Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipatia fursa ya kuchangia Wizara ya Elimu. Niwapongeze Mheshimiwa Waziri Mkenda, Naibu wake Ndugu yangu Kipanga, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Rais wetu kwa kazi kubwa anayoifanya hasa kwenye sekta ya elimu kwa kuwapatia pesa kubwa na nyingi inadhihirisha nia aliyonayo katika kuboresha elimu yetu. Naomba kutofautiana kidogo na wachangiaji waliyonitangulia, naongelea suala la mtaala ambao uko mbioni kutengenezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina wasiwasi tunapotengeneza mtaala kwenye ukachukua maandiko matakatifu yanasema “mvinyo mpya kwenye kiliba cha zamani haifai”. Tunayo Sheria Na. 25 ya Elimu ya Mwaka 1978 ilifanyiwa marejeo na Sheria Na. 10 ya Mwaka 1995. Sheria imepitwa na wakati, kama tunataka kuboresha elimu yetu lazima tuanzie huko kwenye sheria ndiyo chimbuko kubwa la kuboresha elimu yetu hata tufanye nini? Tubadilishe mitaala, tufanye nini? Hatutaweza kuboresha elimu. Turudi kwenye chanzo kule, tuboreshe elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Ukiangalia Wizara ya Elimu leo inaendeshwa kwa nyaraka. Zipo nyaraka nyingi sana na hizi nyaraka zinazotolewa na Wizara ya Elimu kila siku ni ishara kwamba kwenye sheria kuna tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye sheria, zipo nyaraka nyingi sana hapa ukisoma unahitaji unaweza ukafanya research ya PHD. Kwenye maeneo kumi na tatu mahususi ya elimu zipo nyaraka rukuki kwa mfano ukiangalia nidhamu na malezi zipo nyaraka tisa, ukiangalia kamati ya bodi za shule nyaraka sita, udahili wa wanafunzi nyaraka kumi na saba, ukienda mihula na siku za masomo nyaraka tatu, michezo nyaraka tano, elimu ya ualimu nyaraka tisa, kufukuza kurekebisha na kuamisha wanafunzi nyaraka kumi na moja. Uendeshaji wa mitihani nyaraka kumi na sita, ukienda masharti ya usajili wa shule nyaraka sita, kukuza uzalendo hapo kuna nyaraka moja sijui kwa nini? Nyaraka ya ajira za nje moja, ada na michango nyaraka kumi na nne, taaluma ufaulu na ufundishaji wa rula nyaraka ishirini na nane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti sasa ukiangalia hizo nyaraka nane anazitoa kafanya utafiti wapi? Unatoa nyaraka kwa sababu wanataka ku–supplement kuna madhaifu makubwa katika Sheria ya Elimu. Sasa nadhani tunapoongelea mitaala tuangalie sera yetu, tuangalie sheria yetu tuweze kuioanisha, tuweze kupata kitu ambacho ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuishauri Wizara ya Elimu, zimetoka nyaraka nyingi sana na juzi juzi hapa ilitoka nyaraka ya watoto wa bweni, nursery school wasiende boarding, waingie bweni wakiwa darasa la tano. Tunaenda wapi? Tunakwenda mbele, tunarudi nyuma? Hebu tuangalie uchumi wetu, kadiri uchumi unavyokua watu wanavyokuwa na pesa ndivyo watu wanavyo wajibika zaidi kwenye sekta za uzalishaji. Sasa kupanga ni kuchagua, Serikali kazi yake ni kudhibiti ni kufanya kazi ya regulatory regulations siyo kupangia watu waishije? Wasomesheje watoto wao? Hiyo siyo kazi ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifikiri kadri tunavyotarajia kwenda kwenye uchumi wa kati, ndivyo watu wanavyokwenda kuwajibika zaidi kwenye sekta binafsi na sekta nyinginezo. Sasa mtu anaamua mtoto amwachie nani? Amwachie maid hawapatikaniki siku hizi. Kwa hiyo, chaguo halisi ambalo mzazi analiona kwa wakati huo ni kumpeleka shuleni bweni ambako ana uhakika na malezi ya mtoto wake. Niwaombe Wizara ya Elimu tulitafakari hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tena kuishauri Wizara ya Elimu tuiangalie private sector. Private sector ina shule nyingi, inaajiri watu wengi na imewekeza mitaji kwenye elimu hii lakini kwa macho ambayo unaiangalia private sector ni kama mshindani wa Wizara ya Elimu si kweli. Private sector ina supplement pale ambako Serikali haiwezi kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia private sector imewekeza kiasi gani kwenye Wizara hii? Tukiangalia private sector inaajiri walimu wangapi katika Taifa hili? Inalipa mishahara walimu wangapi kwenye sekta hii ambao wengekuwa redundant kama wasingekuwepo? Nashauri, Mheshimiwa Waziri private sector tuichukulie kama ndugu yetu siyo mshindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia mahusiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya TAMISEMI, mahusiano yale hayana tija. Ukiangalia kule TAMISEMI tuna wadhibiti ubora mikoani, tuna wadhibiti ubora wilayani, hao wote wanawajibika kwa Waziri wa TAMISEMI, lakini wanafanya kazi ya Waziri wa Elimu. Kuna mpingano, kuna mkorogano hapo katika mahusiano kati ya Wizara ya Elimu na TAMISEMI. Lazima tuliangalie; na ndiyo maana mimi nashauri badala ya kwenda kwenye mitaala tuangalie kwanza sera na sheria zinasemaje kama tunataka kuleta utulivu kwenye sekta ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda huko hata kwenye shule binafsi, unakwenda TAMISEMI wanasema ya kwao, Wizara ya Elimu wanasema ya kwao. Tumefanya hivyo kwenye sekta ya maji, tumefanya hivyo nadhani na sekta ya TARURA. Nashauri watendaji wote ambao ni wadhibiti ubora ambao wako TAMISEMI warudishwe Wizara ya Elimu. Tuwe na Wizara moja ambayo inafanya kazi ya kusimamia elimu na TAMISEMI wabaki na suala la kusimamia miundombinu tu, masuala ya kisera yote yarudi Wizara ya Elimu, vinginevyo tutakuwa tunacheza mdundiko hapa. (Makofi)

Mheshimwia Mwenyekiti, yanatoka maagizo, yanatokea TAMISEMI; Wizara ya Elimu hawayakubali. Mengine ya Wizara ya Elimu, TAMISEMI hawayakubali; tunakwenda wapi? Nadhani tunapaswa kuoanisha haya mambo. Serikali ni moja, Taifa ni moja na ni Serikali ya Awamu ya Sita ya mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nawaomba mkae chini mkayangalie haya mambo, tuwe na Wizara moja mahsusi inayo–regulate na inayoratibu masuala yote ya elimu kama sera na sheria zinavyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba nirudi kwenye jimbo langu. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana, tunakushukuru sana hasa Mkoa wa Kagera, na salamu zetu tunaomba umfikishie mama yetu Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan; kwa miaka nenda-rudi Mkoa wa Kagera tumepigania kupata chuo kikuu. Tumejaribisha kupitia private sector tulishindwa, vikaja vyuo ambavyo vilianzishwa na mashirika ya dini vinajikongoja. Kama mnavyofahamu, Mkoa wa Kagera ni mkoa wa elimu, upende usipende ndivyo ilivyo, ndiyo historia yetu. Kwa kutupatia chuo kikuu chini ya mradi wa HEET tunakushukuru sana na tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi niende kwenye Wilaya yangu ya Muleba, Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana, juzi hapa tumepewa taarifa wametupelekea takribani milioni 900 kwa ajili ya chuo chetu cha VETA. Kulikuwepo na chuo kidogo hakikuwa na heshima ya Wilaya ya Muleba. Tunakushukuru sana na tunakuomba sasa hicho chuo kijengwe haraka sana. Lakini kama wengine walivyosema, tunapojenga hivi vyuo vya VETA na tunavyotoa elimu yetu, mwaka jana kuna mchangiaji mmoja alichangia hapa, tuangalie tunachofundisha watoto wetu. Walikuwa wanaongelea mambo ya historia, eti tulifundishwa mwanadamu ni evolution, alitokea kwenye nyani na bado tunaendelea kufundisha haya mambo kwa watoto wetu. Hivi kwa nini tusikae chini tukatafakari tukaja na mfumo wetu wa elimu wa kuwafundisha watoto wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nilikuwa naangalia kwenye mtaala ambao wameutoa, Mimi naomba nishauri, ukiangalia mpangilio wa yale masomo mliyoyaweka bado tuna mentality ile ile ya miaka ya 1960. Mimi nilitarajia tuangalie dunia inakwenda wapi, na uchumi unaelekea wapi. Sasa hivi unapoongelea kufundisha watoto unakwenda kuwafundisha historia zilizopitwa na wakati, haina tija kwa watoto wetu na haina tija kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani tungeelekeza nguvu zetu kwenye kufundisha TEHAMA, kufundisha innovation, consumer protection ili watoto wetu wakue wanajua mambo gani ya msingi ya Taifa lao. Taifa letu linasimamia nini? Ukienda nchi za wenzetu unamuuliza mtoto kwa mfano Tanzania inasimamia nini, ukiwauliza watoto wa Kimarekani watakwambia Marekani inasimamia nini miaka 100 ijayo, lakini sisi hapa ukituuliza itategemea tu kama mvua imenyesha, kama kuna maji mito imefurika, tuje na kitu mahususi cha kuwafundisha watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye VETA zetu; hivi hizi taasisi zetu ambazo ziko chini ya elimu sijui SIDO, sijui nini, zinafundisha nini watoto wetu? Hii mitaala kweli inaendana na hali halisi ya maisha yetu Watanzania? Sioni. VETA iko Kagera unawafundisha sijui vitu gani? Badala ya kuwafundisha kutengeneza nyavu, kuwafundisha kuvua samaki, tunafundisha vitu ambavyo tumevi-import kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naunga hoja mkono.