Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Aloyce Andrew Kwezi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nichukue nafasi hii nikushukuru sana wewe kunipa nafasi nzuri ya kuchangia lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dokta Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na kuhakikisha nchi yetu iko salama, miradi inakwenda na hakuna mradi uliosimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nimpongeze Waziri pamoja na Naibu Mawaziri wake wote, pia niwapongeze watendaji wote, nisimsahau Mtendaji Mkuu wa TANROADS pamoja na Meneja wa Mkoa wa Tabora. Meneja wa Mkoa wa Tabora anafanya vizuri sana na sisi Wanatabora, Wanakaliua tunamshukuru sana kwa kazi nzuri anayoifanya katika Mkoa wetu wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mazuri nimeanza kupongeza kwa sababu kazi zinazofanyika Kaliua ni kazi ambazo hazijawahi kufanyika kwa miaka yote iliyopita. Kaliua kwanza tumenufaika kuna barabara inatokea Kaliua kwa maana ya Chagu - Kazilambwa ya kilometa 36. Mheshimiwa Rais wetu ameleta shilingi bilioni 38 na barabara sasa hivi iko zaidi ya asilimia
90. Kwenye miradi ya reli SGR, ule Mkataba wa Tabora – Kigoma unapita Kaliua lakini ukarabati wa reli ya Kaliua – Mpanda unakwenda vizuri. Hii ndiyo sababu ya mimi kuanza kupongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi chini Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Waziri mambo machache, jambo la kwanza kabisa pamoja na kumshukuru ninavyomwambia kwa sasa tunaendelea na kufunga taa pale Kaliua Mjini, lami sehemu kubwa imekamilika na wanaendelea na ufungaji wa taa kutoka relini Kaliua mpaka Kasungu na kwenda kwenye T. Zoezi hilo linatekelezwa na Mkandarasi mzalendo SAMOTA na nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkandarasi yule kwenye Mkoa wa Tabora amefanya kazi kubwa sana, ukiangalia barabara ya kutoka Urambo kwenda Kaliua ni Mkandarasi huyo aliyeweza kuijenga. Wakandarasi hawa hebu muwa-empower mhakikishe kama wana madeni wanalipwa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kubwa kwa Mheshimiwa Waziri, pale Kaliua ile barabara yetu ya mchepuko kutoka Ushokola relini pale kwenda mpaka njiapanda ya kuunga Urambo zimebaki kilometa 2.3, nimeona kwenye bajeti inayoanza mwezi wa Julai mmeweka kilometa moja, Mheshimiwa Waziri nikikuangalia hivi najua ni material ya Kinyamwezi kabisa, kwa heshima zote nakuomba mwezi Julai tunapoanza ile kilometa moja hebu ongezeni ziwe kilometa mbili zikamilike ili mimi nitakaposimama mwakani tunasogea sogea kwenye mambo ya uchaguzi tuendelee kuimba CCM hoye, iyena iyena au siyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ombi langu la kwanza linagusa Ushokola na ni hilo kubwa sana, Mtendaji wako ana taarifa zote na Meneja wako wa Mkoa wa Tabora anafahamu hili. Kwa hiyo, ombi langu la kwanza ni hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la pili kubwa Mheshimiwa Waziri linagusa barabara ya kiuchumi, barabara ya kutoka Mpanda – Kaliua – Kahama. Mheshimiwa Waziri barabara hii imewekwa kwenye Ilani zaidi ya mara tatu na mimi sitegemei nimebakiza miaka miwili kwenye kipindi hiki niendelee kuona maneno. Mimi ni muumini wa utekelezaji naamini na wewe ndivyo ulivyo. Nikuombe kwenye bajeti ya Katavi mmeweka ujenzi wa daraja, ninaomba daraja hilo lianze mara moja isiishie kwenye kuandika bila utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge wa Katavi nimeona anaongelea jambo hilo na mimi naungana naye, tuko pamoja tunategemea mazao ya tumbaku kutoka Mpanda kuja Kaliua kwenda Tabora na maeneo mengine yawe safari nzuri kabisa bila wasiwasi wowote. Pia mazao ya asali tunayategemea sana lakini mazao mengine ni mahindi pamoja na mchele. Niwaombe sana mhakikishe barabara hii inakamilika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri juzi tulikaa na wewe hapa wiki iliyopita, ile barabara ya kwenda Kigoma zile kilometa 36 nilizozieleza, ule mchepuo wa kwenda Ugansa – Usinge ndiyo kilio kikubwa cha Wanakaliua. Mchepuo ule barabara iko chini ya ufadhili wa OPEC kama sikosei. Ulimpigia simu Mtendaji Mkuu na Mtendaji Mkuu akasema hana shida, leo mpo watatu hapa pamoja na Meneja wangu hebu malizeni jambo hili. Fedha ipo kwa nini wasianze? Wazee wa Usinge wanapiga simu kila siku hata hapa nikwambie tu nimepokea simu nyingi sana na nitawataja hawa wazee ili furaha yao ikamilike kwamba Mbunge wao Kwezi nimetamka kwako kwamba ile barabara ya mchepuo ya kilometa Saba inakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wazee hawa walionituma ni George Kamsini, Mzee wa pili aliyenituma ni Juma Kitakala, Mzee wa tatu ni Malabe, Mzee wa nne ni Mademo, kijana Kakobe, Mama yangu Mama Mau na Rehema Hamisi wamepiga simu leo, wanataka lami Usinge. Mheshimiwa Waziri kilometa saba kitu gani na fedha ipo? Mtendaji Mkuu tena nimpongeze Mtendaji Mkuu ni msikivu sana, hata usiku ukituma message anajibu. Mtendaji Mkuu nakwambia Meneja wa Mkoa wa Tabora yuko hapa, mkitoka hapo nje anzeni na Kaliua tafadhali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwathibitishie sisi Kaliua tuko na nyie, wilaya iko makini, iko salama chini ya Mkuu wa Wilaya yetu Rashid Chuachua anasimama vizuri, hakikisheni jambo hili limekwisha, mnampa kero. Mnanipa kero, mnampa kero Mwenyekiti wangu wa Mkoa wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuongelea ni suala zima la reli. Jamani, Kaliua pale ni njiapanda kama ilivyo njia panda Tabora na kwenye upande wa reli ni vivyo hivyo. Niwaombe sana hizi ajira zinazojitokeza hakikisheni wenyeji wamepata ajira hizi, vijana wa Kaliua wapo wa kutosha, vijana wa Mpanda wapo wa kutosha, vijana wa Kigoma wako wa kutosha kwa sababu hizo reli zinatunufaisha wote. Wasihame na watu kutoka mbali sana kuhakikisha wanapata pale. Hata ule ukarabati fuatilieni ule ukarabati wa Kaliua – Mpanda tunahitaji wenyeji wapate. Zipo kazi ambazo hazihitaji shule, zinahitaji nguvu. Si mnasemaga mizigo mizito wape Wanyamwezi? Sasa mnakwepaje mnahama na watu? Niombe mlifuatilie hilo Mheshimiwa Waziri, tufanye kazi kwa pamoja tuhakikishe tunafaulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa kwenye reli ambalo ni la mwisho kwangu nilikuwa naomba kuna vituo kabla ya stesheni na stesheni pale kati kati wanatozwa faini wananchi wanapovuka kutoka vijiji ‘A’ kwenda vijiji ‘B’ naomba ufuatilie jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya, Mheshimiwa Waziri nakutegemea sana, naunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)