa hapa kwenye eneo hili, digital competitiveness ya nchi yaani ushindani wa kidijitali wa nchi unapimwa kutokana na ushiriki wa startups kwa maana ya sekta binafsi. Kwa kuwa e-GA iko chini ya Ofisi ya Rais, Utumishi, e-GA wanafanya mifumo yote wenyewe, hawashirikishi hata kidogo sekta binafsi wala startups zetu, wakati hapa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ninampongeza sana nimefarijika kusikia lengo la Wizara ni kuona namna gani ambavyo tutaimarisha startups zetu ili nasi tuweze kufika mahali startups zetu ziweze kuuza nje ya nchi teknolojia yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tunasifika kwa mfumo wa GePG (Government Procurement) na mfumo wa BRT (Mabasi ya Mwendokasi) lakini nchi zinakuja kujifunza hapa kwetu, kitakachokuja kutokea sasa ni nchi hizi zitajifunza kwetu, zitapeleka haya kwenye sekta binafsi yao, wale watatengeneza halafu wale watauza watanufaika kwa kile ambacho kilanzia kwetu. Hili jambo lazima tuliangalie kwa jicho la kipekee na kwa wivu mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka nitatoa mfano mdogo wa nchi kama Estonia. Nchi ya Estonia ina watu milioni 1.3 tu lakini inasifika katika startups zao kuja na teknolojia ambazo zimeweza kuvuka mipaka. Wana startups 10 na hizi startups 10 peke yake zina thamani ya zaidi ya Dola bilioni moja. Hiyo ndiyo dhana nzima ya kuwa na masuala haya ya e-GA na masuala ya ubunifu kwenye Wizara ya TEHAMA. Kwa hiyo, mimi naendelea kusisitiza kwamba Serikali ione namna ya kuhamisha masuala ya e-GA kutoka ilipo na yaje kwenye Wizara hii ya TEHAMA.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo tu hivyo, kwa kuwa e-GA inafanya biashara peke yake inaiongezea gharama kubwa sana Serikali. Nitatoa mfano mdogo uko Mfumo wa TANePS. Huu mfumo umetumia takriban zaidi ya shilingi bilioni sita na bado haujakamilika. Huu mfumo ungepewa kwenye sekta binafsi ingetumika takribani chini hata ya shilingi bilioni moja na mfumo ungekuwa umeshakamilika. Kwa hiyo mimi ambacho ningependa kumuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake anipe kauli na maoni na mipango ya Serikali, kwa kuwa sasa tunayo Wizara mahususi, Wizara hii ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia na Habari atuambie nini mpango wa Serikali katika kuhamisha suala la e-GA kwa upande wa platform litoke Ofisi ya Rais, Utumishi na lije kwenye Wizara hii mahsusi ili tuweze kupata tija lengwa na tuweze kuimarisha ushindani wetu wa kidijitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)