Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kutuwezesha kuendelea kufanya kazi ya Bunge letu tukiwa tunajadili Bajeti ya Wizara mbalimbali na leo tuko Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niendelee kukushukuru wewe Mwenyekiti pamoja na uongozi mzima wa Bunge kwa kuendelea kuendesha Bunge letu vizuri. Zaidi ya yote namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuongoza Taifa letu vizuri na kuendelea kulipa heshima kimataifa na zaidi ya yote kuendelea kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nitoe salamu za pekee na pongezi za pekee kwa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na Wizara hii, Profesa Mbarawa na wasaidizi wake wote wawili, Naibu Waziri wa Uchukuzi na Naibu Waziri wa Ujenzi kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Hili nataka niweke maneno maalum hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ni Wizara mbili ndani ya Wizara moja. Wizara hii ina taasisi 22 inazozisimamia, lakini ipo taasisi moja tu au zipo taasisi ambazo taasisi moja peke yake ingetosha kuwa Wizara. Kwa mfano, Taasisi kama Shirika la Reli, yaani ingeweza ikatosha kuwa Wizara. Zipo nchi nyingine Shirika la Reli ni Wizara peke yake. Kwa hiyo, unapoona watu hawa wanachapa kazi ya kusimamia taasisi 22, kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana na wanastahili pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka nirudie maneno yangu ambayo nimekuwa nikiyasema mara nyingi, kwamba mnaposikia tunakosoa, tunaelekeza au tunashauri baadhi ya vitu, hatumaanishi kwamba kazi haifanyiki, Hapana. Isipokuwa hata kilicho bora, huboreshwa. Kwa hiyo, wanafanya kazi nzuri, lakini tunataka wafanye kazi nzuri zaidi. Ninyi ni mashahidi, mmeona barabara zilizokamilika zilizooneshwa hapa, mmeona viwanja vya ndege vilivyokamilika na mambo chungu mzima. Kwa hiyo, nawapongeza sana hawa wachapakazi na ninawatia moyo, endeleeni kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nianze na meli katika Ziwa Tanganyika. Nimesikia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia meli ya Liemba ambayo sasa imesimama kwa miaka saba, wananchi wa Ziwa Tanganyika wakiwa hawapati huduma kwamba itaanza kukarabatiwa mwezi Juni mwaka huu, yaani mwezi kesho na kwamba itachukua takribani miezi minane kukamilika na kurudi majini. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kwanza hii kauli umeitoa hapa Bungeni sisi tunaiunga mkono. Nami niliyesimama hapa, mbali na kuwa ni Mbunge wa Kigoma Mjini, lakini kutokana na matatizo tuliyonayo katika Ziwa Tanganyika ya huduma mbalimbali, tumetengeneza umoja wetu wa Wabunge wa mikoa ya Ziwa Tanganyika ambayo ni Kigoma, Rukwa na Katavi, nami ndio Mwenyekiti wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie, hii ni mara ya mwisho kusimama katika Bunge hili kuunga mkono bajeti ya Wizara hii kama hakutakuwa na meli kwenye Ziwa Tanganyika. Narudia maneno haya ili Watanzania wote wasikie. Hii ni mara ya mwisho kusimama katika Bunge hili kuunga mkono bajeti ya Wizara hii kama mpaka tutakapoingia kwenye bajeti nyingine meli hazitakuwepo kwenye Ziwa Tanganyika. Nasema hivi kwa sababu zifuatazo: Wale waliosimama katika umoja na kuishinikiza Serikali katika Lake Victoria sasa hivi wana meli tano zinafanya kazi; MV. Clarius, MV. Victoria, MV. Butiama, MV. Umoja na sasa MV Mwanza Hapa Kazi Tu, nayo imeingia majini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lake Tanganyika hakuna meli hata moja inayofanya kazi. Narudia, hii itakuwa ni mara ya mwisho kuunga mkono bajeti kwa namna yoyote ile itakayokuwa, kwa shinikizo la mtu yeyote yule, hatutaunga mkono bajeti kama meli hazitakuwa ziwani mpaka tunakuja kwenye bajeti nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, MV Mwongozo mmeisimamisha sasa kwa takribani miaka mitano, mnasema mmesimamisha kwa sababu MV Bukoba ilizama na MV Bukoba ni meli pacha wa MV Mwongozo. Mlisema mtengenezaji ni mmoja kwa hiyo hizo ni meli pacha. Mkasema kwa sababu ile ilipata ajali, mkaisimamisha na hii. Ni maneno ambayo ukimwambia mtu hawezi kuelewa. Kuna ndege imepata ajali juzi hapa, sijui mmesimamisha ndege zote za aina hiyo! Maana hii meli ilikuwa inafanya kazi Lake Tanganyika na haikuwa na tatizo lolote. Lake Tanganyika kuna mawimbi makubwa kuliko Lake Victoria, na imekuwa ikisaifiri, haina tatizo, mkaisimamisha. Haya, nia yenu ni njema, mmeisimamisha ili kutengeneza stability iwe stable. Mpaka leo duniani hajapatikana mtu wa kutengeneza stability ya meli hii kwa miaka mitano. Hili ni jambo la aibu sana kwa wataalam waliosomeshwa na Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 94 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia haja ya Serikali kutaka kushirikisha sekta binafsi katika kuboresha bandari zetu. Napongeza sana hatua hii na nimekuwa nikiisemea sana humu Bungeni. Hatua hii ni utekelezaji wa Ilani ya CCM. Ukienda kwenye Ilani ya CCM, Ibara 18(b) (5) kinaeleza hivi nanukuu: “Kuongeza wigo wa upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kutekekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia mfumo wa ubia baina ya Serikali na sekta binafsi (Public Private Partnership - PPP).”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ni sera ya CCM na ambayo tunasuasua sana katika kuitekeleza. Nataka niseme hapa, katika maeneo ambayo tumejaribu, tumefanikiwa, mnachelewa nini? Kwa mfano, niseme Bandari ya Dar es Salaam, pamoja na matatizo yote ambayo tumekuwa tukiyasikia juu ya TICTS, lakini bado tumepata faida ya kuwaweka TICTS katika magati manne. Gati Na. 8, Na. 9, Na. 10 na Na. 11, kuliko hata walivyokuwa TPA peke yao wanasimamia magati yote 11 ya Bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa wanasimamia TPA, Serikali ilikuwa inapata gawio kati ya Shilingi bilioni 180 hadi Shilingi bilioni 200 kwa mwaka, lakini kwa TICTS peke yake kwa magati manne tulikuwa tunapata kati ya Shilingi bilioni 300 hadi 345. Kwa hiyo, pamoja na matatizo ya TICTS yaliyokuwepo na ambayo yanatupa fundisho la kwamba tukimpata mtu mwingine tunayetaka kuingia naye ubia, lazima tuangalie zile changamoto tulizozipata kwa TICTS, lakini Serikali msije mkajiingiza katika jambo la kusema acha tufanye wenyewe, hakuna. Tafuteni wabia, tuendelee kutumia mfumo wa PPP, huo ndio utakaotutoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati wa reli kati ya Kigoma, Tabora na Mabehewa. Hili nalo limekuwa linatengwa kwenye bajeti kila mwaka na bado utekelezaji haupo. Utekelezaji unasuasua. Reli kutoka Tabora kwenda Kigoma ambayo ni kilometa 411 tu, bado hali yake ni mbaya. Nashukuru Serikali mliahidi hapa Bungeni, tena mimi mwenyewe ndiye niliyeuliza swali, mkasema mtaleta mabehewa mapya 22. Naipongeza sana Serikali, imeleta na mabehewa hayo yamesaidia sana na safari za Kigoma - Dar es Salaam zimeongezeka kutoka mbili kwa wiki hadi tatu kwa wiki. Ila mabehewa mliyoahidi ambapo mlisema mtakarabati mabehewa 37, mpaka leo hayajaingia kwenye reli ili kusaidia kuongeza safari zifike hadi nne au tano kwa wiki.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kilumbe, ahsante sana. Muda wako umeisha.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)