Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Jonas Van Zeeland

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo. Nichukue fursa hii nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uzima, lakini pia nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anazozifanya. Nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa na nzuri ambazo mnazifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mengi wenzangu wamezungumza, lakini mimi naomba nijikite kwenye eneo la migogoro ya ardhi, na kwa sababu ya umuhimu wake, nitajikita zaidi jimboni kwangu, kwa sababu tuna migogoro mingi. Moja ya wilaya ambazo bado zina migogoro ya ardhi ni Wilaya ya Mvomero. Pamoja na kazi kubwa na nzuri ambazo wanazifanya watalamu wetu, akiwepo Kamishna wetu wa Ardhi, Bwana Frank ambaye yuko Morogoro na watalamu wengine ambao wako katika wilaya yetu, lakini bado migogoro hii ni mingi, na ni kwa sababu ya eneo ambalo ni potential kwa kilimo lililopo katika wilaya yetu hii ya Mvomero. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mwekezaji ambaye alipewa eneo lenye ukubwa wa ekari 100,000 mwaka 1985 kwa ajili ya shughuli za ufugaji na eneo hili alipotea. Eneo hili ni lile la Kipunguni Mheshimiwa Waziri nafikili unalijua, liko Tarafa ya Mlali. Huyu mwekezaji alipewa eneo kwa ajili ya ufugaji, lakini hajawahi kufanya shughuli zozote za ufugaji kwenye hili eneo zaidi ya watu wachache aliowaweka ambao wanafuga mbuzi zisizozidi 50. Yaani mwekezaji ana eneo la ekari 100,000, anafuga, badala ya kufuga kama eneo linavyomtaka afanye, yeye anakwenda kufuga mbuzi 50 kwenye eneo. Sasa amekuja sasa hivi, anapima lile eneo, anauza vipande vipande lakini wananchi ambao wameishi na lile eneo kwa miaka mingi amewaambia atawapa eka elfu moja moja kwenye vijiji vitatu. Kijiji cha Mkata, Kijiji cha Merela Mlandizi na Kijiji cha Msongozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulipewa ekari 100,000 umeshindwa kuliendeleza, leo unakuja kuwapiga saundi wananchi kwa kuwapa eka elfu moja moja! Hata kama kuna baadhi ya maeneo huku alishatoaga akawapa wananchi, lakini kwa ekari 1,000 bado ni ndogo, na wananchi hawana maeneo mengine ya kwenda kufanya shughuli zao za kilimo na ufugaji isipokuwa ni hili eneo la Kipunguni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pia tuna wafugaji na Mheshimiwa Waziri unajua Mvomero ni eneo pia linalofanya shughuli za ufugaji. Tunao wafugaji. Sasa tunaomba katika eneo la huyu bwana wa Kipunguni ambaye alipewa mwaka 1985, eneo hili pia lipimwe wapewe wafugaji wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba, kuna eneo ambalo tulipewa na watu wa NARCO pale Dakawa, hili eneo tumepewa ekari 10,000. Ekari 5,000zilikwenda Luhindo kwenye Kijiji cha Luhindo, 5,000 zilikwenda kuinzisha Halmashauri. Tulipima kwenye eneo la ekari 5,000 ambalo limeanzisha halmashauri, tumepima eneo la ekari 3,000 tu, eneo la ekari 2,000 liko wazi na linaendelea kuvamiwa siku hadi siku. Sasa sielewi tatizo ni nini? Tatizo ni fedha za upimaji hakuna ili tuweze kulipanga hili eneo ni kimpango mji, ama ni uvivu tu wa wataalam wetu, wanakaa pembeni wakisubiri migogoro pengine inawezekana itakuja kuwanufaisha baadaye? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna eneo la ekari 5,000 ambazo zilikwenda pale Luhindo. Mheshimiwa Waziri hili eneo tunaomba lipimwe ili watu wamilikishwe kishera. Eneo hili tunataka kulitumia kwenye skimu ya umwagiliaji. Eneo hili sasa hivi limeshaanza kuvamiwa na mbaya zaidi wanawavamia watu ambao wanatoka nje ya Dakawa, wanatoka nje ya Kijiji cha Luhindo, mnatengeneza migogoro ninyi wenyewe halafu baadaye mnashindwa kuitatua hii migogoro. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, kama watu wako hawana fedha ya kutatua hii migogoro, wape fedha za kutosha migogoro iishe. Sehemu yenye migogoro hakuna maendeleo Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Rais; Mheshimiwa Hayati pamoja na Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia wamefuta mashamba pori tisa. Haya mashamba pori waliyoyafuta yana ukubwa wa ekari 13,000, lakini toka yamefutwa hayo mashamba Mheshimiwa Waziri pamoja na maelekezo ambayo yametolewa kwamba wapewe wakulima wadogo wadogo, wapewe wafugaji na litengwe eneo kwa ajili ya uwekezaji, mpaka leo tunavyozungumzwa hapa, hakuna kilichofanyika. Hakuna upimaji wowote. Sasa leo tunalia migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kukosa maeneo, halafu kuna ekari 13,000 zimekaa, Rais ameshazifuta, kwenda kupima na kuwapa wananchi mnashindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Mvomero ni miongoni mwa wilaya ambazo watu walikuwa mpaka wanauana kwa sababu ya migogoro ya wakulima na wafugaji. Leo tuna ekari 13,000 mnashindwa kuwapa hao wananchi? Au mnataka waingie wenyewe wajimilikishe mle halafu baadaye mje kutumia tena nguvu za kuwatoa? Mtengeneze migogoro ambayo leo hapa tunazungumza kuitatua wakati migogoro mingine mnaitengeneza inaanza upya ambapo badaye mtashindwa tena kuja kuitatua. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kama utatenga kwenye bajeti zako, naomba uweke hili jambo ili mweze kwenda kuimaliza migogoro pale Mvomero. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna eneo la Wamembiki. Hili ni eneo ambalo lina mgogoro wa muda mrefu sana. Hii mipaka inahamishwa hamishwa mara kwa mara. Wakija hawa wanasema hapa, wakija hawa wanapeleka hapa, mara tatu mipaka imehamishwa. Kuna mgogoro mkubwa sana pale kati ya hifadhi na wananchi. Naomba pia wapeni fedha watu wa Morogoro na Mvomero wakapime yale maeneo ili wananchi waweze kujua hatima ya huo mgogoro ni mgogoro wa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Kijiji cha Mkata. Kijiji hiki kilianzishwa mwaka 1965. Mwaka 1979 Serikali ilitoa tangazo la GN Na. 75 kuongeza mipaka ya hifadhi, lakini baadaye wananchi wakaambiwa, walikuwa wanalima kwenye bonde ambalo linaitwa Ngongoro. Wakaambiwa hili bonde liende kwenye Hifadhi ya Mikumi, wao watapewa bonde linaloitwa Kidaga ambalo lipo mpakani kabisa na Kilosa kule Mkata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu, ilikuwa ni hekta 814 na wananchi wakakubaliana kila mwananchi kwa kipindi kile apewe ekari mbili mbili kwa ajili ya kulima, lakini leo Mheshimiwa Waziri ninavyozungumza hapa, kuna wasanii wawili sijui wamepataje haya maeneo? Wamechukua haya maeneo na sasa wanawakodishia wananchi. Ni mgogoro ambao unawaumiza watu. Eneo walipewa miaka ya nyuma na walimilikishwa kisheria, lakini leo wamekuja watu wawili kwa ujanja ujanja wanaoujua wao, wamekwenda wamepewa haya maeneo na sasa hivi wanafanya biashara ya kukodisha, hawalimi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, timu yako ijue kuna mgogoro huo na tunaomba muende mkautatue. Ni mgogoro wa muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna mgogoro ambao uko pale kwenye mizani, ambapo ukishatoka Dumila kuna mizani, pale ndiyo mpaka wa Kilosa na Mikumi. Mwaka 2014 kulitokea mafuriko Wilaya ya Kilosa, kipindi hicho Rais alikuwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akatoa maelekezo kwamba wale wananchi ambao hawana maeneo ya kuishi baada ya mafuriko, waende pale kwenye lile eneo ambako sasa wamejenga mizani. Wale wananchi wameanza shughuli zao pale na wanazikana pale, lakini leo kuna watu wa Magereza wanataka kuwaondoa wale wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba jambo hili pia Wizara ilichukue kwa uzito wa kipekee. Nchi hii ni yetu sote. Mbona kuna maeneo mengine watu wanajifanya wao ni wakubwa sana? Hivi wewe Askari Magereza, watu wamepewa na Mheshimiwa Rais wakae, wewe unakuja kuleta kitambi chako, unasema hawa waondoke, kweli! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri hawa wananchi wabaki. Walipewa haya maeneo na Mheshimiwa Rais, kipindi hicho alikuwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, lazima hawa watu kama mnataka kuwatoa, mwafidie, lakini hawawezi kuondoka bila fidia yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tuna eneo ambalo pia lina mgogoro na eneo hili linashughulikiwa na watu wa halmashauri. Kama mgogoro huu ukishindikana kule wilayani, mimi nitakuja kwako. Eneo la mwekezaji mwenye Kiwanda cha Sukari Mtibwa na kuna eneo linaitwa Newland, hili ni eneo la muda mrefu sana lenye mgogoro wa zaidi ya miaka 30. Mimi pamoja na watalamu na watu wa Mtibwa na ninashukuru sana na kumpongeza huyu mwekezaji, ametoa ushirikiano katika kutaka kuutatua huu mgogoro na nina imani mgogoro utakwisha na kama hautakwisha kwa namna yoyote ile, Mheshimiwa Waziri nitakuja ofisini kwako ili uutatue huu mgogoro ni wa miaka 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimalize, Mvomero hatutaki wawekezaji feki. Mheshimiwa Waziri kuna watu, na wengine wako humu ndani wana maeneo kule Mvomero, jamani, Mvomero mkichukua maeneo mlime, ama mfuge. Hatutaki mje mwekeze kule majoka. Migogoro hii haitaisha na tunawakosesha watu fursa. Kama tukitoa ardhi na mkaitumia kwenye kilimo, ama kwenye ufugaji, kwanza mtatengeneza na ajira kwenye eneo letu, lakini maeneo ambayo yanatolewa Mvomero, watu wakishapewa, akishapewa hati, anasema hili ni eneo urithi wa watoto wangu. Sasa urithi wa watoto wako si waanze kulima sasa hivi. Hao watoto wenyewe, utakuta mtu ana mtoto wa miaka mitano, anategemea aje amrithishe hilo shamba. Kwa hiyo, likae pori miaka yote hiyo kwa sababu ya mtoto wake akue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, nami nakuamini sana uchapakaji kazi wako tunaujua, Naibu wako tunamfahamu ni mchapaji kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja na nina imani migogoro itaenda kwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)