Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi na mimi kuchangia katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi ya pekee naomba nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri na hasa katika ujenzi wa barabara na miundombinu ndani ya Jimbo la Nkenge, Wilaya ya Misenyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi hizi zinakwenda sambamba na salamu za Wasaidizi wa Mheshimiwa Rais, nikitoa pongezi kubwa kwa Mheshimiwa Waziri, Prof. Mbarawa, kwa kazi nzuri pia na Naibu Mawaziri wako Ndugu yangu, Mheshimiwa Eng. Kasekenya na Mheshimiwa Atupele Mwakibete kwa kazi nzuri mnayoifanya katika eneo la ujenzi na uchukuzi. Pia niwapongeze Makatibu Wakuu wote wawili wa sekta zote mbili na Naibu Makatibu Wakuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, niwapongeze watendaji wenu ambao wako ndani ya Mkoa wa Kagera wakiongozwa na Engineer Yudas Msangi, Meneja wetu wa Mkoa wa Kagera pamoja na wasaidizi wake ndani ya ofisi hiyo, wanafanya kazi nzuri kwa yale malengo na kazi mnazowapangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mambo mawili makuu ambayo nitaongelea, nitashukuru lakini pia nitaomba. Suala la shukrani la kwanza, nishukuru Mheshimiwa Rais kupitia Wizara hii kwa kutujengea daraja zuri na kubwa la Kitengule, na Mheshimiwa Waziri umekuja pale, lile daraja limekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na daraja hilo Mheshimiwa Waziri ukatuahidi barabara ya kilometa 25 ya kutoka Kibaoni – Bunazi kwenda mpaka Kitengule. Ninakushukuru sana kwa sababu uliahidi na manunuzi yameshafanyika na mkandarasi sasa hivi anafanya mobilization kwa ajili ya kuanza kazi. Kwa hiyo, ni faraja njema, nikufikishie salamu za upendo, na shukrani zimuendee pia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru pia kwa kutekeleza ahadi za viongozi. Katika Serikali ya Awamu ya Tano, Mheshimiwa Rais aliahidi barabara ya Mutukula kwenda Minziro. Hii barabara ilikuwa inapita katikati ya msitu. Na Mheshimiwa Waziri mkamtuma Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Kasekenya akaja pale akaona hali halisi. Leo tunavyoongea mmeshafumua ule msitu na barabara inaendelea kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, ambacho ninaomba katika eneo hilo, speed ya utengenezaji wa barabara hiyo siyo nzuri. Mategemeo mazuri ya wananchi wa Mutukula na Minziro kurahisisha usafirishaji katika eneo hilo basi niombe kwa kazi nzuri mliyoianza iweze kukamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa ujumla barabara zote zinazosimamiwa na TANROADS, nikiangalia barabara ya Katoma kwenda Bukwali, ipo katika kiwango kizuri. Barabara ya Amshenyi kwenda mpaka Ruzinga iko katika kiwango kizuri, barabara ya Kibaoni – Kasambya – Mutukula – Minziro iko katika hali nzuri, barabara ya Bukoba Mjini – Mutukula iko katika hali nzuri. Kwa hiyo, hii ni kazi nzuri ambayo TANROADS mnafanya, tunachoomba ni maboresho na kuhakikisha kwamba sasa tunaboresha kutoka katika hatua tuliyopo kwenda katika hatua nzuri zaidi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe maombi kwa ajili ya Wanamisenyi na Wanajimbo la Nkenge. Suala la kwanza Mheshimiwa Waziri, Profesa Mbarawa pamoja na Wasaidizi wako, Mheshimiwa Rais alifanya ziara Mkoani Kagera na akatembelea Wilaya ya Misenyi. Tukamuomba barabara ya Katoma – Bukwali, kilometa 35.7. Ni miaka 10 mpaka leo inajengwa, mpaka sasa hivi imejengwa takribani kilometa saba. Kila mwaka tunajenga mita 200, mita 500 Mheshimiwa Rais aliwapa matumaini mazuri Wanamisenyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, sasa kama ulitembea mara moja Wilaya ya Misenyi ukatupatia kilometa 25, hizi kilometa 35 ambazo umeshaanza kujenga zinakwama wapi? Nikuombe kwa bajeti hii ya mwaka huu tupatie angalau nusu ya kilometa za barabara ile ambayo ni kilometa 35, tukipata 17 mwaka unaokuja tukamaliza ili sasa tuweze kuomba barabara nyingine za lami za Amshonye kwenda Ruzinga au kutoka Kasambya kwenda Minziro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najua hilo liko ndani ya uwezo wako, nikuombe sana katika eneo hili muweze kulifanyia kazi. Kwa sababu ukiangalia hata Hansards za Bunge, michango yangu yote katika Wizara yako kila siku tunaongea barabara hii. Mheshimiwa Profesa Mbarawa na wasaidizi wako, najua hili liko ndani ya uwezo wako. Ninakuomba baada ya kumaliza hii bajeti Jumatano mimi nitakuwa mteja wako wa kwanza ofisini kwako ili tuyajenge ili tuhakikishe kwenye orodha ya barabara ambazo kidogo umetengea bajeti, tuweze kuwa na bajeti ya barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kwamba barabara ya Kyaka – Katoro – Ibwera na Kyetema. Barabara hii ambayo inaunganisha Wilaya ya Misenyi na Wilaya ya Bukoba Vijijini kwa Kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Jasson Rweikiza imeshafanyiwa usanifu. Tukuombe sana, ukitoka Kyaka – Katoro – Ibwera mpaka Kyetema ni barabara ya muhimu na ukiangalia katika barabara zako, barabara ambayo kidogo imechoka kuliko zote ni barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo kwa niaba ya wananchi wa Misenyi, lakini naunganisha na wananchi wa Bukoba Vijijini, nikuombe sana eneo hili uweze kulizingatia ili barabara yetu ipate uwezeshaji na iweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine kwa niaba ya wananchi wa Misenyi ni barabara ya Mpakani, Mutukula mpaka Makao Makuu ya Mkoa. Mheshimiwa Waziri, hii ni barabara ya lami unaijua, inapitika, lakini inahitaji maboresho makubwa. Tunajua kwamba barabara hii iko katika mpango wa barabara za East Africa, lakini Mheshimiwa Waziri, ni miaka mingi barabara hii imekuwa kwenye programu hiyo. Kama ikionekana kwamba huu utaratibu wa barabara za East Africa kujengwa, basi Mheshimiwa Waziri tukuombe utafute mafungu mengine ili barabara ya Mutukula ambayo inapita kata za Nsunga, Kasambya, Kyaka, Bugorora mpaka kuja Bukoba Mjini iweze kujengwa kwa kiwango cha Afrika Mashariki na iweze kuwa katika standard inayotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri lakini kama tunaona sasa utaratibu huo uko mbali basi nikuombe barabara ile ni uso wa nchi ukiwa unatokea Uganda, hiyo inaonesha sura ya Tanzania kwa wenzetu wanaotoka Uganda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia jinsi barabara ilivyo, basi tuiboreshe tuweke na taa za barabani kutoka Mutukula kupita Nsunga – Kasambya – Kyaka – Bugorora – Mushasha mpaka Bukoba Mjini, nafikiri inaweza ikawa na image ya nchi, mtu akiwa anaingia Tanzania anaona kweli hapa ni eneo ambalo ni Tanzania kwa sababu barabara zake zote ni nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, katika barabara hii wananchi wale ambao barabara hii ya East Africa itajengwa walisimamishwa kwa sababu maeneo yao yalichukuliwa kwa ajili ya upanuzi wa barabara mpaka leo wananchi hawajalipwa fidia. Sasa wananiuliza Mbunge, je, tuendelee na shughuli zetu au tusubiri barabara inakuja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Prof. ninakuomba sana, kwa sababu nakuaminia, wakati wa kuja kuhitimisha utuambie kama tuendelee kusubiri tunasubiri, subira yavuta kheri. Lakini kama hilo wazo halipo basi Mheshimiwa Waziri nikuombe sasa uweze kuleta majibu ambayo yatatusaidia sisi wananchi wa Misenyi kuwa na jibu ambalo ni sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, suala lingine ni suala la barabara ya Mutukula – Minziro. Nimeshukuru kama nilivyosema mwanzoni. Lakini katika eneo hili, kama nilivyosema, speed yake siyo nzuri na uwezeshaji unakuwa siyo mzuri, nafikiri bajeti siyo nzuri. Mimi niombe, kati ya vitu ambavyo nitaomba kuja ofisini kwako Jumatano baada ya bajeti, baada ya barabara ya Katoma – Bukwali basi na hii barabara ya Mutukula – Minziro ili uweze kuliangalia kwa mapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, ombi la Wanamisenyi na Wanakagera kwa ujumla lingine ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kajunguti. Hili tumekuwa tukilichangia, lakini Mheshimiwa Waziri, kwa weledi wako unafahamu sekta yako yote ya uchukuzi na ujenzi. Unajua kwamba uwanja huu ni uchumi mkubwa wa Mkoa wa Kagera na nchi yetu kwa ujumla. Unajua kwamba uwanja huu unaunganisha nchi yetu na Nchi sita za Uganda, Kenya, South Sudan, Rwanda na Burundi na hii itainua uchumi wa Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kwamba sehemu hii, uwanja huu, wananchi walizuiliwa kuendeleza maeneo yao ili kupisha uwanja ni miaka mingi Na gharama za uthamini zilishafanyika. Mheshimiwa Waziri, nikuombe, wakati unakuja kuhitimisha basi na huu Uwanja wa Kajunguti uutolee neno tuone kwamba unakuja kuanza kujengwa au wananchi wanapewa fidia au uthamini unarudiwa upya? Tunaloomba kwa Wanakagera ni kuona uwanja huu unaanza kujengwa au basi hatua za awali zinaanza kwa ajili ya kujenga uwanja huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine la Wana-Misenyi ni kuona barabara zile zote ambazo ziko katika mpango wa matengenezo, ziendelee kutengenezwa. Vile vile kuna barabara ambazo zinazilisha hizo barabara zako ambazo zinaunganisha kwenda mpaka mpakani mwa nchi ya jirani. Kwa mfano, tukiangalia barabara ya Abunazi kwenda mpaka Kakunyu, kuna sehemu ambayo barabara hiyo inaenda inapita Mugango mpaka mpakani mwa Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo barabara ambazo zinaunganisha nchi nyingine ni za kwako, lakini ziko chini ya TARURA ambazo zimekuwa hazitengenezeki. Sasa wewe unatengeneza kipande cha nyuma chote vizuri, lakini kwa sababu bajeti haitoshi, ile barabara ya Bugango kwenda mpaka mpakani mwa Uganda, inakuwa iko katika kiwango kizuri. Pamoja na kwamba ni jukumu letu kuomba upandishwaji wa hadhi wa barabara hizo, lakini naomba kupitia ofisi yako na hilo ulione kwa sababu wewe unaunganisha Taifa na Mataifa ili barabara hiyo iweze kutengenezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine ambalo ni la kitaifa lakini linagusa maeneo mengine ambayo nimeona hapa Dodoma, Mheshimiwa Waziri niwapongeze sana kwa ujenzi wa reli ya mwendoksi ambayo inaendelea vizuri, lakini wakati reli inajengwa kuna maeneo ambayo yalichukuliwa ambayo ni sehemu ya miundombinu ya barabara ambayo iliziba wale watu ambao walikuwa wanahudumiwa na hizo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nikiangalia katika eneo la Dodoma hapa, nikianzia Njedengwa na Kisasa juu kote ambapo barabara yenu ya SGR inapita, sasa maeneo hayo, pembeni mlijenga barabara ambayo ilikuwa inasaidia miundombinu ya magari ambayo yalikuwa yanajenga barabara ya mwendokasi, lakini sasa hivi mmeziba. Nimeona mmeweka poles, mnaziba. Sasa wale wananchi unakuta kulia ana nyumba, kushoto ana nyumba, barabara aliyokuwa anatokea ni hii ya mbele ambayo sasa hivi unaweka uzio na kuweka fence.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua sheria ipo ndiyo mnayoisimamia, lakini naomba busara sasa itumike katika eneo hili ili wananchi hao, hii barabara ambayo ilitumika kipindi cha ujenzi, bila kuathiri miundombinu yetu ya SGR basi mweze kuona jinsi ambavyo mnaweza kuruhusu wananchi wakaitumia.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Ninaunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)