Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii adhimu na adimu, kwanza kabisa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenipa kibali mimi pamoja na ninyi tukaweza kukutana, lakini vile vile tukaweza kujadili hoja iliyokuwa mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, kipekee nishukuru kuwa mmoja miongoni mwa wachaingiaji wa hoja hii iliyokuwa mezani ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Pili, nichukue nafasi hii kipekee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kutuamini mimi na Profesa Mkenda kuweza kutupa mamlaka na madaraka ya kuweza kushiriki kwenye uongozi wa Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa ushirikiano, kwa maelekezo, kwa miongozi mbalimbali ambayo imeniwezesha kushiriki lakini vile vile kuweza kuongoza Wizara hii. Vile vile nimshukuru sana Katibu Mkuu, Profesa Nombo, Naibu Makatibu Wakuu, Kamishna wa Elimu, Wakurugenzi wote na Menejimenti nzima ya Wizara ya Elimu pamoja na taasisi zilizokuwa chini ya Wizara ya Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nikushukuru wewe binafsi kwa kuliongoza Bunge letu, Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge lakini vile vile na Kamati yetu ya Elimu na Wabunge wote. Tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano ambao wanaotupa ili kuweza kurahisisha majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee naomba nichukue fursa hii vile vile kuwashukuru sana wananchi wangu, wapiga kura wangu wa Jimbo la Mafia. Kwanza kwa kuniamini, lakini pili kwa kuendelea kunipa ushirikiano. Pamoja na majukumu mengine haya ya Kiserikali lakini bado jimboni kule salama na kila nikienda wananipa ushirikiano wa kutosha ndani ya chama pamoja na wananchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho, naomba niishukuru sana familia yangu kwa kuwa karibu na mimi katika kipindi chote wakati natekeleza majukumu yangu. Tunashukuru kwa hoja ambazo tumezipata, tumezipokea. Nichukue fursa hii niwatoe wasiwasi na hofu Waheshimiwa Wabunge kwa yale yote ambayo wamechangia kwenye Wizara yetu, tutakwenda kuyasimamia. Kuna maeneo ya ushauri, kuna maeneo ya maelekezo, lakini kuna maeneo ya maagizo na kuna maeneo vile vile vya marekebisho. Tutakwenda kuyasimamia haya yote waliyoyapendekeza katika utekelezaji wetu wa bajeti katika mwaka ujao wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa uniruhusu nami niweze kuchangia kwenye baadhi ya maeneo katika hoja iliyopo mbele yetu. Eneo la kwanza naomba kuchangia kwenye eneo la ujenzi wa vyuo vyetu vya VETA.

Mheshimiwa Spika, kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi nafahamu iko Ibara ambayo inazungumzia Serikali itakwenda kujenga vyuo vya VETA kwa lengo la kusogeza huduma ya elimu haswa ya ufundi karibu na wananchi na Serikali imejidhatiti kuhakikisha kwamba tunajenga.

Mheshimiwa Spika, tulianza ujenzi huu karibu miaka miwili iliyopita katika mwaka wa fedha 2020/2021 lakini tumeweza kuendelea nao katika mwaka 2021/2022 tumeweza kujenga vile vyuo 25 katika Wilaya 25 nchini lakini baadae na vile vyuo vinne vya Mikoa. Katika mwaka huu wa fedha tumeweza kuanza ujenzi katika Wilaya zile 64 ambazo zilikuwa hazina vyuo vya VETA na katika Mkoa mmoja wa Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge tutaenda kusimamia eneo hili kwa uadilifu na uaminifu mkubwa,tayari shughuli za ujenzi kule zimeshaanza. Tunafahamu ziko Wilaya ambazo zina Majimbo zaidi ya moja, kulitokea malalamiko mengi humu kwamba tunakwenda kujenga katika Wilaya na siyo katika Majimbo. Niwaondoe hofu Waheshimiwa Wabunge tunajua kuna baadhi ya Majimbo, tunajua kuna baadhi ya Halmashauri zimetenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivi lakini categorically tulisema kwamba tunakwenda kujenga katika Wilaya na siyo Halmashauri au Jimbo.

Mheshimiwa Spika, niwaondoe hofu tumepokea hoja zenu. Mipango ya Serikali ni mingi na mikubwa sana, tutakwenda kuangalia namna gani ya kufanya ili huduma hii iweze kufika katika kila Jimbo na katika kila Halmashauri. Hilo eneo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo tulisema niweze kulizungumza na katika Mradi wetu wa HEET ambao ni mradi wa vyuo vikuu. Tunafahamu Mheshimiwa Rais ametoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 972 kwa ajili ya kuongeza au kuboresha mazingira ya vyuo vikuu nchini. Fedha hizi zitakwenda kutumika katika maeneo makubwa matatu. Eneo la kwanza ni kwenda kujenga miundombinu katika vyuo vikuu hivi vilivyopo lakini vilevile kwenda kujenga kampasi nyingine mpya.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni kufundisha walimu, wahadhiri mbalimbali ili kuwaongezea ubora. Tumezungumza hapa Profesa Ndakidemi amezungumza, Profesa Muhongo saa hizi ametoka kuzungumza kwamba ubora wa vyuo vyetu, hatuwezi kuwa na vyuo bora bila kuwa na mazingira bora. Kwa hiyo eneo la kwanza tunakwenda kujenga miundombinu lakini eneo la pili tunakwenda kufundisha wahadhiri wetu, eneo la tatu tuhakikishe kwamba ni lazima tuwe na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Kwa hiyo, fedha hii tunakwenda kuitumia zaidi ya asilimia 75 itakwenda kwenye hizo infrastructures.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo ya namna gani tunaweza tukatumia fedha hii na alielekeza kwamba tusogeze huduma za elimu ya juu karibu na wananchi. Kwa mantiki hiyo, taasisi ambazo zitanufaika na fedha hizi karibu taasisi 19 na vyuo vikuu karibu 14 lakini na taasisi nyingine mfano, Taasisi yetu ya Elimu ya Juu (TCU) nayo itafaidika na fedha hizi, Bodi ya Mikopo itafaidika, amezungumza hapa Profesa Muhongo. Taasisi yetu ya COSTECH nayo vilevile tunaendelea kuifanyia reform kubwa sana. Fedha hii itakwenda kutumika katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, naomba niitaje Mikoa ile michache ambayo itakayokwenda kunufaika moja kwa moja au tunakwenda kujenga kampasi mpya kabisa katika Mikoa ambayo ilikuwa haina kampasi hizo. Mkoa wa kwanza ni Mkoa wa Katavi, tutakwenda kujenga huko, Mkoa wa pili Mkoa wa Lindi tunakwenda kujenga, Mkoa wa Tanga, Tabora, Ruvuma, Manyara, Shinyanga, Singida, Geita, Kigoma, Kagera, Mwanza, Rukwa na Mkoa wa Simiyu. Mikoa hii yote tunakwenda kufanya kazi, mchakato uko katika hatua za mwisho. Tulianza kwanza na feasibility study wameshafanya procurement ya consultant na sasa tunafanya procurement ya contractors na tayari kazi inakwenda kuanza ndugu zanguni. Kwa hiyo, naomba niwaondoe hofu jambo hili linakwenda kufanyika kwa uaminifu na uadilifu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu ni eneo la Wadhibiti Ubora; limezungumzwa sana suala la Wadhibiti Ubora na tunafahamu kwamba kulikuwa na waraka toka mwaka 2014, namna gani wadhibiti ubora wanakwenda kuwa na stahiki zile zao za kawaida lakini vilevile mishahara. Ni kweli waraka ule hatujaweza kuutekeleza kwa kipindi chote hiki lakini niwaondoe hofu, Mwezi Aprili mwaka huu tulipeleka muundo mpya wa Wizara ambao umeingiza sasa hawa Wadhibiti Ubora kama viongozi na Mheshimiwa Rais tayari amesharidhia waraka ule toka mwezi wa nne mwaka huu na ifikapo mwezi wa saba, Wadhibiti Ubora wale wote wanakwenda sasa kuwa katika zile kada za uongozi wanaweza sasa wakalipwa zile stahiki kadiri mlivyoshauri tutakwenda kufanya hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu ambalo liliambatana na hilo la wadhibiti ubora ni mazingira yao ya kufanyiakazi, imezungumzwa hapa kwamba katika ukaguzi wa taasisi zetu za shule ni asilimia chache sana kama 26 tu ndiyo ambayo imeweza kukaguliwa. Niwaondoe hofu Serikali imeshafanya makubwa sana kwa upande wa Wadhibiti Ubora. Miongoni mwa mambo ambayo tayari yameshafanyika na Serikali ni ujenzi wa ofisi mpya za Wadhibiti Ubora 160 lakini tumefanya ukarabati wa ofisi za Wadhibiti Ubora 31 lakini vile vile tumenunua magari 119 na kusambaza kwenye Halmashauri pamoja na Wadhibiti Ubora katika Kanda pamoja na Mikoa mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hiyo tumeweza kufanya ununuzi wa kompyuta 195 zile kompyuta za mezani, lakini tumenunua laptop 1,082. Sambamba na hiyo tumesambaza vile vishikwambi ambavyo vilitumika. Vile vilivyogaiwa walimu vilevile wadhibiti ubora wamegawiwa. Lengo kuu hapa la Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatengeneza mazingira wezeshi ili wenzetu wadhibiti ubora waweze kufanya kazi yao katika mazingira mazuri na salama kwa sababu ndiyo jicho letu kule la kuangalia elimu ya vijana wetu.

Mheshimiwa Spika, eneo jingine ambalo ningependa labda nilifafanue kidogo ni kwenye eneo la lishe. Nalo vilevile limezungumzwa sana, mnakumbuka tulitoa Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2016 ambao ulikuwa unaeleza wazi namna gani jamii itashirikishwa kwenye suala la kutoa lishe mashuleni. Vilevile tulitoa mwongozo wa mwaka 2022 wa namna gani vile vile jamii itahusishwa.

Mheshimiwa Spika, tumepata malalamiko hapa uchangiaji ule unatofautiana kutoka eneo moja na eneo jingine. Tutakwenda kufanya marekebisho katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba vijana wetu wanapokuwa shuleni wanaweza kupata lishe ambayo itakayowawezesha kujifunza katika mazingira ambayo ni salama.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumza hayo naomba kuunga mkono hoja. Ahsanteni kwa kunisikiliza. (Makofi)