Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naanza kuchangia, binafsi naona Serikali imefanya kazi kubwa kwenye kuhuisha sera hii, ile ya mwaka 2014 kuileta hili toleo jipya la mwaka 2023, labda kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati, lakini naona wamezingatia kwa kiasi kikubwa maoni na matamanio ya Watanzania kwenye elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa hilo niipongeze Serikali, lakini bado ushauri wangu unabakia pale pale tusiishie kwenye kuandika. Kwa kweli ukisoma, ukatulia na ukafuatilia kama kweli yatakwenda kwenye utekelezaji, kama kweli uwekezaji utakuwa namna ile ambayo tunaambiwa, mimi naamini tutakwenda kwenye step nyingine.

Kwa hiyo, nitofautiane kidogo na mwenzangu aliyetangulia kwa sababu pale kuna financial management, kuna mambo ya music, watu wanaopenda music, kuna mambo chungu mzima ambayo tulikuwa tunasema kwamba watu wasifanye kwa mazoea. Sasa hivi yamewekwa kwenye sera na kwenye mitaala, na mimi kwa sababu ni Mjumbe wa Kamati ya Elimu tumepata nafasi mbalimbali za kupitia kushauri na kuelezwa na kuelekezwa ni kitu gani kinakwenda kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo suala la msingi Serikali kweli ikafanyie kazi yale ambayo wameyaweka kwenye maandishi ili kile tulichokikusudia kama nchi tukifikie. Sasa sambamba na hilo, ukisoma ile sera inakwenda zaidi kwenye mambo ya ujuzi, hapo tutapata vyuo vya kati. Lakini sasa wasiwasi wetu ama wasiwasi wangu unakuja hapo kwenye vyuo vya kati ndio inaonekana kuna ugumu wa wanafunzi kusoma kwa sababu ya kukosa mikopo. Serikali sasa itueleze imejipanga vipi ili kuhakikisha wale ambao hawatakwenda kwenye mkondo wa jumla wanakwenda huku kwenye hivi vyuo vya kati kwa ajili ya mafunzo ya amali, wamejipanga vipi kuwawezesha kufikia ndoto zao? Ndio hiyo ninayosema ya utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vyuo vya VETA vinajengwa nchi nzima. Nayo Serikali itueleze imejipanga vipi kuhakikisha wakufunzi wanakuwepo? Sio wakufunzi kwa maana tu wamekaa pale, mkufunzi mwenye sifa stahiki ya kufundisha kile ambacho tumekikusudia mtoto wetu akipate. Serikali ije ieleze kwa undani. Hayo ndiyo mambo ambayo tunataka tuyaone yasiishie kwenye maandishi yaende kwenye utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nifahamu, lile suala la kufanya Chuo cha Ualimu Mtwara kawaida kuwa tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam limefikia wapi? Kwa sababu miaka inapita tunaambiwa, natamani Mheshimiwa Waziri atapokuja kuhitimisha atuambie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotamani kufahamu; kwenye uandaaji wa mfumo wa usajili wa shule kwa njia ya kielektroniki nao umefikia wapi utekelezaji wake? Pia na hilo natamani nipate kuelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka nisisitize, mimi kama mwalimu ukiniambia elimu ya awali Mheshimiwa Waziri unasitasita kusema ya lazima au watu wasome tu kwa kujisikia. Mimi natamani nisikie ya lazima, kwa sababu pale kwenye elimu ya awali watoto wale wadogo ndiyo tunategemea pale wafundishwe namna ya ushirikiano. Unajua tatizo linalokuja tunaona elimu zetu za awali labda kwa sababu zinafundishwa na walimu ambao wengi wao hawajapitia mafunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tunaona wanafundisha mambo makubwa tofauti na umri wa watoto. Kwenye elimu ya awali watoto wacheze wakati wanajifunza, watoto wafundishwe namna ya kushirikiana kwa sababu nyumbani mwingine anatoka peke yake hajui kushirikiana na mwenzie, lakini pia wafundishwe zile language skills mbalimbali, ndivyo tunavyotegemea viwepo kwenye elimu ya awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri ukisitasita ilhali tunajua kabisa hapo nyuma kulikuwa na movement kwamba kila shule ya msingi kuwe na darasa la awali? Sasa leo kimeingia kizungumkuti gani cha kusema kwamba hii elimu iwe ya lazima? Hapo ndipo ambapo mimi hapo bado nina question mark ambayo natamani ukija kuhitimisha utueleze. Ulieleza pale Pius Msekwa, binafsi mimi sikukuelewa, yaani mpaka leo sijakuelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niseme, mchangiaji aliyepita yeye ameongea kwamba shule za private zinaajiri walimu, zina wanafunzi na mimi ninakubaliana naye. Mimi nakupeni data; leo hivi tunavyoongea kuna walimu 25,926 wako katika shule za msingi za private; tuna walimu 21,343 wako katika shule za private za sekondari ambapo hizi shule zisingekuwepo hawa walimu wote wangekuwa wako mtaani wanasotea ajira za Serikali. Lakini leo tunapoongea kuna wanafunzi wa shule za msingi 591,005; pia kuna wanafunzi wa shule za sekondari 291,882 wako private school. Sasa tujiulize, maana hizi shule leo zisingekuwepo hawa wote wangekuwa wamerundikana wapi kwenye shule zetu za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa ninachotaka kukisema, mimi sina shule wala sina interest ya kuanzisha shule, ninachotaka kusema jukumu la kuendeleza au la kutoa elimu kwa wananchi wake ni la Serikali, hii inajulikana kwa asilimia 100. Sasa hawa wawekezaji wanapojitokeza Mheshimiwa Waziri mkae chini, mtatue changamoto kwa amani kwa sababu hawa watoto wanaosoma kule ni watoto wa Kitanzania. Wakielimika wameelimika kwa ajili ya Taifa la Tanzania. Kwa hiyo, yale makandokando mnayoyaona yanaweza upande mmoja yanaleta shida na upande mwingine yanaleta shida, mjitahidi kuyatatua ili tusonge kwa sabaabu hawa ni Watanzania, yaani mtoto akisoma private habadiliki kuwa si Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kuhusu uhaba wa walimu. Mheshimiwa Waziri kwenye Kamati yetu alituletea; unajua hapa zinasomwa data nyingi, inategemea mtu ameitoa wapi data yake. Mimi data ninayoongea ni data tuliyoletewa na Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwenye Kamati yetu ya Elimu alisema hivi, uhaba wa walimu. Elimu ya awali, mahitaji ni 61,487; waliopo ni 8,619; uhaba ni 52,868. Elimu ya msingi, mahitaji ni 300,702; waliopo ni 167,245 na upungufu 133,457. Elimu ya sekondari, mahitaji ni 174,632 waliopo ni 84,700, upungufu ni 89,932. Kwa hiyo, mimi ninaachana na hiyo habari ya awali nikachukua tu msingi na sekondari, si kwa maana awali haina mantiki, ina mantiki sana, nimetoka kusema hapa. Upungufu uko 223,389 ukitoa hiyo ajira mpya ambayo imekuja walimu 13,130 upungufu bado unabakia 210,259. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua wahisani wanaweza kutusaidia kujenga miundombinu lakini hawawezi kutusaidia kuajiri walimu. Kama nchi na kama Serikali, hivi vitu inabidi viende sambamba. Kwa maana ipi? Wakati tunasema elimu bila ada tukumbuke wanafunzi wengi watoto wengi watandikishwa. Tena sasa hivi sera ile inatupeleka mpaka form four. Tuone ni kwa namna gani Serikali inajipanga kuajiri walimu wa kutosha, kujenga miundombinu ya kutosha, vitabu huko shuleni ni majanga. Fedha ya ruzuku mpaka leo mtoto wa shule ya msingi anatolewa shilingi 10,000 kwa mwaka, tena 10,000 hiyo 4,000 inabaki Wizarani huko wanasema ya kununua vitabu, na hapo hapo hiyo 6,000 anapoenda shule ukisoma ripoti ya CAG anasema mwaka 2021/2022 ilikuwa iende bilioni 33.7 lakini katika hiyo hela haikwenda yote, bilioni tano haikwenda, mnategemea walimu wetu wafanye kazi kwa namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Serikali iende kwenye utekelezaji wa sera na mitaala mipya ambayo inaanzishwa. (Makofi)