Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Hapa juzi tumeshuhudia utiaji wa saini wa minara 758 ambayo inakwenda kujengwa kwenye maeneo ambayo ni ya wananchi wa kawaida sana. Hii imetokea ni kwa mkupuo mmoja kwa mwaka mmoja. Huko nyuma tangu uwepo wa Tanzania imekuwepo minara 1383 tu. Jambo kama hili linatokea kipindi hiki cha Mheshimiwa wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, haijawahi kutokea kipindi chochote kile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nataka nisema sisi Wabunge kama wawakilishi wa wananchi hatutakiwi kuona haya wala soni kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Waswahili wanasema mtu husifia chake hasa kinapompendeza. Mheshimiwa Rais, anatupendezesha Tanzania inang’ara. Ahsante sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote yanayofanyika lengo lake kubwa ni kuhakikisha ufanisi wa mawasiliano, data lakini pia kumpunguzia mzigo wa gharama za bundle mtanzania aliyeko huko chini. Pia, haya yatawezekana iwapo kila unapokwenda mnara REA watapeleka umeme na umeme utarahisisha uendeshaji wa minara hiyo badala ya sasa ambapo minara inazungushiwa mafuta ya diesel kila siku, inaongeza gharama kubwa

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa kuliko zote, pamoja na minara yote hiyo ubora wa mawasiliano, ubora wa usikivu usipoboreshwa tutaendelea kuliwa. Na nataka niseme, katika hili kuna mahali mimi ninaamini sisi hatuko vizuri katika Tanzania na hasa katika vertical modulation. Namuona Mheshimiwa Waziri anacheka, ni kwa sababu nimekuwa nikiwaambia siku zote. Hawa Mawaziri wako vizuri sana na nataka niseme ingekuwa ni kipindi kile ndio tunaoita wanajeshi wa mwamvuli lakini katika hili la vertical modulation.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tumefeli hata ukisafiri kidogo ukipanda kakichuguu tu mawasiliano yanakatika na yanapokatika hela yetu inaliwa huko ndiko tunakowaibia wananchi

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mfano mmoja, ukitoka Kasumuru kwenda Blantyre, Malawi ni kilomita zaidi ya 1300. Ukitoka pale, kama unaongea na simu unauwezo wa kuongea na simu isikatike unapanfa milima unashuka milima mpaka unafika Blantyre. Tanzania nini kinashindikana? Ninaiomba Serikali yangu iangalie ubora wa mitandao ili wananchi wapate ile quality inayotakiwa kwenye usikivu na pia hata kwenye pesa yao wanayoitumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo usikivu tu, hata hapahapa ukimpigia mtu simu ukiongea dakika moja hujamalizia hata ya pili itakuta mikwaruzo imeshaingia kwenye simu. Sasa hapo ubora unakuwa wapi ningeomba hili liangaliwe sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili niipongeze Serikali, imenunua mtambo wa kuchapa hapa kwa wenzetu wa TSN, lakini pamoja na juhudi zote hizi iwapo Serikali na Mawaziri hamtasisitiza wadaiwa wa taasisi hizi pamoja na taasisi zingine, hasa Serikali na Wizara kutokulipa madeni tutakuwa tunaua kabisa. Hata tununue mitambo gani msipolipa madeni mtakuwa mnaua kabisa haya mashirika yetu. Tunaomba mlipe madeni mnayodaiwa. Na mnapolipa madeni msiwape hawa wanao simamia wakaanza kuota mnvi kwa sababu inaonekana wao hawadai wakati ni ninyi hamlipi. Kuna wakati mtu unaweza ukadai ukashindwa; sasa naomba tuwasimamie hawa wenzetu wapate pesa zao ni pamoja na TTCL wapewe pesa zao wanazodai kwenye Mashirika, Posta vivyo hivyo Serikali isimamie.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni kuhusu hawa vijana wanaoanza kwenye TEHAMA. Nashukuru sana wapo startups wanakuwa wanalelewa. Wapo Watanzania wazuri hata ukienda kule kwangu Kyela ukienda Mbeya, wana uwezo wa kutengeneza mifumo yote katika Serikali hii e-GA kwa nini inang’ang’ania kutengeneza mifumo wakati wapo vijana ambao kwa kuwapa kazi tungetoa ajira lakini pia tungepata kodi? e-GA ambacho wanatakiwa kufanya ni kusimamia ubora na kuangalia uendeshaji wa mifumo hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ni kuhusu suala la anuani za makazi. Imekuwa kama watu wamerusha tu hili jambo linafanyika. Hivi kweli Tanzania tumekosa majina? Mtu anasema Barabara ya Shule, Barabara ya Church, Barabara ya Msikiti, Barabara ya Mosque. Kweli hakuna majina kabisa Tanzania? Tumeshindwa hata kutoa majina hata ya Wanyama? Haiwezekani, tusijidharirishe, unapoandika anuani hii ni ya kimataifa, unapo mwambia mtu alieko Marekani mimi naishi kwenye barabara ya school anakushangaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.