Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii na mimi kuchangia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Hapa leo nachangia, pamoja na ushauri mwingine, lakini jambo langu kubwa ni moja tu la mgogoro wangu wa ardhi kule Ifakara, Kata ya Mlabani ambao unahusisha eneo la Baba Askofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kabla ya kwenda huko, naomba nikishukuru Chama cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sera nzuri tunazoendelea nazo kuhusu ardhi. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri waendelee kusimamia sera hizi kwa sababu tunavyotembea katika nchi jirani tunaona huko mabalaa, kwamba ardhi huko katika nchi za jirani ni ardhi za watu, lakini sisi Tanzania ardhi bado ni mali ya umma na ni mali ya Serikali. Hili ni jambo la kijamaa kabisa na kwa sisi wajamaa tunataka liendelee kuwa hivyo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa Rombo kule kama DAS, nilikuwa navuka jirani pale Kenya, unaona kwamba mwenye kipande cha ardhi anakuwa kama Mungumtu, kwa hiyo sisi Tanzania ni muhimu sana tukaendelea nalo hili kuliweka katika misingi kabisa kwamba litakuwepo miaka dumu daima dumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwa Jimbo la Kilombero, Wilaya ya Kilombero, Halmashauri ya Mji wa Ifakara, kwa mkakati wa Serikali wa hatimiliki. Katika jimbo langu sehemu kubwa sana za vijijini wamepewa hatimiliki na baada ya kupewa tu zile hatimiliki za kimila, ardhi imepanda thamani sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ambayo tunayo ni kwamba wananchi hawakupewa elimu ya kutosha kwamba wanavyouziana zile ardhi kuna utaratibu wa kisheria wa kufuata ili umiliki utoke katika kaya au mila kwenda kwa mtu mwingine. Kwa hiyo ombi langu kubwa kwenye jambo hili ni kwamba, lazima elimu ya kutosha itolewe kuhakikisha kwamba wanaambiwa maana ya hati ya kimila ni nini na wanavyotaka kuuziana wanauziana kwa namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunakushukuru Mheshimiwa Waziri, tunaishukuru Wizara kwa mikopo ya Halmashauri. Halmashauri ya Mji wa Ifakara ilipata fedha milioni 250 ambazo kwa kweli tunashukuru sana Wizara yako kutupatia fedha hizi angalau mmethubutu na mmeanza kuonesha. Changamoto kubwa katika jambo hili ni kwamba upimaji wa viwanja katika Halmashauri zetu malengo yake ni nini, pamoja na kupanga Miji lakini kitu kingine ni kwamba inasaidia watu wasio na uwezo vijana kupata viwanja vya kujenga. Sasa lazima Halmashauri ifikie kuongeza mapato lakini inaongeza mapato kwa kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona wananachi wangu hasa vijana wakilalamika fedha gharama ya mauzo ya viwanja ni kubwa, nimekusikia kwenye speech yako Mheshimiwa umezungumza umesema hapa gharama hizi ni kubwa. Vijana wetu wadogo, vijana wetu ambao wanafanya biashara kama watoto wa fundi cherehani, nywele zao za kipilipili, kiwanja cha milioni tatu atanunua wapi? Kiwanja cha milioni mbili atanunua wapi? kwa hiyo lazima kuna maeneo na kule kwetu kuna mashamba makubwa ya bei rahisi vipimwe viwanja vya laki tano, milioni na muda wa kulipa uwe mrefu hata kama ni mwaka miezi sita. Mtu anapewa siku 90 alipe milioni mbili, milioni mbili na nusu watu hawawezi wanaacha viwanja na viwanja vinabaki kwa akina Asenga tuna watu wengine. Wale vijana wadogo kwa mfano Hansi wa Kidatu, Maisha wa Lumemeo, Sande, Mijije, wakina Kalyoma, wakina Mido hawa ni vijana wadogo sample ya Jimbo la Kilombero vijana maarufu ambao wanajulikana hawawezi hata siku moja kumiliki maeneo hayo kutokana na bei hiyo kuwa milioni tatu ama milioni nne.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusisitiza pia kwamba wekeni wazi, nimeona maoni ya watu hapa, ninachofahamu Mheshimiwa Waziri ni kwamba Tume hii haina mamlaka ya kupima, mamlaka ya kupima yapo kwenye Halmashauri zetu, kwa hiyo ufafanuzi huo uwekwe wazi ili muweze kuziwezesha Halmashauri kama Wabunge wengine walivyoshauri hapa. Halmashauri ndiyo ziwezeshwe zipime na ziangalie level na maeneo na watu wenye uwezo kama nilivyosema awali vipatikane viwanja, nchi hii viwanja vya laki tano vinaweza vikapatikana vijijini. Ifakara kule pimeni viwanja vya laki tano, tano, milioni, vijana na wakulima wale waweze kumiliki viwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anapata gunia zake tano akiuza alipe kiwanja, sasa mtu anauza gunia kumi bado haitoshi kulipa kiwanja, gunia kumi za mpunga. Sasa hii kwa kweli inakuwa ngumu matokeo yake wageni wanamiliki ardhi na wananchi wetu wa kawaida wanakosa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili ni kubwa Mheshimiwa Waziri, kuna mgogoro pale ambao mimi niliusikia tangu 2015, Kanisa la Roma chini ya Baba Askofu Libena, Baba Askofu Salutaris Libena tunavyozungumza hivi yuko Roma anapiga goti kuombea nchi yetu, anaombea Jimbo letu wako Roma huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mgogoro tangu 2015 Rais alipokuja pale wakati ule aliambiwa mbele ya umati, kuna eneo kubwa la kanisa liko Ifakara Mjini karibu heka 1,000, kuna hekari kama 200 sikumbuki vizuri zimevamiwa na wananchi wamejenga, hawa ni wananchi wetu. Mwanzoni kanisa lilikuwa na msimamo wa kutaka watu wale wahamishwe, lakini mimi mwenyewe nimeenda kuzungumza na Baba Askofu. Baba Askofu Libena amekubali wananchi wale wapimiwe wamilikishwe apewe ardhi mbadala, ni jambo kubwa na ni jambo zuri na nimeenda Kata ya Mnadani nimekaa na wananchi wako tayari kupimiwa kulipa hati zao ile fedha ikatafutie Baba Askofu ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri fedha za kupima tu zinakosekanaje, sasa wewe ni Mama yangu, wewe msikivu, mimi hapa kweli nilete ukorofi wa kushika shilingi kwenye jambo hili, hata wananchi wangu watasema tena kwa Mama Mabula kweli mbona umekosa adabu. Nisaidie Kamishna Frank ni mtu mzuri, Kamishina wetu wa Ardhi Mkoa wa Morogoro mtu mzuri, ukimsaidia kwenye barua yake na barua yake nimekuletea mezani hapo ili Baba Askofu akirudi huko aliombee Taifa.

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Asenga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ndulane.

TAARIFA

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huo anaozungumza Mheshimiwa Abubakari Asenga ni wa kweli kabisa na ulianza wakati nilipokuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara. Just imagine, Kata Tano ya Mji wa Ifakara ziko ndani ya eneo la Kanisa Katoliki Jimbo la Ifakara, kwa hiyo ni mpango muhimu naomba asaidiwe.(Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga taarifa unaipokea.

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kabisa Kaka Ndulane nakushukuru sana Mkurugenzi wangu na ikimpendeza Mungu urudi tena pale kwa mara nyingine kuwa Mkurugenzi! Hiyo nimechomekea tu. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana kwa kweli alikuwa Mkurugenzi wetu wa Halmashauri yetu ya Mji wa Ifakara, yeye na Mbunge wa Mikumi Mheshimiwa Dennis Londo naye alikuwa Mkurugenzi pale wanajua mgogoro huu, nasi Wakurugenzi wetu wana bahati ya kuwa Wabunge. Kwa hiyo hawa wawili walikuwa Wakurugenzi na sasa hivi ni Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kusema ukweli kwamba hili jambo ni very serious kabisa na tunashukuru Baba Askofu asije akabadilika kama amekubali kutoa ardhi hii kwa wananchi wale waliovamia na ameweka mpaka kabisa hawaruhusiwi kuendelea kuvamia tena maana pale kuna hospitali kubwa ya kansa amejenga, Good Samaritan, kuna hospitali ya St. Francis katika hilo eneo ya Rufaa ya Kanda, sasa wananchi wale hawawezi kuendeleza, hawawezi kupata mikopo, kwa sababu ardhi ile siyo ya kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo Mbunge mwenyewe nimetafuta hela nimepeleka katika Kata ya Mnadani fedha za zahanati, hatuna eneo la kujenga zahanati Baba Askofu anasema mpaka mmalize mgogoro wangu ndiyo nitawakatia eneo la kujenga zahanati. Kwa hiyo, maendeleo katika Kata ya Mnadani na Ifakara kwa ujumla yanakwama kutokana na mgogoro huu, viwanja hivi ni takribani elfu kumi tu, wananchi wale wapimiwe wapate hati zao waweze kwenda kukopa huko waweze kufanya maisha yao vizuri, tupate baraka za Baba Askofu, maana Baba Askofu unajua akishavaa madude yake yale anatisha Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, tunakuomba sana utusaidie jambo hili liishe na mimi sitaki kukukera hapa wala kuongea sana muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimechangia ardhi kwa sababu ya agenda hiyo moja kubwa na Baba Askofu aliniambia sijui kama mlisoma wote anakufahamu vizuri, sasa mimi napata mashaka wewe Waziri huwezi kumsaidia Baba Askofu kwenye jambo la haki kama hili, mimi nataka kusikiliza majibu hapa leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)