Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia siku hii ya leo. Kwanza kabisa ninaomba nimshukuru Mungu ambaye ametupa uzima na uhai tuko hapa kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya kwa ajili ya Tanzania. Ninaomba nimpongeze Waziri pamoja na Naibu Mawaziri kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sisi Mkoa wa Katavi ametujengea bandari, alitupa bilioni 47. Bandari imekwisha kwa asilimia 100, tunategemea bandari ile tuweze kupata mizigo. Sasa tunaipataje hii mizigo bila kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, lazima sasa hivi Watanzania tukubali wawekezaji waje kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam wawekeze ili uchumi wa Watanzania uweze kuongezeka. Kwa sababu maendeleo tunayapenda, tukienda kwa wenzetu, nchi za wenzetu tunafurahi, tunasifia, sasa tunakuja kwetu kuhakikisha sasa maendeleo yanakuja, Serikali inajitahidi kuleta maendeleo, mabadiliko sisi wenyewe tunaanza kupinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ni kitu ambacho hakikubaliki, Mheshimiwa Waziri songa mbele, weka wawekezaji Bandari ya Dar es Salaam wametujengea bandari ili wawekezaji waje, uchumi wa Watanzania uweze kuongezeka. Nakuja kwenye jimbo langu, fidia; Wabunge wenzangu wameongea hapa, najua Waziri anahangaika, safari hii bado hajaweka bajeti yake kuhakikisha analipa fidia, lakini tunaomba Serikali tujipange vizuri, tuhakikishe bajeti inayokuja tuweke pesa ilituweze kuwalipa wananchi wanaotudai fidia. Wengine sasa hivi wameshakufa, huko tukienda katika majimbo yetu watu wanalalamika. Tunaomba sana Serikali ijipange kuhusu fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie kwa upande wa TRC. Naomba niishukuru Serikali kwa ajili ya standard gauge na kuhusu reli yetu ya kutoka Tabora - Kaliua mpaka Mpanda. Najua Serikali ina mkakati mzuri ina mpango mzuri kuhakikisha gauge zile zinabadilishwa ili treni yetu ya kutoka Tabora kuelekea Mpanda iweze kubadilika. Hata hivyo, nina masikitiko, tuna wafanyakazi ambao ni vibarua ambao wanakaa katika magenge. Wale vibarua wamekaa sasa takribani miaka 15, wengine miaka 20 mpaka leo bado vibarua, lakini wale ndio wanatulindia reli yetu, kwa sababu bila kutunzwa reli ile uharibifu unaweza ukatokea wakati wowote, halafu majanga yanaweza yakatokea wakati wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iwatazame wale vibarua, kulipwa kwao ni shida. Hawalipwi kwa wakati, wanaweza kukaa miezi mitatu, wanakaa porini, wanakaa kwenye mazingira magumu. Naiomba Serikali iweze kuchukua jukumu hili kwenda kuonana nao hususan Mkurugenzi wa TRC, aende akaongee na hawa vibarua. Najua wana mipango mzuri, mikakati mizuri kwa ajili yao lakini waende wakaongee nao ili waweze kupata morale kwa ajili ya kuhakikisha wanakaa kwenye mazingira mazuri hususan wanaokaa Genge la Ugala, Kamini, Kabuziyoti, Katumba, lazima twende tukawaone tuwape moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana mabehewa ni machache, wasafiri ni wengi. Tunaomba tuongezewe mabehewa, wananchi wanahangaika kutoka Mpanda behewa linakuwa moja au mabehewa mawili, wasafiri wako wengi. Tunaomba wasafiri wa kutoka Mpanda kuelekea Tabora tunaomba tuongezewe behewa. Tuongezewe behewa kwa sababu wananchi wanahangaika, usafiri umekuwa mzuri na usafiri ukiwa mzuri watu wanafurahia ndio maana wanatamani kupanda treni yao, basi tunaomba mabehewa yaongezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilituahidi barabara ya kutoka Kawajese ya lami kupitia Ugala na kujenga Daraja la Ugala. Barabara ile inaenda mpaka Kaliua, Kaliua mpaka Kahama. Naomba Waziri aje kutueleza barabara hii kwa kiwango cha lami na kujenga Daraja la Ugala, vitajengwa lini na lini tutaweka pesa, kwa sababu barabara hii iko kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Tunaomba sana barabara hii iweze kujengwa kwa sababu itafungua fursa kubwa sana kwa ajili ya kutoka Mpanda mpaka Kaliua, Kaliua mpaka Kahama, Kahama mpaka Mwanza, kwa ajili ya maendeleo na fursa mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna Ziwa Tanganyika, wenzangu wamesema, Ziwa Tanganyika hatuna meli. Tunaomba meli, tulikuwa tuna meli ilikuwa inapita, lakini toka ilivyosimamishwa meli ile mpaka leo hii hakuna meli ya aina yoyote inayofanya kazi katika Ziwa Tanganyika. Tunahitaji meli na sisi watu wa Ziwa Tanganyika tunataka tujengewe meli, kwa sababu maendeleo tunaona, wanatuletea maendeleo mengi na sasa hivi wanatujengea barabara ya lami kutoka Mpanda mpaka Kalema. Sasa ina maana mizigo itakuwa mingi, abiria wako wengi na ndio maana tunasema basi kama hivyo, tuwaweke wawekezaji ili waweze kufanya kazi hii ili maendeleo yaweze kukua katika Nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba niunge mkono hoja. (Makofi)