Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Eng. Dr. Leonard Madaraka Chamuriho

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ENG. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia katika bajeti hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Napenda kukupongeza wewe unavyoongoza Bunge pamoja na Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wenzako kwa kazi nzuri mnayofanya katika kuendesha Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda vile vile kutumia fursa hii kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa maendeleo ya nchi hii. Tumeshuhudia kwamba anaweka utendaji mkubwa sana wa mara moja katika sekta hii ya elimu na hili ni jambo kubwa ambalo sasa tunaanza kuona matokeo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimechungulia bajeti ya elimu, katika miaka mitatu kama ilivyo katika vitabu vyetu, inaongezeka kila mwaka, na hii ni dhahiri kwamba Mheshimiwa Rais ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba elimu inakuwa bora katika nchi hii. Vilevile nampongeza Waziri Profesa Adolf Mkenda pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Omari Kipanga kwa kazi nzuri wanayoifanya, vilevile na wataalam wao, Katibu Mkuu, Profesa Nombo na Manaibu Katibu Wakuu wawili, Makamishna wote nakadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii imesheheni wabobezi na tunaona kweli kazi inakwenda vizuri, tunawapongeza sana. Uwekezaji huu mkubwa ambao umewekwa na Mheshimiwa Rais katika miundombinu ya elimu unahitaji kulindwa na vilevile kupatiwa viwezeshaji. Ulinzi wa miundombinu utawezeshwa katika matengenezo ya mara kwa mara kuhakikisha kwamba miundombinu hiyo inadumu, lakini katika huduma zake viwezeshi kuhakikisha kwamba walimu na vifaa vinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita zaidi katika elimu ya juu ambayo katika hayo mawili nitaangalia utafiti pamoja na utayarishaji wa walimu. Walimu wa Elimu ya Juu hawana chuo maalum cha kuwafundisha kama ambavyo tunafahamu vyuo vingine vya walimu hapa kwamba kuna chuo kinachofundisha walimu, lakini kwa elimu ya juu ni vyuo vyenyewe ndiyo hutengeneza walimu wake kulingana na hadhi ya chuo. Kwa hiyo, chuo kinaandaa walimu wake na ubora wake unategemea na jinsi ambavyo itapanga yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, nimeangalia ukurasa wa 34, kwenye utakelezaji wa bajeti iliyopita, nikaona kwamba ndiyo, ameshughulikia mambo ya udahili vizuri, ameshughulikia vilevile na elimu ya wadahiliwa, lakini nilivyoangalia jinsi anavyoshughulikia walimu wa walimu, nikaona hapo kuna ombwe. Nilipoangalia vilevile katika ukurasa wa 76, nikaona mapendekezo ya bajeti hii anayoiomba, nikaona vilevile kwamba ameweka utafiti, ameupa kipaumbele. Kwa hilo nampongeza sana, kwani hilo ndilo ambalo linawezesha ufundishaji wa hao walimu wa walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba bajeti hii haijaweka wazi jinsi wataalam hao, walimu wa walimu wanavyotengenezwa, kwa sababu kama nilivyosema mwanzoni, hakuna vyuo vya kuwaandaa walimu wa walimu. Hivyo, vyuo vinakuwa huru kutengeneza hayo matokeo ya walimu wanaowatengeneza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi kwa sababu walimu hao wanakuwa wana shahada, vilevile ni zao la vyuo vikuu; na kuondoa huu utaratibu wa mwalimu kusoma hapo hapo na kufundisha hapo hapo, ambapo kitaalam wanaita inbreeding, vyuo vingi huhitaji kufundisha walimu katika vyuo vingine, na hapa ndipo changamoto inapoanza, kwa sababu inahitaji aidha watengewe fedha au wapate ufadhili. Sasa hapa kwenye ufadhili, ndipo changamoto inapokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna methali ile inayosema kwamba “anayemlipa mpiga zumari ndiye anayechagua wimbo.” Sasa katika hili, wafadhili wengi huchagua kufadhili fani ambazo wanazipendelea wao, siyo fani ambazo chuo kinazihitaji. Kwa hiyo, hapo ndipo changamoto inapoanzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta kwamba fani ambazo hazina mvuto kwa wafadhili zinaathirika katika vyuo vyetu. Unakuta vyuo vinapata wafadhili, lakini walimu wanaokwenda kufundishwa wanalundikana katika fani ambazo ni fani pendwa za hao wafadhili. Kwa hiyo, unakuta kwamba kweli ukihesabu idadi ya Shahada za Uzamivu ni nyingi lakini mchanganuo wa fani katika hiyo fani inakuwa kidogo kuna changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatokana na vitu viwili. Moja, kuna fani nyingine unaweza kuziona kama ni fani ngumu, ambazo hazina mvuto kwanza kwa wanafunzi wenyewe. Pili, ni fani ambazo ni ghali kuzifundisha. Kuna fani nyingine ambazo kumfundisha mwalimu mmoja au mhitimu mmoja, unaweza ukafundisha wengine watatu. Kwa hiyo, hiyo haivutii wafadhili katika kuwekeza huko. Matokeo yake inakuwa ni nini sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta kwamba katika idara mbalimbali fani ambazo hazina mvuto zinapungua miaka hadi miaka, lakini matokeo tunapata. Wahitimu wanazidi kutoka lakini wamehitimishwa na nani? Wamehitimishwa na walimu ambao, fani zile ambazo hazipo, vilevile zinakuwa vichwani mwao hazipo, na matokeo yake unakuta baadhi ya kozi nyingine zinaahirishwa, kwa sababu wataalam hawa hawapo. Vilevile wanafunzi wa wauzamivu na wa uzamili wanaathirika kwa sababu wanakosa hiyo huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kushauri Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwamba, moja, vyuo vya elimu ya juu vianishe hizi kozi au utaalam ambao hauna mvuto kwa wafadhili. Baada ya kupata orodha hiyo ya fani ambazo hazina mvuto kwa wafadhili, basi Serikali itenge fedha kwa ajili ya fani hizo, kwani ni muhimu kwa Taifa lakini hazina wa kuzifadhili. Kwa hiyo, hiyo itatuwezesha kuhakikisha kwamba mazao ya chuo yanapotoka, pamoja na hiyo degree kubwa, lakini vilevile fani ambayo iko kichwani kwao imekamilika kama ambavyo tunaitarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa muda mfupi, Serikali iruhusu vyuo viendelee na utaratibu wao wa kutengeneza walimu wao wenyewe bila kuviingilia kwa sababu hilo ndiLo litakaofanya waweze kuainisha hizo fani na kuzitafuta na kuzitengeneza jinsi wanavyoweza. Hii ni pamoja na kuruhusu watoe mikataba kwa watu ambao wanadhani wanaweza kuwa na fani hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, japokuwa utafiti umetajwa mle ndani, vilevile tuondoe hii dhana kwamba fedha za utafiti katika vyuo ni fedha za kuliwa na hawa walimu. Ni fedha muhimu sana ambazo ndiyo chanzo cha kutengeneza utafiti na utafiti huo ndiyo unaofanya kutoa hao walimu bora; walimu wa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona muda wangu unakwisha. Natoa shukurani kwako na kwa hili, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)