Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya mimi kuwa mchangiaji katika hotuba ya bajeti ya Wizara hii muhimu ya Ardhi ambayo kimsingi imeshika hatma ya Wabunge wengi ndani ya Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mtovu wa fadhila kama sitaanza mchango wangu kwa kumshukuru Rais wetu Mama yetu Samia Suluhu Hassan pamoja na Watendaji wake wa Wizara ya Ardhi kwa jitihada ambazo wanazionesha kuziwezesha Halmashauri zetu kupata fedha kwa ajili ya kupima maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya Halmashauri ambazo zimefaidika na fedha hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na Jimbo la Mikumi hasa pale Makao Makuu ya Jimbo la Mikumi, tumepata fedha za kutosha ambapo tumepima viwanja zaidi ya 2,000. Hatujawahi kupima tangu uhuru na zoezi hili linaashiria commitment ya Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba ifikapo 2025 asilimia 50 ya maeneo ya nchi yetu yatakuwa yamepimwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo pale Ruaha kuna Miji ambayo inakua kwa kasi sana peri urban, Tanzania nzima ukienda ambazo watu wanawahi kujenga kabla ya Serikali kufika kupima, kupanga na kumilikisha. Matokeo yake ni nini? Tunaona slams zinatengenezwa halafu Serikali inakuja baadae kurasimisha, sasa ni mapendekezo yangu kwamba ni vema fedha ambazo tumezipata kama mkopo kuhakikisha kwamba tunaenda kupima maeneo yote ili wananchi wanapofika au wanapohitaji ardhi waende kwenye maeneo ambayo yamepimwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mpango wa matumizi bora ya ardhi, Watanzania wanaongezeka na tunazaliana kweli, lakini ardhi ya Tanzania haiwezi kuongezeka na haitakuja kuongezeka. Namna tunavyoenenda ni kana kwamba tuna nafasi ya kuongeza ardhi ya Tanzania, namna ya ujenzi wa majengo yetu tunayojenga hata hapa Dodoma, tunaweza kuona wazee wetu miaka ya 1970 walivyotengeneza Mji wa Area D, pale kuna Site One, Site Two, kuna Site Three lakini unaanza kujiuliza Site Four, Site Five, Site Six ziko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona maeneo yamepimwa katika viwanja vidogovidogo vya square meter 200, 300, 400 hivi haturudi nyuma kujiuliza wale wazee wakati huo miaka ya 1970, 1980 wakati Dodoma sehemu kubwa ikiwa Jangwa ikiwa pori hawakuona sababu ya kujenga hivi vibanda ambavyo tunavijenga katika kila mtaa? Kwa nini walijenga magorofa pale Area D, ambayo yamekaa kimpango ambayo sasa hivi hayapatikana kila Mbunge anatamani kwenda kukaa pale na hawapati nafasi, lakini ni mawazo ya watu ambao walitutangulia. Kwa hiyo, suala la uendelezaji wa makazi ni muhimu kama lilivyo suala la kupima, kupanga na kuendeleza ardhi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili hatuwezi kulifikia kwa kutegemea fedha na bajeti ya Serikali. Ni vizuri Serikali ikakaa ikatafakari namna bora ya kushirikisha sekta binafsi, kuziwezesha, kuweka incentive wajenge majengo mengi kwa gharama nafuu ili iwe gharama kubwa kwa mtu kujenga nyumba yake binafsi badala ya kununua apartment, kwa kufanya hivyo Serikali itakuwa imepanga watu wake, inaweza ikakusanya mapato makubwa zaidi kwa sababu wanakaa katika maeneo ambayo yanaeleweka na kufahamika ambayo yamepimwa na yana hati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu suala la migogoro. Sisi watu wa Kilosa tuna migogoro ya ardhi katika maeneo mawili. Moja, kati ya wafugaji na wakulima; na pili, kati ya hifadhi na wananchi. Tunashukuru kuna jitihada za Serikali ambazo zinaendelea kufanyika. Kipekee kabisa namshukuru Kamishna wa Ardhi wa Mkoa wa Morogoro, ndugu yangu Frank, amejitahidi na anajitahidi na hata wiki iliyopita alikuwa katika vijiji kwa ajili ya kuondoa changamoto kati ya wananchi na mipaka ya vijiji kule Ukwiva na Paulanga katika Kata ya Kisanga lakini pia Kata ya Ulaya na kule Kilangali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro hii iko katika kila sehemu ya Tanzania. Ziara ya Mawaziri nane walikuja Morogoro, kwa bahati mbaya hawakufika Mikumi, na sina hakika kama watakuwa na uwezo ama watakuja kuwa na nafasi ya kupita katika kila eneo la Tanzania. Ni vizuri tukaweka mifumo ambapo kila mmoja kwa nafasi yake aiheshimu. Wananchi pale wanalalamika kwamba mipaka ya TFS, mipaka ya hifadhi inahama. Kwa nini mipaka ya hifadhi ihame? Kwa nini kuwe na ramani zaidi ya tatu ambazo zinatafsiri mipaka tofauti? Kuna GN ngapi kwenye hii nchi? Kuna Serikali ngapi ambazo zinaweza zikafanya maamuzi ya mipaka kati ya wananchi na hifadhi na kati ya wananchi na vijiji? Kwa hiyo, ni vizuri tukaangalia suala zima la GN na mipaka katika jitihada za kutatua migogoro kati ya wananchi na hifadhi na kati ya wafugaji na wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la matumizi bora ya ardhi. Kuna changamoto. Kuna Wabunge wamechangia suala hili, lakini mimi nina mfano. Pale Kata ya Zombo kwenye Jimbo la Mikumi, kuna Sheria ya Matumizi Bora ya Ardhi na wananchi wametengeneza utaratibu wao, lakini wanapochukua hatua hawapati support ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Kwa mfano, Machi, 2022 kulikuwa na wimbi la ng’ombe zaidi ya 2,000 zilivamia mashamba ya watu, wakatozwa kwa sababu hawakufuata Sheria ya matumizi bora ya ardhi. Polisi wakaingilia. Mpaka leo faini halali ambayo imetozwa na Kijiji haijalipwa, na hakuna jitihada ambazo zinaonesha kwamba kuna usimamizi wa Sheria ambayo imewekwa na wanakijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatuwezi kuheshimu sheria ambayo imewekwa na mamlaka ya Kijiji: Je, ni sheria zipi ambazo tunaweza kuziheshimu? Tutambue kwamba Serikali ya Kijiji ni Serikali kamili, ni Serikali ambayo iko kikatiba, ni Serikali ambayo ina kauli thabiti na lazima iheshimiwe na vyombo vyetu lazima visaidie Serikali za Vijiji katika utekelezaji wa maamuzi ya Serikali za Vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni maeneo ya huduma za jamii, yanahangaikia kodi. Tunatoza kodi kubwa kwenye maeneo ya huduma za jamii kama hospitali, kama shule. Pale Mikumi kuna hospitali ya St. Kizito ambayo ni hospitali teule inayohudumia wananchi wa kipato cha chini pale katika Jimbo la Mikumi, Wilaya ya Kilosa na maeneo ya jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi ya ardhi ambayo wanatozwa ambapo kimsingi anatozwa mgonjwa ni kubwa sana ambayo inakwenda kudumaza ubora wa huduma ambazo zinatolewa na hiyo hospitali. Ni vizuri Serikali ikaangalia maeneo ambayo yanatoa huduma kama siyo chanzo kikuu cha mapato kupitia ardhi. Kwa sababu unapotoza kodi ya ardhi katika maeneo hayo, maana yake unamtoza mgonjwa ama mwanafunzi ambaye anahudumiwa ama anapata huduma kutoka kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni Sheria Na. 7 ya Ardhi ambayo inatambua Serikali za Mitaa kama Msimamizi wa Kupima, Kupanga na Kumilikisha. Kwenye eneo hili tunaona masterplan mbalimbali na maeneo mengine hayana masterplan, lakini hata maeneo ambayo yana masterplan unaona kinachojengwa ama kinachoendelezwa ni contrary na masterplan. Sasa, hapa nani tumchune ngozi? Ni Wizara ya Ardhi ambayo ina dhamana ya kusimamia ama Wizara ya TAMISEMI ambayo ina wajibu wa kusimamia Sheria hii Na. 7?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili napenda nishauri suala zima la mawasiliano na mahusiano kati ya taasisi na Wizara za Serikali. Ni vizuri Wizara ya Ardhi, Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Maliasili zikawa na mawasiliano ya karibu katika kusimamia na kuendeleza ardhi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kuona hata ile asilimia 30 ya retention fee ambayo ilikuwa inarudi katika halmashauri kama incentive ya kuendelea kusimamia ardhi, hairudi tena. Matokeo yake yamekwenda kufubaza jitihada za halmashauri katika kusimamia suala la ardhi katika halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutazungumza kwamba Serikali ni moja, ni vizuri kukawa na uratibu hasa linapokuja suala la ardhi. Kinachoendelea katika maeneo mbalimbali ya halmashauri zetu hakiakisi ukweli kwamba tunaishi katika karne ya
21. Ukienda kwenye maeneo ya taasisi mbalimbali za Serikali, unaweza kuona nyumba ambazo zimejengwa miaka ya 50, 60, 70, zimejengwa siyo kwa gharama lakini zimejengwa kwa mpango na zinavutia. Ukiangalia kile ambacho kinafanyika sasa hivi, viwanja vinavyomegwa, viwanja vinavyogwanywa, haviakisi uhalisia kwamba ardhi hii tumepewa kizazi hiki kama dharama kwa ajili ya kurithisha watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalize kwa kusema kwamba, ni vema tuka – review Sera ya Ardhi ya Mwaka 1995. Je, itatupeleka tunakotaka kwenda? Watanzania wanaongezeka na sensa tumeiona. Hii sensa ina-reflect vipi katika mikakati ya halmashauri kwenda kutimiza malengo yake, kupima maeneo yote na kuendeleza miji midogo midogo, kwa mfano, Mikumi, Ruaha, Kibodi, Ulaya na Masanze? Haya yote ni maeneo ambayo yanakua kwa kasi na tunahitaji Serikali kuona inachangia vipi katika kupima, kupanga na kumilikisha ili watu wasiende kujenga bila utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)