Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi pia kuchangia bajeti ya Wizara ya Elimu. Naomba niungane na Wabunge waliotangulia kuchangia kuishukuru Serikali, hasa katika sekta ya elimu. Kuna maboresho makubwa ambayo yamefanyika katika sekta ya elimu na ninaomba nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mikumi kuna mambo mengi katika sekta ya elimu, ujenzi wa shule mpya za sekondari, ujenzi wa shule mpya za msingi, kupunguza umbali wa watoto kutoka shuleni mpaka nyumbani au nyumbani kwenda shuleni na kuongeza kiwango cha ufaulu ni maeneo ambayo hayawezi kupita bila kutoa kauli ya pongezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, naomba nitoe pongezi kwa Serikali kuona umuhimu wa kuboresha mitaala yetu ni suala ambalo limekuja katika muda muafaka. Ni matumaini yetu kwamba maboresho haya yamekuja kwa sababu ya mapungufu ambayo tumekuwa tukiyashuhudia huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba elimu yetu kimsingi ilikuwa na changamoto nyingi, nyingine zimefanyiwa kazi na nyingine tunaendelea kuzifanyia kazi, lakini bado tunaweza tukakiri kwamba ilishindwa kukidhi matarajio ya wengi kwa sababu ilikuwa imejikita kumjenga kijana wetu kitaaluma zaidi kuliko kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida hii imesababisha vijana wetu wengi kushindwa kukabiliana na mazingira yao, kushindwa kupambana na mazingira yao, kukosa ajira na kukosa ubunifu wa kuwa sehemu ya majibu ya changamoto ambazo zinawakabili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumaini yangu kwamba mtaala mpya wa Serikali unaenda kujibu changamoto ambazo tumezipitia. Pamoja na hayo, unakwenda kuongeza kasi na umuhimu wa kumtengeneza kijana wa Kitanzania kimaadili na kuwa na hamu ya kutimiza wajibu wake kwa Taifa lake pamoja na ari ya kujituma kupitia mitaala yetu ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu kwamba mtaala huu mpya unakwenda kuongeza kasi ya Watanzania kupambana kupata ujuzi, maarifa na weledi, mtaala huu unakwenda kujibu changamoto ya mahitaji ya soko la ajira ndani ya Tanzania na soko la kazi katika ulimwengu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba mtaala huu mpya unakwenda kuupunguza umri wa kuanza shule toka miaka saba mpaka sita, lakini tuna mifano huko duniani, kwa mfano nchi kama Finland ambayo imeongoza katika ubora wa elimu, hasa ya msingi na sekondari, mataifa yote ambayo yameendelea yanakwenda kujifunza Finland, kwa sababu Finland ndiyo nchi pekee katika nchi ambazo zimeendelea mtoto anaingia darasa la kwanza akiwa na miaka saba wakati wengine anakwenda akiwa na miaka mitano mpaka sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni kwa nini sisi badala ya kuona kwamba hawa wenzetu wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kujenga ari ya mtoto kupenda masomo na kumudu masomo yake akiingia darasa la kwanza akiwa na miaka saba. Kwa nini sisi tumeenda kushusha miaka sita, nini ambacho tunakitarajia kutoka kwa huyu mtoto ambaye tunampeleka shule akiwa na miaka sita?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, tunafahamu kuna maboresho mengi huko nyuma yamepita. Mengine yamefanikiwa kwa kiasi, mengine yalishindwa. Ukiangalia kwa nini yalishindwa, kwa sababu maboresho mengi yalijikita kwenye kubalisha elimu, mitaala na masomo lakini hayakuweka mkazo kwenye kumuandaa Mwalimu ambaye anakwenda kumudu skills za kufundisha watoto ambao tunataka waende kujifunza hayo masomo. Nina wasiwasi hata kwenye huu mtaala mpya hakuna msisitizo wa maandalizi ya Mwalimu ambaye anaenda kuwafundisha watoto wetu katika mtaala mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatutawekeza kwa Walimu siyo rahisi kupata matarajio ambayo tunayatarajia. Vyuo vyetu vya ualimu tumeviandaa vipi kukabiliana na mabadiliko ya sera na mtaala, walimu wetu tumewaandaa vipi kukabiliana na haya yote ambayo tunayaita mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini maandalizi mazuri kwa walimu wetu yatatuletea matokeo mazuri, tusipowaandaa walimu wetu kulingana na mahitaji yetu hata kama tutafanya mabadiliko makubwa ya mtaala wetu, siyo rahisi kupata kile ambacho tunakitarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia uhaba wa walimu, lakini huko miaka ya sabini na themanini, masomo mengi yalikuwa yanafundishwa kupitia redio, sasa hivi tuna televisheni, tuna vishkwambi, tuna YouTube, WhatsApp, kuna initiative gani ambayo inafanyika kuhakikisha kwamba maeneo ambayo yanakosa walimu watoto wanatumia technology kupata elimu yote kwa mujibu wa curriculum ambayo tumejiwekea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya teknolojia hatuwezi kuyaepuka na yanaweza yakatusaidia siyo tu kufikia wanafunzi ambao wamekosa walimu, lakini yanaweza kutusaidia kupambana na tatizo la uhaba wa walimu hasa katika maeneo ya pembezoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamesisitizia sana lugha, nami naomba nisisitizie tena suala la lugha, lakini lugha ambazo nasisitiza ni muhimu siyo tu Kiingereza, sasa hivi dunia inakiangalia Kichina, Kifaransa na Kiarabu. Hizi lugha zote ni nzuri kwa mawasiliano kwa ajili ya kufikia watu ambao tunaweza kufanya nao kazi, tukafanya nao biashara, tukaingiliana nao kwa maendeleo ya uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wakati tunatoa kipaumbele kwenye lugha hizi nyingine za mawasiliano ni vizuri tukaangalia kwa mapana yake wapi tunataka kwenda na tunawafikiaje watu katika dunia kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia mustakabali wa Taifa letu. Juzi hapa tulikuwa na Sensa Kitaifa, zoezi la sensa lilikuwa kubwa sana. Ninapenda kujua wakati Mheshimiwa Waziri anahitimisha ni Watanzania wangapi ambao hawajui kusoma na kuandika. Tuna mpango gani wa kuwafikia Watanzania hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokujua kusoma na kuandika ni mzigo mkubwa sana katika kizazi hiki na katika jamii tunayoishi. Hasa ukizingatia kwamba takwimu zinaonesha kuna watoto zaidi ya 55,000 ni drop outs kutoka shule, lakini tunajua kwamba kuna watoto wengi zaidi ambao wako nje ya mfumo wa shule. Hawa hatuna uhakika kama watajua kusoma na kuandika kesho, na ni jeshi kubwa sana. Tunajiandaaje na kuangalia jinsi gani watoto hawa ambao hawajui kusoma na kuandika wanaingizwa katika mifumo na hii mitaala mipya inakwenda kutumika kama tool ya kufikia hawa watoto ili tusiwaache nyuma wakati Taifa linaenda mbele?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja; ahsante sana. (Makofi)