Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara muhimu sana ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametujalia afya njema na ametujalia uhai tupo hapa leo. Jambo la pili namshukuru Mheshimiwa Rais kwa hakika anayo dhamira njema, ana nia njema. Sisi ambao tunatoka maeneo ambayo yana migogoro wanafahamu kwamba iliteuliwa Kamati ambayo ina Mawaziri Nane ambao wanashuhulikia huu mgogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kidogo sana kuhusu mgogoro na watu Chemba nisiposimama kuongea kwenye Wizara hii watanishangaa sana na inawezekana nikapoteza kabisa asilimia 40 ya kura zote. Kwangu kuna changamoto moja ndogo sana lakini shida kubwa ya changamoto hii ni utashi wa Viongozi tuliyonao. Hii naomba niseme wazi kama kumsema hivyo nakosea potelea mbali lakini nataka niseme ukweli. Tuna mgogoro ambao umeanza mwaka 2014, mgogoro huu umeacha wakulima wananchi wangu 1,168 bila mashamba. Ni jambo la ajabu sana kwamba unakuta watu wana mashamba alafu unawaondoa tangu mwaka 2014 mpaka leo wanaendelea kuzurura haujui wanaishi vipi? Ni jambo la ajabu na haliwezi kutokea sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha mgogoro huu ndiyo maana nasema shida ni viongozi. Chanzo cha mgogoro huu ilikuwa ni ku–review mipaka, wakati wana – review mpaka kati ya Chemba na Kiteto maeneo ambayo yalikuwa ya Kiteto yalirudi 197 Kondoa wakati huo, sasa hivi ni Chemba. Baada ya kurudi Kondoa ambaye ni Chemba mashamba yao yakabaki Kiteto maana yake ni nini? maana yake kiijiji baada ya kuweka mipaka mipya wananchi wangu wamebaki na kijiji lakini mashamba yao yamebaki Kiteto na sisi wote tunafahamu, kwamba mipaka ya utawala haikufanyi upoteze haki yako ya shamba lako. Hii inafahamika lakini cha ajabu wananchi wale walilazimishwa na kunyang’anywa mashamba yao kwa sababu tu sasa mipaka ya kiutawala wamerudi huku Chemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la ajabu sana. Ninayo hukumu ya Mahakama hapa, wameenda Mahamani wameshinda, tena Mahakama ya Wilaya ya Kiteto kule kule lakini mpaka leo bado watu wamebaki hawana mashamba. Sasa mimi namuomba Waziri kama kuliko nibaki na watu ambao hawana mashamba naombeni kile Kijiji cha Oruboroti kichukeni kiwe Kiteto ili mashamba yao wabaki nayo, kuliko kubaki na watu 1,168 hawana mashamba maana yake wamekuwa tegemezi kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nimekuwa nikipata ushirikiano sana wa Viongozi wa kutoka Kiteto wenyewe, ninayo barua ya Waziri wa TAMISEMI wakati huo, ambayo inamuelekeza Mkuu wa Mkoa wa Manyara na Dodoma kwamba kwa sababu ya ku– review mipaka hiyo isiwe sababu ya wananchi wa Oruboroti kupokonywa mashamba yao, mipaka hiyo ni ya kiutawala tu. Barua hiyo haijawahi kufanyiwa kazi ninayo hapa Mheshimiwa Waziri, matokeo yake watu wangu wakienda kulima wanashikwa, wengine wanapelekwa, imagine mtu anachukuliwa Kiteto anapelekwa kufunguliwa kesi Arusha badala ya Manyara, huko anabambikiwa kesi ya nyara za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimuombe sana mimi nina uhakika yeye anaweza kutusadia, jambo hili limekuwa linaumiza sana hasa kwa watu wa Chemba. Siyo hivyo tu, nataka nikuonyeshe jambo la ajabu sana, baada ya hukumu ya Mahakama kutoka Mkuu wa Wilaya ya Kiteto ninayo barua hapa, alimwandikia Afisa Tarafa wa Makame ambapo ndiyo mashamba yapo. Kwa sababu wananchi hao wameshinda kwenye kesi yao Mahakamani, warudishiwe mashamba hayo ndani ya wiki saba. Mkuu wa Wilaya anamwagiza Afisa Tarafa wake na hakuwahi kutekeleza mpaka leo, sasa hii ndiyo nchi ya namna gani? Hii ndiyo nchi ya namna gani? wakati alikuwa ana uwezo tu wa kumpigia simu tekeleza hilo mara moja, tafsiri yake ni kwamba, yawezekana haya maandishi lakini utashi wao wa kutatua changamoto hii haipo, kwa hiyo nikuombe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana pia tulikuwa na Mkuu wa Mkoa, Mbunge mwenzetu hapa anaitwa Mnyeti na wakati huo Mkuu wa Wilaya pia alikuwa Mbunge hapa, nakumbuka majibu waliomjibu maana Mnyeti alimwambia kwa nini unachukua mashamba ya watu wa Chemba? Mkuu wake wa Wilaya ambaye ni Mbunge sasa hivi ananisikiliza kasema hao watu ni wa Chemba lakini, akamwambia Chemba ni Rwanda? Wewe una akili gani? Nakumbuka nilikuwepo, nakushukuru sana Mheshimiwa Mnyeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo unaweza ukaona sababu ya migogoro hii ni sisi viongozi wenyewe. Mimi nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, juzi kama siku tatu, nne zilizopita wameenda tena kubandika maeneo ya Chemba. Kuna changamoto nyingine ni ya ajabu sana, vipo vijiji ambavyo viko Wilaya ya Chemba lakini vinaitika Kiteto kwa sababu tu wao ni Wamasai kwamba wako tayari kwenda kwa Wamasai wenzao. Kitongoji kipo Chemba lakini wao michango yote kila kitu wanafanya kwenye Wilaya ya Kiteto na ukienda kuwagusa shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi niombe sana, kwa sababu kama ni suala la ku– review mipaka na beacon tayari limefanyika, sasa sijui tutumie maarifa gani? mimi nikuombe sana Mheshimiwa Waziri hebu upate fursa na wewe ukatembee, safari hii Mheshimiwa Waziri eneo lile watu wamekufa mara kadhaa, naiona hali, naliona joto lilivyo, ninaona kabisa hali ilivyo kwamba mvua zikinyesha mwaka huu hali itakuwa tete sana. Sasa niwaombe sana, niwaombe sana hebu ifikie mwisho wa mgogoro huu kwa sababu kama ni Mahakamani tumeenda tumeshinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo limekuja pale Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri kuna watu wanaitwa WMA, WMA wamekuja wamekuta watu wana mashamba, wameongea na kijiji, kijiji hakikuwahi kulipa fidia wala hiyo WMA hawajawahi kulipwa fidia wanawaondoa wananchi wangu na sasa hivi wameendelea kujitanua kwenye maeneo mengine kumekuwa na mgogoro mkubwa sana. Migogoro hii ya ardhi inamaliza ndugu zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi wiki mbili zilizopita amekufa Mwenyekiti wangu wa kitongoji, kwa sababu ya mgogoro wa ardhi, wamemuua kuna mgogoro wa ardhi pale wameenda wakamuua na sasa hivi kesi inaendelea Mahakamani. Kwa hiyo unaweza ukaona namna ambavyo kuna changamoto kubwa hii. Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri nimesimama hapa kwa ajili ya kuongea hili tu, na nimesema kwamba kama kuna sababu yoyote au kama ni lazima wale wananchi wa kijiji cha Oruboroti kurudi Kiteto ili mashamba yao yabaki naomba wawachukue, ili mradi warekebishe beacon kuliko kukaa na watu ambao hawana mashamba na kila siku wanatuletea shida. Mimi nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, mimi mchango wangu leo ulikuwa huo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo wanashukuruni sana, ahsante sana. (Makofi)