Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Haji Amour Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makunduchi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nakushukuru sana kwa kuweza kunipatia nafasi hii. Pili, nampongeza Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anafanya kazi kubwa ya kuweza kuipatia Wizara hii ya Ujenzi pamoja na Uchukuzi fedha nyingi sana katika kutimiza miradi yake. Kwa kweli Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi ni Wizara mama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ni Wizara kubwa sana na Wizara ambayo ni kiunganishi cha uchumi katika nchi yetu. Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tukiangalia kwa hali ya kawaida, maana yake uchumi wa nchi yetu unategemea Wizara hii. Ukiangalia suala la utalii, linategemea Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninazungumza hivyo? Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imebeba mambo yote makubwa, tukiangalia barabara pamoja na masuala yote ya miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliangalie suala hili kiukweli kabisa katika Wizara ambayo imefanya mambo makubwa sana ni Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Wizara hii kwa kweli ni Wizara ambayo inatakiwa kupigiwa mfano wa hali ya juu sana. Nizungumze ukweli wangu, kwa namna yote ile na niweze kuwasifu viongozi wa Wizara hii akiwepo Mheshimiwa Prof. Mbarawa pamoja na timu yake, kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. Bahati nzuri tumezunguka sehemu nyingi sana zenye miradi mikubwa sana, tukianzia suala la Mpanda kuelekea Uvinza, Uvinza – Kigoma, kwa kiasi fulani maana yake huko mahali kuna miradi ambayo ni mikubwa sana tukielekea na Mwanza kuangalia miradi ya meli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzungumze ule ukweli, katika sekta ambayo imefanya kazi kubwa ni Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Nazungumza hivi kutokana na kwamba, watu wanasema kwamba mwenye macho haambiwi tazama. Ukweli ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, nasema labda pengine tungefanya safari ya kuzunguka katika maeneo ya Tanzania tukaona namna Wizara hii inavyofanya kazi, ni Wizara ambayo inafanya kazi kubwa sana, ni Wizara ambayo inafanya jitihada kubwa sana. Kiukweli kama alivyozungumza mama kwamba kazi iendelee, miradi yote ambayo imeachwa na mtangulizi wake Marehemu John Pombe Magufuli, miradi yote mpaka sasa hivi kwa 70%, au 80% naweza kuthubutu kusema kwamba kupitia Wizara hii, maana yake imeshakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije na suala langu la upande wa sekta ya PPP ambayo mara nyingi watu wanaizungumza sana hapa kwamba katika suala la uunganishaji, hii Private Public Partnership kwamba kuna suala la huu uunganishaji wa bandari yetu ya Tanzania kupitia Bandari ya Dar es Salaam, hili suala kwa kweli nasema kwamba ni suala zuri na ninaweza kusema kwamba kwa Tanzania nzima, maana yake ni suala ambalo tusiliache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili kwa upande wa Zanzibar, kitu kama hiki cha uwekezaji wa bandari, maana yake tayari Zanzibar wameshaingia mkataba na Kampuni ya South Africa katika suala la PPP (Private Public Partnership), sasa na sisi kwa kuangalia suala la ufanisi wa bandari yetu ni lazima suala hili tuliangalie katika hali kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine mimi nitakuwa nashangaa sana kuona watu wanabeza suala la uwekezaji wa pande tatu; Private Public Partnership kwa dunia nzima. Maana yake kwa sasa hivi, maendeleo mengi makubwa yanaendeshwa kwa mpango wa PPP. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la barabara ambalo nalo Mheshimiwa Waziri alizungumza kwamba kuna barabara ambayo nayo itakwenda kwa mfumo wa PPP. Mimi nadhani kwamba suala hili tujaribu kuliangalia katika hali ya umadhubuti mkubwa sana, isipokuwa suala ambalo ninalolishauri tuwe madhubuti ni katika suala la kuangalia sheria zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala la taasisi zetu hizi ambazo ziko chini ya uendeshaji wa Wizara yetu hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Tukiangalia kwa mfano, kama taasisi ya TEMESA, inafanya kazi vizuri, lakini kama ilivyozungumzwa kwa upande wa hotuba ile ya Mheshimiwa Waziri kwamba TEMESA ipo kama ni kutoa huduma, nashauri TEMESA iwe ni taasisi ya kibiashara. Kwa sababu inavyokwenda, haiendi katika suala la kuleta tija isipokuwa ni sekta ambayo iko upande wa kutoa service.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika utekelezaji wa majukumu yake. Pia namshukuru mama kwa kiasi kikubwa sana kwa kuweza kutekeleza miradi yote ambayo ipo ikiwemo ya barabara, ikiwemo ya reli, ikiwemo ya meli na miradi yote ya madaraja makubwa ikiwemo ya daraja la Kigongo - Busisi pamoja na Bwawa la Mwalimu Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)