Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika kuifungua Tanzania kwa njia ya mawasiliano. Nimpongeze Waziri Mkuu, nimpongeze Waziri Nape, nimpongeze Waziri Kundo pamoja na watendaji wote wa sekta hii ya Habari.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo nitachangia kuhusu usikivu wa redio ya TBC katika maeneo ya mipakani, ukosefu wa mawasiliano katika maeneo ya mipakani pamoja na Hifadhi ya Mkomazi ambayo jina lake maarufu kwa kule kwetu inaitwa Kambi ya Simba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuhusu ukosefu wa mawasiliano ya redio ya Taifa (TBC). Katika Mkoa wa Kilimanjaro maeneo ya mipakani hatuna usikivu kabisa wa redio yetu, mara nyingi ukifungua redio unasikiliza redio za kenya kitu ambacho Watanzania wanakosa kupata Habari ya nchi yao. Jambo hili tumekuwa tukiliongea, mimi binafsi nimeliongelea sana hapa katika Bunge hili lakini hata leo hii katika Mkoa wa Kilimanjaro maeneo ya Rombo, Vijiji vya Kikererwa na vijiji vingine jirani ambavyo viko mpakani hawasikii kabisa redio yetu ya TBC.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali, katika minara hii ifanye jitihada ya kupeleka minara hiyo katika maeneo hayo ili na sisi Watanzania tujivunie shirika letu la mawasiliano jinsi linavyofanya kazi kuliko tukikaa kule tunasikiliza redio za wenzetu hatupati habari zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi tena katika mawasiliano maeneo hayohayo. Safaricom imekuwa ikitawala sana maeneo haya, kiasi kwamba hata mtu akiwa yuko kule kijijini hawezi kupata mawasiliano ya Vodacom, Tigo na kampuni nyingine za Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme walinzi wakubwa wa mipakani ni wananchi wanaoishi kule. Kwa hiyo kwa kukosa mawasiloiano kwao tunakosa hata kupata taarifa mapema pale ambapo panakuwa na changamoto yoyote katika maeneo ya mipakani. Niiombe Serikali katika minara hii 758 wahakikishe sasa kwamba maeneo yote ya mipakani yanapata minara ili Watanzania na sisi tuweze kupata huduma stahiki ya mawasiliano katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika maeneo ya Hifadhi ya Mkomazi. Nimesimama hapa Bungeni zaidi ya mara mbili nikiongelea changamoto ya mawasiliano katika Hifadhi ya Mkomazi. Hifadhi ile inawanyama wakali, hifadhi imetokea kuwa na changamoto nyingi za wananchi kuporwa mali zao, hifadhi ile hata Askari wa Wanyamapori maeneo yale walituomba sisi kama Kamati tusaidie ili waweze kupata mawasiliano kwa kuwa inaweza ikatokea changamoto yoyote ndani ya hifadhi lakini hawana mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali yangu sikivu Serikali ya Chama Cha Mapinduzi; Mheshimiwa Rais ameshuhudia utiaji saini wa minara 758. Katika minara hiyo niiombe sana Serikali iangalie maeneo ya hifadhi kwa kuwa kule ndani ya hifadhi kunakuwa na changamoto nyingi. Inaweza ikatokea hata Wanyama wakali lakini utoaji wa taarifa ukawa ni hafifu sana hivyo niombe katika minara hiyo 758 serikali itupe jicho katika Hifadhi ya Mkomazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nichangie kuhusu suala la wizi wa mitandaoni. Ni ukweli kwamba vijana wengi wanatumia kuibia wananchi katika mitandao unaweza ukafungua simu ukaambiwa nitumie pesa kwa namba hii hii jina litatoka fulani fulani fulani. Mheshimiwa Nape nakuamini Waziri wangu, Mheshimiwa Kundo nakuamini Waziri wangu, ninyi ni vijana mmepewa hii Wizara kwa kuwa ni vijana ambao ni wachapakazi hakikisheni kwamba kazi hii wanayoifanya matapeli wanataka kuwazidi akili. Msikubali kabisa hali hii ya wizi wa kutumia simu nchini Tanzania ukaendelea, udhibitini. Naamini mnao uwezo wa kufanya hivyo ili wananchi waweze kuishi vizuri na kuona kwamba wizi huu umetokomea.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo na mimi naungamkono hoja, lakini nitaomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa uwaeleze Watanzania hasa wa Mkoa wa Kilimanjaro…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: …ni lini wataondokana na adha ya kusikiliza safari com badala ya Vodacom na mitandao mingine ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.