Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipatia nafasi na mimi kutoa mchango wangu kwenye Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimekuwa nikisema awali, mimi ni mdau lakini nimekuwa mtumishi zaidi ya miaka kumi kwenye Wizara hii. Kwa hiyo, nikisimama huwa napenda ni-declare interest kwa maana kwamba Wizara hii ndiyo imenilea, maoni yangu na ushauri wangu nitatoa kulingana na taaluma yangu niliyonayo kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anapambana. Anatusaidia Wabunge lakini lengo lake ni jema kuhakikisha angalau kunakuwa kuna ustawi kwenye sekta ya ardhi kupunguza migogoro, angalau ardhi sasa iwe katika sehemu, itumike kama sehemu ya uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya, natambua changamoto zipo nyingi lakini kwa kuwa Wizara ndiyo Wizara Mama na inabeba sekta nyingi lazima mkutane nayo na nichukue nafasi hii kuwapongeza sana namna mnavyopambana kuhakikisha mnayatatua yale ambayo yanapaswa na mnaweza kuyafanyia kazi. Niwapongeze Watumishi ndani ya Wizara hii kwa namna ambavyo na wao wanaendelea kuhakikisha angalau nia na dhamira ya Mheshimiwa Rais inatimia kwa wakati wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema naunga mkono hoja mapendekezo ya Kamati yale yote yaliyotolewa na ninaamini kabisa yanatoka kwa nia njema Wizara imesikia na Serikali imesikia itakwenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo mawili leo ya kuchangia, kwanza ningetamani sana nichangie kuhusu chanzo cha migogoro nchini. Kwa study yangu ya kawaida tu inaniambia kwamba moja ya sababu ambayo inaweza kuwa inasababisha migogoro kwa sasa kwenye Taifa letu Tanzania ni kupitwa kwa sera ya ardhi na maendeleo ya makazi hilo ni la kwanza kabisa kwa sababu sera tunayoitumia ni ya mwaka 1995 haiendani na kasi ya uzalishaji na shughuli za kiuchumi za wananchi wanazofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, population iliyokuwa wakati sera inatungwa 1995 haiwezi kuwa sawa na population ya sasa na namna ya shughuli za uzalishaji zinavyofanyika. Kwa hiyo, kwa namna moja au nyingine lazima kutakuwa na mwingiliano wa namna moja kwenda sehemu moja na sehemu nyingine. Pili ni kukosekana kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye ngazi za vijiji. Hili na lenyewe linaweza likawa linachangia kwa kiasi kikubwa sana; na jambo la tatu ni muingiliano wa Wizara za Kisekta, muingiliano kati ya Wizara ya Ardhi, Maliasili na TAMISEMI. Haya yote ya muingiliano huu wa shughuli za kiuchumi zinazofanyika yanatokana na kutokuwa na sera iliyopitwa na wakati. Ndiyo maana mimi nimekuwa nikikuomba sana kwamba jitahidi sana kwa namna moja inayowezekana sera ya ardhi ndiyo chimbuko na solution kubwa inayoweza kutatua changamoto hizi ambazo zinajitokeza kati ya muingiliano wa Wizara na Wizara lakini pia na maeneo ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo hapa kuhusiana na migogoro. Utakubaliana na mimi, migogoro mingi ya ardhi kwenye maeneo mengi kwanza inatugombanisha Wabunge na wananchi lakini mbili inaigombanisha Serikali na wananchi, tatu inagombanisha Chama na wananchi, pia inagombanisha kati ya jamii moja ya wananchi sehemu moja na sehemu nyingine. Sasa kwa namna tunavyokwenda na kutatua migogoro tumeona migogoro mingine pia inatugombanisha kati ya Wabunge na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kutokana na maelekezo wanayopewa ya kusimamia na kutatua ile migogoro na wengine hatupendi haya yatokee, kwa hiyo hii Mheshimiwa Waziri lazima uitazame sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano kwangu Rorya nina mgogoro, siwezi kuita ni mgogoro ni sintofahamu ya eneo la Utegi kati ya Kitongoji cha Kiwandani na Begi. Siwezi kuita mgogoro kwa sababu katika vijiji 975 vilivyoainishwa vyenya mgogoro nchini ambavyo Mawaziri wanapita hivi vitongoji havimo, lakini unaweza ukaona sasa hivi tumekwenda tumetengeneza taharuki pale, tunawaambia wale wananchi zaidi ya kaya 300, wananchi zaidi ya 1,200 wahame hawalipwi fidia wanalipwa uwezeshaji peke yake, sasa tunataka kutengeneza mgogoro ambao hauna tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nichukue nafasi kukuomba sana Mheshimiwa Waziri kwa kipekee kabisa naamini hili unaliweza, jambo la kwanza twende na maoni ya wananchi wanacho sema. Wananchi wanasema kabla hatujafika huko, kwanza tusimamie Sheria ya kushirikishwa kwenye mikutano waambiwe dhumuni ni nini la wananchi kuondoka eneo lile na hii ndiyo Sheria ya uthamini inavyotaka. Ningeomba sana hili lifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili wananchi hawa wasingependa uendelee utaratibu wa kuitwa wao ni wavamizi, wana miaka zaidi ya 60 pale, wana miaka zaidi ya 70. Shule ya Msingi pale imejengwa toka mwaka 1959, tukiwaita wavamizi kwamba waondoke bila kuwalipa tunakwenda kutengeneza mgogoro mwingine na lengo la Wizara ni kupunguza na kuzuia mgogoro, mimi kama Mbunge nisingependa kwenye kipindi changu hiki nizalishe mgogoro kwenye Wilaya yangu ya Rorya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo manufaa mengi ambayo tumeyapata kupitia kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Rais, tumepata maji, tumepata miundombinu ya barabara, nisingetamani tena tuende tukatengeneze mgogoro mwingine ambao utanikwamisha mimi kama Mbunge kutimiza wajibu wangu. Mheshimiwa Waziri ndiyo maana naomba sana haya matatu ambayo wananchi wanaomba, moja kushirikishwa kwenye vikao, mbili kutokuitwa hili jina, lakini tatu ikibainika wanatakiwa kuhama walipwe fidia stahiki kwa mujibu wa Sheria. Wale wananchi hawajagoma lakini wanachogoma ni ushirikishwaji na wanavyoona namna wanavyotaka kupelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri utakubaliana na mimi kabla tunakwenda kutamka juzi hakuna kiongozi aliyewahi kwenda kukaa nao wale wananchi akawaambia ABC, kwa hiyo ukija ukitamka vile maana yake unakwenda kutengeneza mgogoro mwingine ambao hauna tija na hauna afya kabisa kwenye Wilaya yangu ya Rorya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, lipo jambo linazungumzwa hapa na mimi niombe sana Mheshimiwa Waziri chukulia hii changamoto siwezi kuita changamoto, chukulia haya maoni ya Waheshimiwa Wabunge yanayotoka ndani ya Bunge kama ni sehemu ya kukutakia mema na wanakupenda sana na mimi nitajenga hoja kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ukurasa wa 120, Ibara ya 74 inasema, kwa miaka mitano kwa maana ya 2020 mpaka 2025, vijiji vinavyotakiwa kupangiwa matumizi bora ya ardhi ni 4,131 Ilani inatamka. Mpango wa Tatu wa maendeleo unasema angalau kufika 2025/2026 tuwe tumepanga matumizi bora ya ardhi. Naomba hapo nieleweke, kupanga matumizi bora ya ardhi sizungumzii kupima. Kupanga matumizi bora ya ardhi angalau kufikia asilimia 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hapa ndani alipokuwa anahutubia Bunge alikazia hili kwamba angalau kufika 2025 tuwe tumepanga matumizi bora ya ardhi ya asilimia 50 ya vijiji vyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji tulivyonavyo sasa ni 12,318, tulivyopanga toka uhuru ni elfu mbili mia nane kumi na kitu, maana yake ni asilimia 23 peke yake, lakini kwa miaka mitatu ilikuendana na Ilani, ilikuendana na mpango, ili kuendana na maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa miaka mitatu tumepanga vijiji 681 peke yake. Wabunge wanachosema Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa haya yote tunatambua ambao tumekuwa kwenye Wizara hii muda mrefu tunajua yote haya yamekuwa ni changamoto kwa sababu ya ukosefu wa fedha, tunashindwa kutimiza haya matatu ambayo ni maelekezo kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri sasa umepata fedha, tumepewa mkopo zaidi ya bilioni 345 tunachotakiwa pale ni kutenga bilioni 60 peke yake unakwenda kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kupanga vijiji vyote 4,131, unakwenda kutekeleza mpango wa tatu wa uchaguzi, unakwenda kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais lakini utakwenda kutengeneza legacy kubwa sana kwenye nchi hii kwa sababu kutoka uhuru wewe ndiyo utakuwa umepanga matumizi ya vijiji vingi kuliko wakati mwingine wowote, utakuwa umetengeneza legacy kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais. Kwa sababu kama toka uhuru tunazungumza vijiji 2,600 tukipeana miaka mitano sasa tukapanga vijiji elfu nne na kidogo maana yake Mheshimiwa Waziri unakwenda kutengeneza legacy na wataalam ambao tuko kwenye sekta ya ardhi hatutakusahau kwenye hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ndiyo maana, mimi nikuombe maoni yote ya Waheshimiwa Wabunge yanayotolewa humu yachukue kama sehemu ya kuboresha ili angalau tuende tufike mahali fulani. Tunaamini uwezo wako, tunaamini unaliweza hili, kama utachukua haya yanayozungumzwa ukafanya adjustment ya ule mkopo, uka- impose fedha kwenye Tume ya Mipango, ukaipa maelekezo kuhakikisha wanapanga matumizi bora ya vijiji hivi kupunguza migogoro, utakuwa umefanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuambie Mheshimwa Waziri migogoro hii haina tija kwetu kwanza kama nilivyosema inatugombanisha na wananchi lakini kutokupanga matumizi maana yake umepunguza thamani ya kile Kijiji chenye ardhi, lakini pili inatusumbua sana wanapokuja wawekezaji. Leo akija mwekezaji ambaye anataka kuwekeza Wilaya ya Roya hatuna land bank, hakuna mahali anapofika akaambiwa hili eneo ni kwa ajili ya viwanda ukienda Wilaya ya Rorya, hili ni kwa ajili ya kilimo, hili ni kwa ajili ya ufugaji, hili huwezi kwenda kwa sababu kuna hifadhi, kwa sababu eneo lote limepangwa matumizi halisi, hiyo land bank hakuna kwa hiyo Mheshimiwa Waziri mimi nikuombe sana kwa unyenyekevu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yanayozungumzwa kwa sababu yamezungumzwa na Kamati, tumeyashauri mwaka jana tumeyashauri mwaka huu kama kuna uwezekano wa kufanya adjustment ya mkopo huu ili kuleta maslahai ya Taifa, ili kwenda kugusa maeneo mengi, kupunguza migogoro ya Wabunge wanayozungumza humu, ningetamani sana ulione hili na hili linkwenda kukubeba mimi nikutie moyo kwa namna yoyote hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na kama kuna mtu anakwambia hili litakuharibikia haliwezi, ndiyo maana nikasema unakwenda kutengeneza historia kwa kupunguza migogoro ya wananchi wanaumizana kule nje. Mheshimiwa Waziri mimi naamini sidhani kama unapendezwa leo tuko hapa ndani unasikia kati ya mkulima na mfugaji wanapigana, unasikia kati ya maeneo ya hifadhi wananchi wameingilia. Kuna maeneo ya vishoroba ambayo Tembo wanapita kwenye vishoroba wanaingia kwenye maeneo ya wananchi, wananchi wanakufa maeneo yale, kwa nini hakuna mpango bora wa matumizi ya ardhi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikiliza sekta ya maliasili wanakuambia solution hapa ni kupanga matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo haya. Mheshimiwa Waziri nikuombe kwa haya ambayo nimeyasema mimi naamini kabisa kesho utakuja kuyatolea maelezo vizuri na niseme tu kweli kesho nisiporidhika nitakuwa miongoni mwa watu wa kushika shilingi kwenye hili ili angalau niweze kupata ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)