Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia katika Wizara yetu ya Ujenzi na Uchukuzi. Nami kama walivyosema wenzangu, kwanza natoa shukurani za dhati kwa Rais wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake mkubwa wa kuendelea kufanya kazi katika nchi yetu. Anasema, hakuna kilichosimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tulikuwa Ikulu tunazindua jengo, kuna watu walifikiri litasimama, halijasimama; mradi mkubwa wa Maji wa Bwawa la Nyerere, haujasimama unaendelea; Daraja la Busisi halijasimama, linaendelea. Sana sana vile vilivyosimama, sasa hivi vinaendelea. Mfano ni barabara yetu ya Ifakara – Kidatu ilikuwa imesimama huko nyuma na sasa inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno mazuri haya yanathibishwa na kauli ya kaka yangu Mheshimiwa Freeman Mbowe, anasema mama anaupiga mwingi sana na mama anafanya kazi kubwa. Mheshimiwa Mbowe ameanza kumwelewa mama sasa hivi, hawaongei tupu tupu, wanaanza hata kufanya fanya miradi ya maji, nimeona huko, na wakichangisha pesa wanazibakiza kwenye vijiji, hawaondoki nazo zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii yote ni uthibisho wa uongozi mzuri wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujenga umoja wa nchi yetu na tunamuunga mkono tunampongeza sana. Mheshimiwa Waziri wewe na watumishi wako wote katika Wizara hiyo, tunawashukuru sana na tunawapongeza sana kwa kazi mnayofanya. Wenzangu wametangulia kusema Wizara hili ni kubwa na kazi ni kubwa kweli kweli na maneno ni mengi, lakini wote ambao Mheshimiwa Rais amewaamini, endeleeni kumsaidia, onyesheni uwezo wenu katika kufanya kazi kubwa na wasaidizi wako wengine kama ma DG Bandari na akina Kadogosa huko ni vijana wadogo, wameanika sana katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaambia sisi tunajua ipi ni ipi, na ipi siyo ipi? Kama kuna maneno mengine ya kuupuza, wayapuuze waendelee kufanya kazi. Watu wanataka kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kwa reli. Walale Dar es Salaam waje wafanye kazi Dodoma warudi Dar es Salaam kula bata, Mji wa kibiashara, mama kashasema na kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri amekuja hapa leo anaomba 3.5 trillion katika bajeti yake na nina imani Bunge litampitishia bajeti yake. Tunamwomba sana na tunaiomba Serikali hasa Waziri wa Fedha ahakikishe fedha hizi zinakuja kwa wakati ili miradi hii itimie. Kwa mfano, Serikali kufikia mwaka Februari, 2023 katika sekta ya ujenzi imetoa fedha za kutosha karibu 85 percent, lakini ukienda kwenye uchukuzi kule kweli fedha ni chache ni asilimia 59 tu peke yake. Kwa hiyo, tunaweza tukapitisha hapa bajeti lakini utoaji wa fedha ukichelewa, automatically miradi itapungua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya ujenzi, Wizara ya Ujenzi ni mambo ya fedha tu. Sasa ni muhimu sana kama kuna maeneo Mheshimiwa Waziri mnaweza kufanya uwekezaji, ambavyo Mheshimiwa Rais amesema na Wabunge wenzangu wengine wamechangia, yatakayozalisha fedha za kutosha msiyacheleweshe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza hapa, na hii ni mara ya pili nazungumza. Rais wa nchi, kiongozi wa nchi Dkt. Samia Suluhu Hassan anasema tukiwekeza katika bandari tunaweza kupata nusu ya bajeti ya nchi yetu. Hili siyo jambo dogo, ni jambo kubwa sana kusema nusu ya bajeti ya nchi yetu. Sasa hapa tunazungumza, Wabunge wote tunadai fedha. Tunadai fedha, lakini hili jambo kwanini mnalichelewesha? Kwanini mnasema mnachelewesha uwekezaji katika bandari? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Rais, alienda Dubai mwaka 2021 katika Dubai Expo, tukamwona Waziri wa Kilimo na Waziri wa Viwanda. Mheshimiwa Waziri ulikuwepo pale, watu wa bandari walikuwepo pale. Mkaonesha fursa siku nzima pale za nchi yetu, mkapata wawekezaji, mkaanza kuzungumza katika mikata ya nchi na nchi kushirikiana. Jambo mojawapo likiwepo ni bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Dubai na Dubai Port, wameonesha nia nzuri ya kutusaidia katika Bandari yetu, DP World. Agreement imeingiwa pale, mchakato hatuoni unaendelea. Tumekwama wapi? Wekeni jambo hili wazi, muungeni mkono Mheshimiwa Rais tupate fedha hizi. Hii bandari imebinafsishwa huko nyuma, imeshabinafsishwa sana, wanasema ooh, usiogope, usiseme, ukisema watu wakubwa; huko nyuma ilikuwepo tangu enzi ya Mkapa mmeweka wapi? Sasa leo Dubai inafanya vizuri duniani, watu wanakimbilia Dubai, Serikali ya Dubai, DP World wanataka kuja kuwekeza katika bandari yetu. Cha msingi, mtuweke wazi, mnawekeza nini? Ajira za Watanzania zitakuwa ngapi? Tunapata Shilingi ngapi? Sasa hivi tulikuwa tunapata Shilingi ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato, thirty five percent ya TRA ni karibu Shilingi trilioni saba wanachukua bandarini. Akija mwekezaji tunapata Shilingi ngapi? Wafafanulieni Watanzania, wata-support uwekezaji huu na bandari haiuzwi, haibinafsishwi tunaingia mashirikiano ya uendeshaji. Hawa DP World wanaendesha nchi saba Afrika ya Bandari. Duniani wana bandari 70. Hapa tunafanya siasa, siasa nusu ya bajeti ya fedha tunaikosa. Ukienda huyu wanamkuta huyu; mfanyabiashara anataka kwenda bandarini anachafua wengine, vurugu. Muungeni mkono Mheshimiwa Rais, agreement hiyo imeshaingiwa, imeshasainiwa kule Dubai, mchakato wa pili ufuate na mchakato wa tatu ufuate tuweze kunufaika kama wenzetu wa Senegal, Algeria, na Egypt ambapo DP World wako kule na wanawekeza kitu kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumalizia kwa kusema kwamba, kwa upande wangu wa Jimbo, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri, umekuja Kilombero mara mbili. Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 nilijua ajenda ya Barabara ya Kidatu – Ifakara ni kubwa. Pale Jimboni Kilombero hujakamilisha barabara hii, miaka yako mitano unasepa. Kwa hiyo, nikakaa na wazee wakaniambia, tumezunguka kwenye kampeni tumesema barabara ile isipojengwa hatugombei tena. Ndiyo maana unaona tumelala kwenye matope, tumekaa kwenye kapeti Bungeni, kilomita 66.6. Mheshimiwa Waziri leo karibu kilomita 50 mmeweka. Hiyo ni kasoro kama 15 au 16 hivi ambazo mimi naomba Mungu ngoma hii imalizike hiyo, iishe. Sasa Mheshimiwa Waziri unanijengea barabara mpaka roundabout ya Ifakara pale kibaoni, ni kama kilomita tano za mjini unaziacha, ile kilomita tano ya lami ya zamani ni ndogo sana…

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Abubakari kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Taletale.

TAARIFA

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa ndugu yangu Mheshimiwa Asenga, naona anachangia kwa furaha sana, nami natamani furaha yake ihamie kwetu jibu la Kisaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa. Ndiyo ukae vizuri na Profesa Mbarawa, na muda wangu ananiishia.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Asenga, taarifa unaipokea?

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea. Akae karibu vizuri na Waziri hapa apate matunda mazuri. Profesa Mbarawa ni msikivu, Engineer Isack ni msikivu, Engineer Mativila ni msikivu, watamsadia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema Waziri anatujengea barabara mpaka roundabout ya Kibaoni. Barabara hii ikikamilika keshokutwa, mabasi yatapita mjini kwenda Ulanga, kwenda Malinyi, kwenda Mlimba, Ifakara Mjini hapatoshi. Tunaomba ile barabara ya kilometa 10 ya mchepuko ya Mbasa – Katindyuka ijengwe kwa lami watu walipwe fidia. Ndiyo matunda ya barabara ya Ifakara – Kidatu yatatokea. Maana vinginevyo tunaenda kupeleka msongamano Ifakara Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameelekeza barabara kubwa hizi zinazopita kwenye vijiji, mweke taa za barabarani. Kidatu – Sanje – Mkuwe – Mang’ula A – Mang’ula B – Mwaya – Kiberege – Kisawasawa, wekeni taa kwenye vijiji barabarani. Watu wanauza maembe, wanauza ndizi jioni kwenye vituo vya daladala. Waziri Mkuu kaelekeza, nataka kujua kama mnatuletea taa za barabarani ama hamtuletei?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemwona Naibu Waziri wa Uchukuzi. Ifakara ina kituo kikubwa sana cha TAZARA, Ifakara tuna Uwanja wa Ndege sasa hivi kutokana na Mradi wa Kupambana na Malaria wa Ifakara Health ambao Mheshimiwa Rais alienda Marekani. Wanafugwa mbu Ifakara pale, ndege zinatua miruko mpaka 50 kwa mwezi. Kila siku karibu inatua ndege ndogo, uwanja wetu haufai. Waziri wa Uchukuzi tunakuomba, kwa sababu barabara hii ya Ifakara – Kidatu sasa hivi inaishia kilomita moja kwenda Airport, kwenda TAZARA tuunganishie hizo kilomita moja ama mbili tuunganishe na hii barabara kubwa na Airport, barabara kubwa na TAZARA. Ni jambo ambalo linaweza kusaidia Kata yetu ya Kibaoni ikachangamka kwa sababu ni Makao Makuu ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa taa za Ifakara Mjini na TANROADS barabara ile lakini ni kilomita mbili tu umefunga taa katika kilomita tano nilizokuomba. Tuletee hizo taa zilizobaki Mji wetu uendelee kuchangamka na sisi ni wauzaji wazuri wa mchele mzuri, unaonukia. Wanakuja Watanzania wengi sana kununua mchele kule, Wazanzibari wako wengi pale Ifakara. Taa zile zitasaidia mji wetu utapendeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti la mwisho. Juzi tumekutwa na mafuriko. Nimeenda na Meneja wako wa TANROADS Mkoa Eng. Razak, mtu mzuri. Baada ya mafuriko tu amekuja, ametazama makalavati yale na changamoto zake. Ameona, amesema yuko tayari kutusaidia endapo Waziri utamsaidia. Msaidie Engineer atusaidie jambo hilo la makalavati, atusaidie ahadi ya Mang’ula Kona. Mheshimiwa Waziri, umefika Mang’ula Kona, umeona pressure ya watu, ahadi ya chama ya Mang’ula Kona. Nimeambiwa karibu shilingi milioni 300 zinatakiwa kukata ule mlima wa hifadhi ambao Rais ametupatia kwa nia njema ya kuondoa kero ya wananchi. Mheshimiwa Waziri tusaidie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)