Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, napenda kupongeza hotuba ya Wizara na kwa ujumla wanavyofanya kazi kwa ushirikishwaji, napongeza sana hili linaloendelea la kuhuisha mitaala na sera, ushiriki mpana wa wadau bila shaka utasaidia kupata mawazo mapana ambayo hatimaye tutapata kile tunachokusudia.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza pia Watendaji wa Bodi ya Mikopo kuanzia Meneja wa hapa Dodoma na Mtendaji Mkuu wa Bodi Ndugu Badru na wasaidizi wake, wamekuwa msaada sana hasa wakati wa changamoto za mikopo, wapo watoto wa wapiga kura wetu wakiwa na changamoto kwa kweli watu wa Bodi ya Mikopo wako very cooperative katika kutusaidia nini cha kufanya, nawashukuru, nawapongeza na endeleeni na moyo huo huo wa kuwa solution oriented.

Mheshimiwa Spika, sasa katika vyuo, baada ya mtoto kupata mkopo kumekuwa na changamoto, mara fedha hazijaingia au zitaingia kwa awamu, nashauri vyuoni, vitengo vinavyohusika na disbursement ya funds kuwafikia wanafunzi vifanye kazi kwa speed kama wanavyofanya Bodi.

Pili, nawapongeza kwa ujenzi wa Vyuo vya VETA, hata hivyo nina ushauri na maombi maalum kwa ajili ya Halmashauri ya Mji Mafinga.

Mheshimiwa Spika, eneo hili linakua kwa kasi na hii ni kutokana na sekta ya mazao ya misitu, nafahamu kwamba kunajengwa Chuo cha VETA Mufindi, hata hivyo kwa ombi maalum, naomba katika mpango ujao kujumuisha Mafinga TC kutokana na umuhimu wake hasa kwa kuwa ni centre ya uzalishaji wa mazao ya misitu.

Kuhusu elimu ya awali; nafahamu kuna muingiliano wa majukumu katika baadhi ya maeneo ya usimamizi wa elimu kati ya Wizara ya Elimu na TAMISEMI, hata hivyo kuimarika au kuporomoka kwa elimu, mwenye dhamana ni Wizara ya Elimu, kwa sababu hiyo bado tunao wajibu wa kuyatazama kwa macho mawili baadhi ya maeneo hasa eneo la elimu ya awali. Kwa mfano, kwa ufahamu wangu ukiacha courses za early childhood katika baadhi ya vyuo vikuu, kuna vyuo maarufu kwa muundo wa ki-montesory ambavyo ni mahususi kuwaandaa walimu wa kufundisha watoto wadogo. Lakini kama Serikali tunapoajiri walimu ni nadra kabisa kuona ajira mahsusi kwa ajili ya walimu wa kufundisha watoto wadogo kwa maana ya madaraja ya awali.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu tusichukulie elimu ya awali kama ziada bali tuchukulie kuwa ndio msingi wa kuanza kumjenga mtoto kujiamini, kujitambua, kushirikiana na wenzake na hivyo kumjengea msingi wa kuanza kuwa raia bora na mwema.

Mheshimiwa Spika, kuna kama woga wa ku-declare kuwa elimu ya awali itambulike kama sehemu ya elimu ya msingi na izingatiwe na kupewa uzito katika mipango yetu kama Taifa. Ushauri wangu, tusitawaliwe na woga wa gharama na tukumbuke kauli ya Mwalimu if you think education is expensive, try ignorance. Kwa hiyo, kama tumefikia hatua ya kuhuisha mtaala na sera, ni muhimu kuifanya elimu ya awali kuwa ni jumuishi. Tusiogope maana wakati ni sasa.

Mheshimiwa Spika, wakati tunaendelea na mijadala na mashauriano kuhusu kuhuisha mitaala na sera yetu, ni muhimu tukawa makini hasa katika kuangalia wapi tulikosea na wapi tuparekebishe na kwa kiwango gani. Nasema hivi kwa sababu wapo baadhi yetu ambao tunaona kama mfumo wetu umefeli kabisa which is not, mfumo huu umewezesha baadhi ya Watanzania kufanya kazi duniani kote, wapo madaktari wanaofanya kazi nchi za Kusini mwa Afrika na wanategemewa, wapo wahadhiri wanafanya kazi katika vyuo mbalimbali duniani, lakini pia vijana wetu wanaosoma katika mfumo wa elimu yetu wanapata udahili katika vyuo mbalimbali duniani iwe ni Amerika, Ulaya, Asia, Arabuni na kadhalika hawajawahi kukataliwa kwa hoja kwamba mfumo wa elimu yetu ni mbovu au haukidhi vigezo vya Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunapofanya mapitio haya tusije tukafikia hatua kuona kama vile mfumo wetu wa elimu uliopo ni kama haufai, ni zero; hapana, lazima tujivunie mfumo wetu ulikotutoa mpaka hapa tulipo, na kwa hiyo tufanyie marekebisho baadhi ya maeneo muhimu na kwa uzito wake.

Mheshimiwa Spika, mwisho nimekuwa nikijiuliza, hivi hatuwezi kuja na utaratibu wa kidato cha tano kuanza mapema kuliko ilivyo sasa ambapo kijana anamaliza shule kwa maana ya kidato cha nne Novemba, kwenda kidato cha tano anasubiri mpaka Julai jambo ambalo ni risk sana hasa kwa watoto wa kike kukaa idle miezi almost sita. Kwa kuwa kuna maendeleo ambayo yamewezesha matokeo kutoka mapema, je, hatuoni ni wakati sasa watoto wanaojiunga kidato cha tano kuanza mapema kadri wataalam watakavyolidadavua. Nafahamu linaweza kuleta ukakasi na kuvurugika kwa mihula ya shule/vyuo lakini kwa kuwa tuna wataalam tujaribu kuwaza nje ya box kuona kama linaweza kufanyika.