Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii jioni ya leo ili nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi. Naomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha mimi jioni hii kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kama ilivyo ada nami naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa yale yote ambayo ameyafanya katika Wizara hii. Sisi ni mashahidi hadi mwezi Mei Wizara hii imepata asilimia 82 ya makisio yake, lakini wote sisi ni mashahidi tumeona jinsi gani Mama Samia Suluhu Hassan alivyokuwa na uchungu na wananchi wake na kusamehe madeni yale ya nyuma ili wananchi waendelee kulipa katika muda unaokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Mheshimiwa Rais ameweza kutafuta fedha nyingi karibu bilioni 345 na kuwakabidhi Wizara ya Ardhi ili Wizara hii iweze kutenda yale ambayo wananchi wanayatarajia. Ni matarajio yangu kuwa watendaji watazitumia fedha hizi vizuri sana ili wananchi waweze kuona matokeo ya fedha zao. Sina shaka kabisa na Mtendaji Mkuu wa Wizara ndugu yangu Sanga, uaminifu wake, uadilifu wake unajulikana huko alikotoka na nina imani ataitendea haki Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, namshukuru tena Mheshimiwa Rais kwa kuunda ile Kamati ya Mawaziri Nane wa Kisekta ambao wamezunguka Tanzania nzima kutafuta majawabu ya matatizo ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa naomba nijielekeze katika mchango wangu. Mheshimiwa Rais aliunda Wizara ya Kisekta ya Mawaziri Nane, Mawaziri hawa walitembea almost katika nchi yote hii na bahati nzuri katika Mkoa wa Mtwara walifika. Mheshimiwa Waziri yeye ni shahidi tulikuwa naye pale Mtwara na tulikutana nae. Yeye ni shahidi aliona jinsi gani watendaji wake walivyofanya kazi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kushangaza sana sisi Wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi hatukushirikishwa kabisa katika mchakato huu. Ndani ya wilaya yangu, Kata ya Mkonona Vitongoji vya Wanika, Kitongoji cha Nambunda na Malomba. Vitongoji hivi vimehusika kabisa katika mchakato mzima wa kuhakikisha kwamba wananchi walipo ndani ya eneo hili wanahamishwa na kutafutiwa makazi katika eneo lingine. Cha kushangaza halmashauri kwa maana ya Madiwani sisi hatukushirikishwa hata siku moja. Kwa hiyo, kila kitu kilifanyika siri na Mheshimiwa Waziri mwenyewe ni shahidi na alishangaa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Mtwara alipogundua jambo hili alitumia hekima kubwa na kulimaliza jambo hili kwa busara sana na tukashiriki kikamilifu, tukaondoka sisi, Wabunge na Kamati nzima ya Waziri mpaka katika eneo la tukio na aliona jinsi wananchi wasiopungua 10,000 wako pale ndani ya eneo wakisubiri maamuzi ya Serikali. Sasa Serikali imeshafanya maamuzi na sisi hatuna tatizo na maamuzi na Waziri ameikabidhi Serikali ya Mkoa iandae mchakato mzima. Najiuliza Serikali ya mkoa wanazo nyezo za kufanyia kazi maamuzi ya Waziri. Serikali ya Mkoa wamefanya tathmini ya wananchi wahame, wamewatafutia maeneo wananchi waende, lakini mpaka sasa hivi wananchi wale wanasubiri fidia ambayo ndani ya ripoti ya wataalam wamezungumza bayana kwamba wananchi wapewe fidia ili wahamie maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri, Wizara ifanye maamuzi sasa na sina uhakika kama ndani ya bajeti hii wale wananchi wa Wanika na Malomba, Nambunda wametengewa fedha ili waondoke katika maeneo hayo na waende katika yale maeneo ambayo wamepangiwa. Kama eneo hili halitashughulikiwa kesho nitatoa shilingi. Sitakubali wananchi wale waendelee kukaa miaka saba wakisubiri maamuzi ya Serikali, tunawatia umaskini wananchi wale. Kwa hiyo kesho Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze wananchi wale lini watalipwa fedha zao ili waende eneo ambalo Serikali ya Mkoa imeshawapangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili ni suala la migogoro. Migogoro imekuwa karibu kila mahali katika nchi hii na ndani ya Wilaya yangu ya Nanyumbu migogoro ipo. Naishukuru sana Wizara katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri ameeleza jinsi gani ya kuweza kupunguza migogoro na ni kweli ndani ya wilaya yangu mimi nina masikitiko makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ile hatuna Baraza la Ardhi la Wilaya, matatizo yetu yanakwenda kilometa 100 ups and down mwananchi anapopata matatizo ndani ya Wilaya ya Nanyumbu inabidi aende Masasi ambapo ndipo kuna Baraza la Ardhi, jambo hili linakwamisha utoaji wa haki kwa wananchi, jambo hili pia linasababisha wale wenye fedha ndiyo wanapata haki, kwa sababu mgogoro uko Nanyumbu, kesi iko kilometa 50, huyu mwananchi maskini ataweza kwenda kilometa 50?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana kwa kuamua kuunda Mabaraza ya Ardhi kwa kila Wilaya, wasiwasi wangu naomba kesho utakapokuja unithibitishie, Wilaya ya Nanyumbu Baraza la Ardhi litakuwepo katika mwaka ujao wa fedha? Vinginevyo kesho patakuwa matatizo makubwa Mheshimiwa Waziri, sitakubali tupite tena mwaka mwingine bila kuwa na Baraza la Ardhi la Wilaya ya Nanyumbu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasaema hivyo kwa sababu wananchi wanahangaika, leo unapigiwa Mbunge fedha umsaidie kwenda kwenye kesi Masasi, hili jambo siyo sawa hata kidogo. Kwa hiyo, lazima tuwasaidie wananchi wetu katika kutafuta haki vinginevyo watakuwa wanapata haki wale watu ambao wana fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda sana kulizungumzia hapa ni haya makampuni yanayopewa kazi kuja kufanya shughuli za upimaji katika maeneo yetu. Tunayo kampuni ambayo ilikuja kufanya upimaji wa ardhi katika maeneo yetu ili wananchi baadae wapate hati, ile kampuni mpaka leo imefanya ile kazi, wananchi hawajapata hati na wananchi wanahangaika. Jambo hili nilishalifikisha ndani ya Wizara na Wizara ikaahidi, tena kampuni yenyewe ni ya Serikali, Chuo cha Ardhi Morogoro lakini cha kushangaza mpaka leo wananchi wale wanahangaika, wananchi wale nikifika tu kutoka Dodoma wanajaa ofisini kwangu kuomba kujua ufafanuzi wa hatma yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakuomba sana, naiomba sana Wizara haya ambayo Wabunge tunashauri wayafanyie kazi. Kampuni hii kama kweli ipo, basi ilete hati ambazo wananchi wale wamechanga fedha zao na wanahitaji sasa kupata hati ili mambo yao yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuhusu hati za kimila; hati za kimila zinatolewa, Mheshimiwa Waziri amezungumza kwamba unaweza ukaitumia hati ya kimila kupata mikopo. Mimi naomba anithibitishie hili, kesho atakapokuja kuhitimisha anielezee tu wananchi japo wanne wa Wilaya ya Nanyumbu ambao wana hati za kimila, wamepata mikopo katika benki zetu, vinginevyo tutakuwa tunadanganyana, tuelezwe ukweli hati za kimila, dhamira yake ni nini? Ukipata hati ya kimila, unapata mkopo? Lakini siyo unanipa karatasi ambayo mimi haina manufaa yoyote, kwa hiyo naiomba sana Wizara kesho ituthibitishie hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naiunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)