Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Ahmed Yahya Abdulwakil

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. AHMED YAHYA ABDUWAKIL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, ambayo ni bajeti mkombozi na Wizara ambayo inaweka ustawi mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda mbele zaidi napenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na namna anavyotupendezesha na kutufurahisha katika uongozi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwanzo nilivyosimama kuongea kwenye kiriri hiki nilisema maajabu ya Reli ya SGR, leo Tanzania tunakuwa kama Marekani. Tunakuwa na reli ya kisasa ambayo ni sawasawa na Shirika la Reli la Marekani linaloitwa FELA na kama nasema uongo Balozi Mulamula analijua vizuri shirika hili. Kwa hiyo na sisi Tanzania tunaingia katika historia mpya kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiingia kwenye nukta ya pili tuseme tu kwamba nchi inasonga mbele, ndugu yangu Profesa Mbarawa na timu yake na Engineers wake wanafanya kazi usiku na mchana. Nimewahi kushuhudia daraja la Wami, kazi imemalizika kabla ya muda ambayo si rahisi kwasisi tunaoshughulika na shughuli za ujenzi, lakini Daraja la Wami limeokoa vifo kabla muda na limefunguliwa kabla ya muda. Hili niseme tu ni kwa sababu ya kuwa na watendaji wazuri na aliyevaa kiatu cha TANROADS Engineer Mativila lazima apongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda mbali zaidi kwa shukurani kwamba kwa sisi watu wa Kusini Zanzibar tunaitwa kwamba Profesa na timu yake “hawana lala” kucha kutwa “wa kazini” maana yake wao kutwa muda wote wako kazini. Kwa hiyo nampa hongera sana sana Profesa, anafanya kazi nzuri na timu yake yote, Engineers wote hapo Mwakibete na wenzio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi humu katika Bunge imezungumzwa Air Tanzania ambayo inafanya kazi kubwa. Pamoja na matatizo madogo madogo yaliyokuwepo lakini Air Tanzania wanafanya kazi kubwa sana. Mashirika ya Ndege kama Ethiopia, Alitalia American Air na mengineyo hayakuanza hivyo, walianza kwa kusuasua mpaka yakatengemaa. Yapo matatizo madogo madogo ya kiutendaji na CEO Matindi anachukua juhudi kubwa sana kuweka sawa. Kwa hiyo tuwapongeze, tungepata wapi kama si juhudi za Mama? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Timu ya Yanga Africans inakwenda Algeria kwa ndege yetu, tungepata wapi? Kwa jeuri tunaipeleka na kuirejesha, kwa hiyo kwa sifa hizo, naunga mkono bajeti hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)