Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Janeth Elias Mahawanga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JANETH E. MAHAWANGWA: Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri na kubwa iliyofanyika katika kuinua na kuboresha elimu katika Taifa letu, lakini sambamba na kuyafanya mazingira kuwa bora na ya kisasa.

Mheshimiwa Spika, pia naipongeza Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri inayofanya lakini pamoja na kuwa wanapokea ushauri mbalimbali unaotolewa na Waheshimiwa Wabunge katika kuhakikisha elimu yetu ya Tanzania inakuwa ya viwango vya ushindani kwenye soko la ajira.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Wizara iangalie sana suala la mabweni kwa shule za sekondari hasa za watoto wa kike kwani watoto hawa wanakutana na changamoto nyingi sana kutokana na umbali wa makazi wanayoishi na shule walizopangiwa mfano Shule ya Sekondari Morogoro hakuna mabweni ya kutosha kwa watoto wa kike hali inayopelekea watoto wa kike wa kidato cha sita tu ndio wanaopewa kipaumbele, lakini watoto wa kike wa kidato cha kwanza mpaka cha nne wanatakiwa wajitegemee huko nje.

Mheshimiwa Spika, kwa nini Wizara isiige mfano wa chuo kikuu wanavyofanya ambapo watoto wa mwaka wa kwanza ndio wanapewa kipaumbele cha kupata hosteli kabla ya wenyeji? Watoto wa kidato cha kwanza ni wadogo sana hata busara ya kujilinda huko nje kwenye nyumba za kupanga bado hawana, tunaomba walindwe kwa kujengewe mabweni ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, tunaomba pia Wizara iweke utaratibu mzuri wa kuwahamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi kwa kutoa motisha na kuwatambua watoto wa kike vinara kwenye masomo ya sayansi, hesabu na ufundi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia watoto wa kike ambao wanapata mimba wakiwa shuleni wanaporudi baada ya kujifungua waruhusiwe kijiunga madarasa ya watu wazima kwani wengi wao wanajisikia vibaya kurudi shule zile zile.

Mheshimiwa Spika, kuna wanafunzi ambao wazazi wao walipokuwa na uwezo walikuwa shule za private, lakini baada ya wazazi hao kupoteza maisha au kupata changamoto za kimaisha inakuwa ni ngumu sana kurudi kwenye shule za Serikali, tunaomba Kamishna alishughulikie hili kwani limechukua muda mrefu sana.

Mheshimiwa Spika, nashukuru na naomba kuunga mkono hoja.