Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Maimuna Ahmad Pathan

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hoja kwenye Wizara ya Elimu. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi yake ya uhai na kufikia siku hii ya leo. Pia naomba nitoe sifa nyingi sana kwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa sana anazozionesha kwa upande wa elimu. Ameweka majengo mengi sana, madarasa ya kutosha, kwa kweli anastahili sifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Waziri wa Elimu, ndugu yangu Profesa Mkenda na Msaidizi wake na Katibu Mkuu, Dada Carolyne na wasaidizi wake, kwa kweli wanajitahidi wanafanya kazi kubwa sana. Tumeona mitaala hii iliyotoka, kwa kweli kazi yao inaonekana, tunaendelea kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu mambo yawe mazuri ili nasi tufaidi, na nchi yetu Tanzania iwe vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuunga mkono hoja zilizopo mbele yetu mezani. Pili, nawaunga mkono Wabunge wengi waliotoka kuongea, akiwepo dada Latifa sasa hivi. Mitaala hii mipya inayokuja, tujitahidi sana tuwekeze kwa walimu. Tusipowekeza kwa walimu tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu. Walimu wapewe semina, wapewe mafunzo mbalimbali, tuache tabia ya kuanza kubagua. Najua Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wake huko Wizarani hawana nia mbaya, lakini huku chini ukishuka, kuna mambo yanaendelea siyo mazuri. Kuna shule nyingine utakuta kuna mwalimu fulani na mwalimu fulani wanajua kila kizuri kitakachotokea wao wanakuwepo, kila semina itakayotokea watakuwepo, kwenye kusimamia mitihani, watakuwepo, lakini kuna baadhi ya walimu masikini wa Mungu wananyanyasika kama wao ajira yao walikuwa wameenda kukopa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kitu naomba Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwa kutumia wafanyakazi wake walioko Wizarani, afuatilie vizuri haki itendeke kwa walimu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wakipata mafunzo vizuri na pia haki zao za msingi, naomba zikumbukwe. Wakati mwingine unaweza ukaenda kwenye shule za sekondari na za msingi, ukasikitika juu ya viti walimu wanavyokalia na meza. Kwa kweli wanakaa kwenye ofisi mbaya, viti vya ajabu, vimevunjika vunjika, meza ziko ovyo ovyo. Wakati huo tunawapa watoto wetu wawafundishe, unategemea watafanya kazi vizuri kweli! Basi tujitahidi. Kama mama yetu Rais alivyoleta majengo mazuri, na yale ya zamani tuyaboreshe na ofisi zao tuziboreshe. Tujitahidi. Tuweke agent ambaye atakwenda kurekebisha...

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

TAARIFA

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimpe taarifa Mheshimiwa anayechangia kwamba ni kweli, walimu wanatakiwa waboreshewe mazingira, kwa sababu kuna shule nyingine, ofisi za walimu ziko chini ya mti. Yaani mvua ikinyesha, kila kitu kilichoko pale kinapeperuka. Kwa hiyo, waboreshewe mazingira, yaani wawe na ofisi ambazo zina furniture. Unakuta wakati mwingine walimu wengine wanabeba viti kutoka nyumbani wanaenda navyo mashuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuunga mkono mchangiaji kwamba Serikali iwajali walimu, maana yake ndio wanatengeneza wataalam mbalimbali, hivyo iwaboreshee maofisi na ikiwezekana wawekewe na AC kabisa ili wawe na fikra nzuri wanapofanya kazi hizi za ualimu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili taarifa hiyo, ni nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala moja, kuhusu Chuo Kikuu cha Iringa, ambacho zamani kiliitwa Tumaini University. Naomba Serikali yetu kwa kupitia Waziri wetu mpendwa, itupie macho mawili iangalie sana kile chuo, kina matatizo makubwa sana. Chuo hicho system yao ya kulipa ada na administration kwa ujumla iko weak so weak, haiko vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mmojawapo wa wahanga wa Chuo kile cha Tumaini cha zamani, sasa hivi kinaitwa Chuo Kikuu cha Iringa. Kuna watoto ambao walikuwa wanasoma pale walikuwa wamefanya malipo. Wanapofanya malipo, namba wanazopewa za kulipia, wanapewa na Wahasibu na watu wa IT, kumbe wanapewa namba fake za malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazazi wengi tunajua hali zao kiuchumi. Watoto wamefanya malipo yale, kumbe malipo yale kulikuwa na makundi mawili; wengine hawakujua, walijua ndiyo namba halisi za kulipia, zaidi ni wale wa mwanzo mwanzo, lakini kuna wengine walikuwa wamekaa na hao baadhi ya wahasibu, wakaamua ku-fake yale malipo yakalipwa. Ilipofika kipindi cha kufanya mitihani, watoto wengi wakaanza kudaiwa. Wale ambao walikuwa wahawajui, wakasema tumelipa, wakapeleka risiti zao, lakini ikaonekana zile akaunti walizolipia ni fake. Baada ya kufuatilia mpaka wazazi, wakaamua wawaruhusu wafanye mitihani lakini wakaambiwa matokeo yenu yatazuiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli matokeo yalizuiliwa, baadaye uongozi wa chuo ukaanza kufuatilia tatizo ni nini kwa kuwaambia wanafunzi waliopata changamoto hiyo ambao ni zaidi ya 40, (na orodha ninayo Mheshimiwa Waziri nitakupatia), kwamba waandike barua za maelezo za kujieleza. Wanafunzi wale waliandika barua za kujieleza. Kweli kuna wengine walikuwa hawajui kinachoendelea, walioamua ku-tamper ni baadhi ya wafanyakazi ambao sio waaminifu. Kuna wengine baada ya kufungiwa matokeo yao, wakaambiwa tu wewe ume-sup somo fulani na somo fulani unatakiwa uje urudie mtihani, lakini kwenye mtihani unatakiwa ulipie tena ada kwa mara ya pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri, mtu kama mimi, angalau namshukuru Mungu nina uwezo wa kulipia ile ada mara ya pili: Je, yule mkulima au yule mama aliyeko kule ndani na baba aliyeko kule ndani wenye uwezo wa chini, wana uwezo wa kulipia kweli mara ya pili jamani? Hiyo ni haki kweli kwa Watanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, walipofanya vile, watu wengine wakalipia, mmojawapo ni mimi nikalipia mara ya pili. Baada ya kulipia mara ya pili, tena niliwafuatilia sana kutaka wanipe hiyo akaunti hiyo ya uhakika. Nilisumbuana nao kwa muda mrefu sana, mpaka nikaamua kumshirikisha rafiki yangu Mheshimiwa Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini anisaidie. Baada ya kulipia mara ya pili, hawakutaka kufungua matokeo ya Watoto. Ilivyoanza semester nyingine, tukaanza kuwasiliana nao kusumbua, kwamba mlisema tulipie mara ya pili, tumeshalipia, mbona hatuelewi kinachoendelea? Majibu yao ni kwenye simu, “mtoto wako amefaulu aje.” Matokeo yako wapi? Tutajuaje kama amefau? “Aje baada ya kufanya marudio ya mitihani anafaulu tu, aje tutakupa matokeo baadae.” Sasa unajua ukifuatilia muda mrefu kila siku unaona kama utakuwa ni kero unaamua umruhusu mwanafunzi nenda chuo ukasome. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku tunafanya ufuatiliaji pale chuoni kwa Mkuu wa chuo, unapewa namba ya Mhasibu, unapewa namba ya Mwanasheria yaani tuna namba kibao za pale Chuo Kikuu cha Iringa. Tukiwasiliana nao wanapiga dana dana “sasa hivi lipeni hela tu ya hostel msilipe ada lakini mtoto atasoma”. Anasoma vipi? Basi tukaona tuwasikilize wao walichosema. Wazazi wakalipia hostel wanawapa na watoto hela za chakula lakini coursework zao hazirekodiwi wala hawajasajiliwa. Tukawa tunafuatilia kila siku muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwishoni walipoona tunafuatilia sana wakasema “senate haijakaa kutoa majibu japokuwa walishafaulu subirini msiwe na wasiwasi majibu yatatoka”. Ni lini? Baada ya kuona nimemshirikisha Mbunge wa Iringa, wakaanza kushtuka sasa, wakaanza ku-forge barua ku-backdate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina barua hapa na baadae nitaomba nimpatie Waziri wa Elimu. Wakiwa wanaandika barua hii ambayo imeandikwa tarehe 5 Desemba, 2022 wakati nimeulizia mpaka Machi wakawa wanasema bado senate haijakaa, wamejisahau wamenijibu hivyo. Pia, wakasema kwamba kikao kilichokaa tarehe 14 Octoba, 2022 kimeamua Kumfukuza huyo mwanafunzi. Naomba ninukuu hivi “This is to inform you that based on your abscondment from studies, The university Senate sitting on 14th October 2022. Wakati waliniambia hizo tarehe mpaka Machi mwaka huu nawasiliana nao wakasema bado senate haijakaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wakasema kwamba unaweza ku – appeal before 10th January 2023. Wakati huo wanasema unaweza ku – appeal before hiyo ni Machi nimewasiliana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barua ni halali, forgery au ni nini? Ina maana kwenye ofisi nyingine bado mpaka sasa hivi kuna forgery za ajabu namna hii kweli? (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Maimuna.

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu umeisha?

MWENYEKITI: Ndio, kengele imelia mara ya pili.

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nitaonana na Mheshimiwa Waziri wa Elimu kumpatia documents zote.