Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipatia nafasi ya kuchangia. Pili, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dokta Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya na kwa kutenga fedha kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Waziri Dokta Angeline Mabula, Naibu Waziri wake Mheshimiwa Pinda, Katibu Mkuu Injinia Sanga, Naibu pamoja na Wizara nzima kwa ujumla kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ni mali, ardhi ni vizuri tuitunze, ardhi tuithamini kwa sababu watu wanaongezeka lakini ardhi haiongezeki. Kila mmoja anaongelea migogoro, kila mmoja anatamani ardhi yake iweze kupimwa. Namuomba Mheshimiwa Waziri aangalie suala la upimaji wa ardhi ili kusudi tuweze kwenda vizuri kadri tunavyokwenda kwa sababu ardhi haiongezeki lakini binadamu wanaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Morogoro. Nyote mnaamini kuwa Mkoa wa Morogoro unaongoza kwenye migogoro ya ardhi. Mheshimiwa Waziri wewe ni shahidi, naamini ulishafika Mkoa wa Morogoro, Mawaziri wengine wengine wamefika kwenye Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Mkoa ameweza kutatua migogoro ya Morogoro, Wakuu wa Wilaya wameweza kutatua migogoro na wataalam lakini migogoro bado iko hapo hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hii migogoro hasa ninayoisema kwa Mkoa wa Morogoro hasa ni kwa upande wa wakulima na wafugaji. Ninaomba Mheshimiwa Waziri wa upande wa Ardhi uweze kushirikiana na upande wa Wizara ya Mifugo muweze kutatua tatizo hili ambalo limekuwa sugu kwenye Mkoa wetu wa Morogoro. Migogoro hii ya ardhi ambayo iko kwenye upande wa wakulima na wafugaji iko kwenye Wilaya zote za Mkoa wa Morogoro ikiwepo Malinyi, ikiwepo Kilombero, hasa Kilombero ni hatari sana kwa sababu iko kwenye Bonde la Kilombero. Kwenye Bonde hili la Kilombero ndiyo linatoa maji ambayo yanakwenda kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo, kama litaharibika hatutaweza kupata maji ya kutosha na umeme hatutaweza kupata umeme wa kuzalisha umeme kwenye bwawa hili. Kwa hiyo naomba muiangalie. Mvomero pamoja na Wilaya zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaacha kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa jitihada alizozifanya kwa Mkoa wetu wa Morogoro, licha ya matatizo hayo lakini angalau ameweza kupima maeneo machache kwenye Mkoa wetu wa Morogoro kwenye Wilaya mbalimbali ikiwepo Wilaya ya Malinyi, Kilombero, Ulanga na Kilosa pamoja na Mvomero lakini upimaji umesimama, ninaomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kujibu pale tuweze kujua kuwa upimaji huu unaendelea lini? Kwa sababu migogoro bado inaendelea na kutatua migogoro hii ni kupima ardhi kwa sababu ukipima ardhi watu watajua watapata hati miliki yao na wataweza kuwa na ardhi yao na wataweza kuzitumia bila ya mgogoro. Wakulima watakuwa na ardhi yao na wafugaji watakuwa na ardhi yao, itakuwa hakuna kuingiliana. Kwa hiyo, ningeliomba kujua ni lini upimaji tena utaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikifuatia hapo pia naongelea kuhusu vyuo vyetu vya ardhi ikiwepo Chuo cha Tabora pamoja na Chuo cha Morogoro na Chuo Kikuu cha Ardhi cha Dar es Salaam. Naomba sana kwa sababu wataalam inaonekana kuwa wanahitimu na wataalamu hawatoshi. Naomba udahili hasa kwenye vyuo vya kati uweze kueleweka, uweze kudahiliwa wanafunzi wengi kwa sababu hawa wa vyuo vya kati hasa ndiyo wanafanya sana upimaji wa ardhi, kusudi waweze kuajiriwa na tuweze kupata wataalam kwa sababu matatizo haya ya ardhi yatakwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kusema kuwa utafiti wa migogoro wala siyo utafiti, migogoro inayoeleweka, huu utafiti wa kubainisha hii ardhi uweze kufanyika kwa sababu ili tuende na sayansi na teknolojia lazima tufanye utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba kuongelea bajeti. Bajeti inatolewa lakini naomba bajeti ya maendeleo iweze kuangaliwa kwa sababu hii bajeti licha ya kuongeza fedha na kutupatia fedha ndiyo ikitolewa kwa wakati na fedha zote tunazoziidhinisha humu Bungeni zikatolewa kwa wakati na zikatolewa zote miradi yote ya maendeleo ikiwepo upimaji wa ardhi itaweza kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kusema kuwa namsihi sana Mheshimiwa Waziri uliangalie hili suala la upimaji wa ardhi kwenye nchi yetu nzima, kusudi tuondokane na hii migogoro ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nakushukuru na Mwenyezi Mungu akubariki. (Makofi)