Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Bahati Keneth Ndingo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbarali

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata fursa. Nami niungane na kaka yangu Mwita Waitara kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Tunaona nia ya dhati kabisa ya Mheshimiwa Rais wetu kuhakikisha kwamba anamaliza suala la migogoro ya ardhi ndani ya Taifa hili. Nia hiyo tunaona tafsiri nzuri kabisa ya Mheshimiwa Rais, hataki migogoro ya ardhi ndani ya Taifa, lakini tatizo linakuja kwa wasaidizi wake huku chini kwenye tafsiri ya nia njema ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tarehe 18 mwezi wa kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifika pale Mbarali. Alifika pale Kapunga, Mbarali na Mheshimiwa Waziri alikuwepo Mama yangu Dkt. Angeline Mabula. Aliona kiu ya Wanambarali kutaka kujua hatma ya mgogoro huu. Wanambarali walijitokeza kwa wingi pamoja na shughuli za shamba hawakwenda ili wasikilize Mheshimiwa Waziri Mkuu anasema nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu alituambia kati ya migogoro ya vijiji 34 ambavyo tumedumu navyo Mbarali kwa miaka 15, vijiji 29 vitarudi kwa wananchi na vijiji vitano vitabaki kwenye hifadhi. Sasa kinachoendelea kule Mbarali tunaona watu wa TANAPA wanaendelea kuweka beacon kila mahali. Hata vile vijiji ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu alitamka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mama yangu Mheshimiwa Angeline, kesho anavyokuja kufanya majumuisho hapa, tunachotaka sisi Wanambarali na Wanambarali wamesema kesho watakuwa kwenye TV watashika kalamu na karatasi wajue kijiji kwa kijiji, vipi vijiji hivyo 29 ambavyo vinabaki kwa wananchi na vijiji vitano vipi ambavyo vitabaki hifadhini? Kesho tutamsikiliza mama yangu, la sivyo kesho, nitaondoka na shilingi ya Mama yangu mpendwa, asipotutajia vijiji hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo ni salamu za Wanambarali, kesho tunamsubiri mama yangu Mheshimiwa Waziri hapo, atuambie kwa majina kijiji kwa kijiji na vinavyoondoka ni vipi na vinavyobaki ni vipi?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa inatoka wapi? Mheshimiwa.

TAARIFA

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Anachokizungumza Mheshimiwa Bahati ni sahihi kabisa. Licha ya nia njema ya Serikali ya kutatua mgogoro ambao uko Mbarali, kumekuwa na changamoto ya uwekaji beacon kiholela kwenye maeneo ambayo wananchi wanafahamu kabisa Serikali iliwazuia. Kwa hiyo ni vyema Serikali ikaenda kuangalia, kinachozungumzwa hapa Bungeni na kinachofanyika nje, ni vitu viwili tofauti. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bahati unaipokea hiyo taarifa?

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili kaka yangu Festo naye ni muhanga kwa sababu Mbarali na Makete ni watu wale wale wanaingiliana. Kwa hiyo anaijua vizuri hii historia ya kule Mbarali. Namshukuru sana my brother. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, inasikitisha sana kuona kwamba mpaka sasa hivi 25% tu ya ardhi ya Tanzania ndiyo imepimwa. Hii migogoro tunayoimba kila siku humu Bungeni ni kwa sababu tunaenda pole pole sana kwenye kupima ardhi ya Taifa hili. Hivi kwa mfano, kweli tangu tumepata uhuru, leo hii tumepima 25% tu ya ardhi, tunahitaji miaka 180 kumaliza kupima nchi hii, kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo sawa, teknolojia zimekua. Ujuzi wetu umeongezeka, kwa nini hawapimi ardhi? Watu wanashindwa kuendelea, leo hama hapa, ondoka hapa, yaani fujo tu, kwa sababu hawapimi ardhi. Wapime ardhi ya Taifa hili tuondokane na migogoro ya kila kukicha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wanawekeza watu hapa, walime, kesho ondokeni hapa nenda hapa, wamekaa miaka 70, wamezika babu, vijukuu, kesho ondokeni hapa, tunakuwaje hivyo? Why? Kwa nini hatupimi ardhi yetu na wanaangalia kabisa taarifa za Mtakwimu wa Serikali. Sasa hivi…

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.

TAARIFA

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nataka nimpe taarifa dada yangu Bahati kwamba anachosema ni kwamba itatuchukua muda mrefu kupima ardhi. Leo mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji vyetu, mfano, Wilaya ya Ikungi, katika vijiji vilivyopo 101, it’s only vijiji vitano tu ndiyo vina mpango wa matumizi bora ya ardhi. Kwa hiyo tusitegemee kwamba bila kupima tutamaliza migogoro. Kwa hiyo migogoro itaendelea, dawa ni kupima ardhi ya nchi hii. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bahati unaipokea hiyo taarifa?

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nazipokea taarifa zote, ni kweli kabisa hatuko serious kwenye upimaji wa ardhi ya Taifa letu na hatuwezi kumaliza migogoro ya Taifa hili kama hatupimi ardhi. Kwanza tunawarudisha watu nyuma kimaendeleo kila siku, leo watu wanalima hapa, kesho ondoka hapa nenda hapa, hatuwezi kuendelea kama Taifa. (Makofi)

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bahati kuna taarifa.

TAARIFA

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba ule mradi ambao Mheshimiwa Waziri ameuzungumza hapa ndiyo una lengo la kwenda kutayarisha miundombinu ya teknolojia bora ya upimaji ili tukimaliza kuutekeleza ule mradi, sasa itakuwa ni rahisi kwa kuweka miundombinu bora ya upimaji na tutakwenda kwa haraka zaidi katika upimaji, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bahati unaipokea hiyo taarifa?

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa, yaani kweli leo hii ukaende kupima vitu vya hivyo? Hapana, siipokei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima Wizara iwe serious na tuone kwenye mikakati yao wako serious kupima ardhi ya Taifa hili. Hivi wenzenu kila siku ni migogoro, kila siku ni migogoro. Mama yangu atakwenda kule, wapime ardhi, matatizo yote haya yatakuwa hamna. Kwa kweli tunaomba wapime ardhi ya nchi hii. Mipango yao hiyo haionyeshi kama kuna uthabiti kabisa na wana malengo la kweli la kutaka kupima ardhi ya nchi hii. Kwa kweli mama yangu Mheshimiwa Waziri ili na apumue, wapime ardhi ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata fursa. (Makofi)