Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu katika hii Wizara ya Ardhi. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, kwanza kwa kuondoa riba na kwa kuwaongezea wananchi muda wa kuweza kulipa. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Makatibu pamoja na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache tu ambayo nataka nichangie yanayohusu jimboni kwangu. Kwanza kuna jambo moja ambalo linaendelea jimboni kwangu kuhusiana na urasimishaji. Mheshimiwa Waziri jambo la urasimishaji tunalipenda kwa sababu linawasaidia wananchi ili waweze kupata hati. Sasa jambo hili limekuwa kero. Tumefanya mikutano na hizi kampuni ambazo zinakuja kwa wananchi katika kata nyingi sana, ukianzia Kata ya Minazi Mirefu, Kata ya Tabata, Kinyerezi, Kiwalani, mpaka leo hawa wananchi hawajapata hati zao. Hizo kampuni ambazo zinakuja kwa ajili ya urasimishaji zinachukua muda mrefu sana, halafu tunapokuwa tunaenda kufanya mikutano yetu, kwa mfano, kama Diwani au Mbunge anafanya mkutano, basi kero kubwa za wananchi kwa Jimbo la Segerea ni kuhusiana na kampuni za urasimishaji. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba sana Mheshimiwa Waziri hili jambo ulifuatilie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linaendelea katika Jimbo la Segerea ni kuhusiana na uwanja. Mheshimiwa Waziri unajua na ninafikiri nilikwambia, tuna uwanja wetu ambao ulikuwa unaitwa kwa jina la maarufu Uwanja wa Sigara. Huu ni uwanja ambao uko Kata ya Liwiti. Huu uwanja umekuwa unatumiwa na wanafunzi na watu mbalimbali katika mambo mbalimbali ya michezo kufanya mazoezi na watu wengine ambao wana shughuli mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2020 kuna mtu alijitokeza akasema kwamba hili eneo ni lake, lakini kipindi kile tuliweza kuzuia na akaondoka, lakini sasa Mheshimiwa Waziri kwa kipindi hiki mwezi wa Nne ambapo tuko hapa Bungeni, nasikia tayari huyo mtu ameishajitokeza katika Uwanja wa Sigara, na hivi ninavyokwambia, ameshapeleka grader limesafisha kabisa ule uwanja. Kwa hiyo, sehemu ambazo zilikuwa zinatumika kwa ajili ya mambo ya michezo na mazoezi mbalimbali, huu uwanja sasa hivi haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kata ya Liwiti pamoja na Jimbo la Segerea walitaka wajue, hili eneo lilikuwa ni eneo la wazi, inakuaje mtu anajitokeza na anasema ni eneo lake na anapeleka grader linaanza kufanya kazi na vyombo na Serikali ipo tu inaangalia. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri utusaidie tuweze kupata majibu ili pia tuweze kuwaambia wananchi, ni jambo gani linaendelea katika Uwanja wa Sigara? Kwa sababu ni wengi ambao tunalalamika na huu uwanja una kazi nyingi za kiserikali zinafanyika hapo. Kwa sasa hivi hatuwezi kufanya kitu chochote kwa sababu tayari ameshaenda pale, amepeleka grader, ameshaanza kuziba, hakuna kitu chochote ambacho kinaendelea. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri ufuatilie jambo hilo, utakapokuja kufanya wind-up uweze kutuelezea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye Kata hiyo hiyo ya Liwiti, kuna wananchi karibu 1,800 Mtaa wa Amani Ladwa. Hawa wananchi 1,800 Mheshimiwa Waziri wote wana leseni za makazi, lakini wote wamewekewa huduma za jamii kwa maana ya maji, umeme na vitu vingine ambavyo vinahusisha huduma ya jamii. Jambo la kushangaza na la kusikitisha, ametokea mwananchi anasema kwamba lile eneo lote ni la kwake. Kwa hiyo, anahitaji wananchi wahame au wasipohama waweze kumlipa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa wamekaa kwenye hiyo sehemu kwa miaka 40, kuna watu wapo wanasomesha watoto, kuna watu wanasomesha wajukuu, imekuwaje siku zote hizo huyo mtu asijitokeze, mpaka leo baada ya miaka 40 ndiyo aje kusema hilo ni eneo lake? Tulikuwa tunaomba Waziri uingilie huu mgogoro ili watu waweze kujua ni jambo gani linaendelea katika huu mtaa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kusema kwamba hivi anavunja sheria, kwa sababu hatujajua. Kwa sababu huwezi kujua, watu wamekaa miaka 40 na wanalipa leseni, wana huduma zote za kijamii. Kama watu wangejua kwamba hili eneo siyo lao au Serikali ingekuwa inajua kwamba hili siyo eneo la hawa watu, ina maana hata hizo huduma za kijamii wasingewekewa, na ni watu 1,800 Mheshimiwa Waziri na huyu ni mtu mmoja. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iweze kuingilia kati, tuangalie ni jinsi gani mnaweza mkawakomboa hawa wananchi. Kwa sababu hakuna mtu ambaye anaweza kuwahamisha wananchi 1,800 yeye akiwa peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kwenye Jimbo la Segerea nina kata kama nne ambazo ndiyo zenye makazi holela. Amezungumzia hapo mjumbe aliyemaliza. Tuna Kata ya Vingunguti, tuna Kata ya Buguruni, na Kata ya Mnyamani. Kwa hiyo, tulikuwa tunasubiri huo mradi ambao mna-plan kwenye miji ili nasi tuweze kufaidika. Kama unavyojua, Vingunguti, Buguruni pamoja na Mnyamani ni karibu sana na mjini. Kwa hiyo, tunaomba katika huo mradi ambao mtauanza wa ku-plan miji, basi na hizi kata zetu tatu mweze kuziingiza ili wananchi hawa nao waweze kufaidika, kwa sababu wanakaa mjini, pamoja na kwamba sasa hivi hawana uwezo wa kujenga nyumba zao, lakini najua Serikali mnaweza mkatengeneza mradi pale, wananchi wakafaidika na Serikali ikafaidika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, kwa hiyo, naomba masuala yangu matatu yaweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)