Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu na mimi nichangie hoja hii ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mambo mawili ya kuchangia katika Wizara hii. Kwanza ni shukrani; na ninaipongeza sana Serikali kwa kazi nyingi na miradi mikubwa inayofanya na kwa kipindi hiki chote ambacho tumepita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mikubwa imefanyika ikiwemo viwanja vya ndege, barabara, madaraja, meli zinazojengwa huko, vivuko na baba lao kabisa SGR. Baada ya miradi hii kukamilika Serikali itakuwa bingwa wa usafirishaji wa nchi kavu, pia usafiri wa baharini na katika maziwa kote nchini; lakini bila kusahau maombi ya wenzetu wana Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema hongera sana kwa Mama Samia Suluhu Hassan na Wizara hii na hasa Profesa Mbarawa na wenzake wamefanya kazi kubwa sana. Sisi kule kwetu Unyamwezini tuna msemo unasema “hapana kujidharau” au kinyamwezi “yaya kuibyeda.” Hili ni jambo kubwa sana sana, hela za ndani na za nje lakini tumejenga barabara zetu madaraja na yale niliyoyasema yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni kuhusu suala la bandari ya Dar es salaam. Kwanza nikiri kwamba mimi ni mkandarasi daraja la kwanza, kwa hiyo naitumia sana bandari hii kuagizia vitu kutoka nje. Bandari ilivyo sasa ilifika wakati mimi nilipata hasara kandarasi tatu; mradi mkubwa wa STR pale Arusha na mradi wa ZBC kule Zanzibar na mradi wa Bunge hili. Wakati tukiagiza mitambo kupitia bandari palikuwa na matatizo makubwa sana, meli zilikuwa zinakaa nje muda mrefu mpaka leo zinakaa nje muda mrefu lakini vilevile kulikuwa na ukiritimba ambao ulifanya mimi nicheleweshe mizigo kuleta kwenye miradi kwa hiyo nikapigwa adhabu kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za bandari si huduma, ni biashara, na wafanyabiashara wanafanya biashara ili wapate faida, hakuna mfanya biashara anayependa kupata hasara; na bandari ina kipimo au KPI, na KPI kubwa ya bandari ni kutoa mizigo. Kama bandari haitoi mizigo inakuwa hasara kubwa sana. Lakini nimejifunza kwenye bandari nyingine, kwa sababu wakati fulani tuliacha kupitisha mizigo, nikiwemo mimi mwenyewe, kupitisha mizigo Bandari ya Dar es salaam tukapitisha Mombasa.

Muda wa kupeleka mizigo kule na kupeleka magari kuleta mizigo tena Dar es salaam au Arusha ilikuwa muda mfupi kuliko meli iliyokaa muda mrefu pale bandarini, kwa siku 21. Asubuhi unaambiwa meli yako imefika lakini bahati mbaya unaambiwa rudini meli iko nje siku 21na mzigo unatakiwa uje kwenye site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hiyo ni bahati kama mzigo umefika moja kwa moja, lakini bahati mbaya zaidi ukifanyiwa Tran sequent, yaani mzigo unaokuja Dar es salaam meli inaona kwamba hautoshi mzigo kuja Dar es salaam inaancha mzigo Durban halafu meli nyingine ifuate kule inayokuja huku ikae wiki tatu inangojea mzigo kuja hapa, matokeo yake mzigo unachelewa sana, sababu ni nini uwezo wa bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu tusiangalie hapa usoni tuangalie huko mbele tunakokwenda. Ndani ya miaka mitano sita Bandari ya Dar es salaam haitafaa tena kufanyia kazi kubwa kwa sababu meli kubwa zinazoitwa kizazi cha nne na tano au fourth and fifth generation, hazitaweza kuweka nanga Bandari ya Dar es salaam mbili tatu au nne kwa pamoja kwa sababu bandari ni ndogo sana. Inatakiwa bandari hii ipanuliwe na iwe kubwa, lakini mpango mzurini kujenga Bandari kubwa ya Bagamoyo. Tunataka tufanye hivyo sisi, hatuna uwezo, hatuna hela za kujenga Bandari ya Dar es salaam, kuipanua kuweka vifaa vya kisas.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bandari nyingine kila dakika kumi contena tatu nne tano zinatoka sisi hapa kontena ngapi kwa siku? kontena ngapi kwa wiki? Meli zimepiga foleni kule nje tunataka aje mwekezaji ambaye atakuwa na nia ya kuendesha bandari kama ilivyo kule duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishasema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haifanyi biashara, bandari siyo huduma ni biashara, kujitoa Serikali na kuweka mkandarasi, kuweka mwekezaji ambaye atakuwa na malengo mawili kwanza a- operate aendeshe bandari lakini licha ya kuendehs bandari ile awe na lengo la uwekezaji kuipanua bandari lakini bandari imefika kikomo haiwezi kupanuka ni ghali sana. Njia rahisi mwekezaji huyo anayekuja awe na wazo la kujenga Bandari kubwa ya Bagamoyo ili tuweze kufanya biashara ya usafiri wa meli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napata tabu sana watu ambao hawaoni umuhimu wa kuipanua bandari, kuikuza bandari, ni sawa na kuwa na ng’ombe mzuri mmoja au wawili umewakamata unasema wa kwangu. Watu wanakwambia ngoja tuwalishe hao ng’ombe wewe unasema a’ a’ ng’ombe ng’ombe wangu. Ndivyo ilivyo Bandari ya Dar es salaam tutaendelea kuikamata sisi bandari ile haitatusaidia baada ya miaka kumi, itakuwa absolute, haitafanya kazi na fedha hatuna, tuna miradi mikubwa sana ya kufanya huku bara kwenye maeneo mengine kuliko bandarini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashauri na ninashauri kabisa, aje mkandarasi, lakini hatutaki mkandarasi aliyekuwa mbaya kama TICTS, tunataka mkandarasi ambaye atakuja na malengo yanayojulikana na Serikali ituhusushe wadau wote tuone atafanya nini, na tukubaliane mkandarasi atapata hiki na wananchi au Serikali ya Tanzania watapa hiki ili tuweze kuleta ufanisi wa bandari yetu. Sasa hivi bandari hii itatudodea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina uhakika baada ya makubaliano mazuri ya mwekezaji mzuri, aje na malengo mazuri na Serikali ikubali, bandari itakuja kuwa eneo la biashara kubwa na kuingiza hela kwenye Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo nakushukuru sana kuniruhusu kuchangia, naunga mkono hoja.