Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia eneo hili nyeti sana kwa uchumi wa nchi yetu. Wahengwa wana msemo wao wanasema, kila shida huzaa fursa na kila fursa huzaa shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie, kila shida yoyote inayompata mtu, inayotokea hapa duniani huzaa fursa na kila fursa unayoipata inakuzalia shida. Sasa nchi yetu imepata fursa ya kuwa na binadamu, kuwa na watu wengi, hii ni fursa, kuna nchi hazina watu. Sasa fursa hii hivi tunavyozungumza inakwenda kutuzalia shida, tunaanza kuhangaika sasa tutafanyaje vijana wetu? Watapataje ajira? Watafanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio tunakuja na mtaala mpya. Sasa huu mtaala unaouona huu mtaala ulioanzishwa sasa hivi unaokuja na ndugu yetu Mheshimiwa Profesa Mkenda, namheshimu sana, mtaala huu lazima Serikali ichukue tahadhari kubwa sana. Maneno haya nayasema, mimi ni mdau wa elimu, leo zaidi ya miaka 32. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili nataka niseme maneno mengine makubwa sana ya wanafalsafa wa elimu. Wanasema, kuna watu sita bora sana duniani, watu wote ni bora, lakini kundi la hawa watu sita ni bora sana duniani. Kundi la kwanza la heshima bora duniani ni wazazi wawili; Kundi la pili la heshima duniani ni viongozi wa dini au viongozi wa kimila; Kundi la tatu la muhimu sana ni Walimu. Mtu anayeitwa Mwalimu ni kundi la tatu la watu wenye heshima duniani; Kundi la nne ni la watu wanaotoa haki, yaani Mahakimu na watu wengine wote wanaosimamia haki; Kundi la tano ni la Matabibu, Waganga, Madaktari; na Kundi la sita la watu muhimu ni watawala, kwa upande mwingine tunasema wanasiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya makundi sita wakikosa uadilifu dunia si mahali salama pa kuishi. Wazazi wasiposimamia nafasi yao kuwa wazazi, basi ni hatari kubwa sana, lakini viongozi wa dini wasipochukua nafasi yao ni hatari kubwa sana. Walimu wasipochukua nafasi yao ni hatari kubwa kote mpaka juu. Sasa leo tunakwenda kubadilisha mtaala na huu mtaala ni sehemu kubwa sana, nafikiri katika mitaala iliyobadilishwa huu unaweza ukawa ni mtaala wa saba au sita katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaala wa kwanza ni wa Mjerumani ambao ulikuja kubadilishwa na Mwingereza mwaka 1914. Baada ya hapo tulikaa na mtaala wa Mwingereza mpaka mwaka 1967, zaidi ya miaka 53 na baada ya hapo mtaala ukabadilishwa na Baba wa Taifa mwaka 1967 mpaka mwaka 1977, huu ni mtaala wa tatu. Mtaala wa nne umebadilishwa mwaka 1977 mpaka mwaka 1984 akiwepo baba wa Taifa. Sasa tunakwenda katika mtaala wa tano ambao aliubadilisha Mzee Mwinyi mwaka 1997, baada ya hapo Rais wetu Benjamin Mkapa, marehemu, alibadilisha mtaala ambao umekuja kubadilishwa mwaka 2008. Sasa tumekuja 2014 ukabadilika mtaala, huu tunakwenda mtaala wa saba, tuwe na tahadhari kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nimeyasema haya? Ni kwamba, wanazuoni waone, wapime, kwamba, tokea mwaka 1905 mpaka 1914, waone Mjerumani alifundishaje, Mwingereza naye hivyohivyo mpaka 67, baada ya hapo sisi ule mtaala tumekuja kuupokea. Tuwaangalie Waingereza ule mtaala ambao walituletea sisi tukaubadilisha mwaka 1967, je, wameshabadilisha mtaala mara ngapi? Hii ndio tahadhari yangu kubwa. Tusije tukawa abunuwasi, tukawa tuko juu ya mti, tunakata chini tuanguke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani nasema hivyo? Haya masomo ambayo ni ya amali yanayokuja kufundishwa sasa hivi ni kwamba, lazima tuwe tuna tahadhari, tusome masomo yetu. Tuangalie mtaala uliopita na mtaala huu, tusome kuanzia saa moja na nusu mpaka saa nane. Baada ya saa nane tuwe na masomo mengine matatu au mawili kwa masaa haya mawili au matatu, elimu yetu sasa hii ya amali ifundishwe. Vinginevyo tutakataa haya masomo mengine tuje tufute haya masomo, tutakuja kuingia kwenye hatari kubwa sana. Sasa lazima tuchukue tahadhari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya nayasema mimi kama Tabasam lakini natoa ushauri kwa wasomi wetu, hii Mheshimiwa Profesa Mkenda, nakuomba tu, pamoja na kwamba nimeuptia mtaala wako vizuri kabisa kwa heshima, kwa sababu ni lazima tuandae vyuo vya elimu, kwamba tutakuwa tuna vyuo vya elimu kumi vitakavyokwenda kuwafundisha walimu elimu ya amali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuwa na shule ambazo watoto hawa wakitoka wanakwenda kufundishwa walimu kule kwenye zile shule za sekondari wapo pia vyuo vyetu vya ufundi katika kuendelea wapo na utoaji wetu wa certificate, tunakwenda na mitaala hii lakini mtu akimaliza form four basi apewe certificate hata kama hakufaulu lakini ni mjuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi nakupa sasa hivi elimu iliyoko mtaani, kuna mafundi baiskeli, unaileta baiskeli kwenye boksi anakuja anaiunda yule mtu, anaifunga anaiunganisha, hana certificate, na huyu mtu hatambuliki kwa sababu hana cheti. Kuna mafundi pikipiki hivyohivyo, wanakwenda kutengeneza pikipiki, anaiunda inakuwepo lakini hana cheti. Sasa je, Serikali inakwendaje kuwatambua hao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, unamwona Profesa kabisa kama Mheshimiwa Prof. Mkenda anapeleka gari lake mtaani na anayekwenda kulifanyia kazi hana cheti, Profesa Mkenda yuko pale anasubiri, anamwona fundi anamwaga oil, anabadilisha tairi, anafanya nini. Je, hawa umewaweka katika upande gani unawapa vyeti lini? Kuna mafundi wanakujengea nyumba wewe mwenyewe, Mheshimiwa Profesa Mkenda na ukenda pale mainjinia wako wanasema hii nyumba iko sawa. Je, huyu naye cheti chake atapata lini? Lazima tuangalie haya makundi yote tumejipangaje kwenda kuwapa vyeti hawa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wafugaji. Hawa Maprofesa na Madaktari wote mnaowaona wanakwenda kufanya research kwa wafugaji, mtu amefuga ng’ombe ana miaka 30, mtu amelima mtama au mpunga ana miaka 30, anayekuja kufanya research pale anakuja kumuuliza Mzee hii mbegu yako inatoa magunia mangapi, gunia 30, ukifanya hivi inakuaje, ukiacha maji yanakuwa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo mtu akitoka pale anakwenda SUA kupata degree, lakini amekwenda kumuuliza mkulima wa darasa la pili, ndiyo anajua kabisa kwamba ukipanda mbegu ya karanga ambayo inazaa tatu, itatoa watoto watatu, ukipanda karanga inatoa mbegu mbili utatoa karanga mbili. Haya anayajua Bibi yangu hakwenda hata shule, hana degree, sijui unaniulewa vizuri, lakini anayekwenda kufanya research mnakuja kumpa degree. Sasa lazima muangalie hivi vitu. Tunakwenda katika mitaala tusije tukaacha ya kwetu tukaenda kubeba kila kitu kipya. Sisi tuko vizuri unatuona hapa akina Tabasam, tumesoma mtaala huu unaouona, ulibadilishwa mwaka 1967 tukaenda nao mpaka mwaka 1984 ukaja kubadilishwa, siwezi kulinganishwa na mtoto sasa hivi unayempeleka akapata degree SUA. Atanishinda kuongea Kiingereza tu lakini mambo mengine yote tukiyatunga Kiswahili hanipati ng’oo. Haya nakueleza hapa hapa tu, leteni paper tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lugha inayotakiwa kufundishwa ni ile ya kumfanya mtu aelewe, nieleweni vizuri. Kwa sababu utamtoa mtoto huku anasoma Kiswahili halafu ukija ukambadilisha baadae huyu mtoto anakwenda kufeli kwa sababu tu ya kushindwa kujua Lugha ya Kiingereza. Lugha ya Kiingereza itolewe maksi zake na lugha nyingine itolewe maksi zake vilevile kwa sababu yule mtoto ukimfundisha kwa Kiswahili anafaulu ule mtihani, halafu somo la Kiingereza aje alisome ni la muhimu sana kusomeshwa na lenyewe lipate cheti chake, lakini habari ya kutuambia kuitengeneza meza na kupiga msumari mtu aje afanye mtihani wa kiingereza, kutengeneza gari halafu mnasema kwamba amefeli, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabsam, muda wako umeisha naomba umalizie mchango wako.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongeze kidogo tu nimalizie.

MWENYEKITI: Haya, sekunde 30 malizia.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ni suala la usajili wa shule. Suala hili limekwenda kwa Mheshimiwa Prof. Mkenda anajua, mmekuwa mnazifungia hata sekondari zenu za Serikali. Mara hazina kichomea taka, ulipeleka bajeti hiyo? Unazuia kichomea taka unashindwa kusajili shule, watoto wanakaa 800 darasani. Shule ya Msingi ina watoto mpaka 300. Kuna shule nyingine iko pembeni wamejenga wananchi unaiita shule shikizi unashindwa kuipa usajili. Haya maneno inakuaje upande wa ukaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani ninyi wenyewe shule ni za kwenu bado mnaziwekea masharti makubwa wakati hamjapeleka bajeti? Hii nchi tunakwenda wapi? Tumsaidie Mama Samia Suluhu Hassan, kule mmeweka Polisi kwenye sehemu ya elimu hata kwenye shule zenu, tukabeni kwenye shule binafsi hivyo lakini siyo shule za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)