Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa na mimi nafasi nichangie hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu. Kwanza nampongeza Waziri pamoja na timu yake kwa kazi kubwa aliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu toka tumepata uhuru tunapigana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi pamoja na umaskini, lakini unaangalia toka tumepata uhuru sasa tuna miaka 60, ukikaa saa zingine unafikiria hivi tunatumia silaha gani butu namna hii miaka 60 bado tunapigana na ujinga, magonjwa na umaskini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, silaha pekee ya kupambana na hao maadui ni elimu. Sasa tuangalie mfumo wetu wa elimu kweli umetuandaa kupambana na ujinga? Kama tunasema mtoto wa shule ya msingi angalau ajue KKK (K- Tatu), hivi KKK katika ulimwengu wa sasa wa dijitali wa utandawazi ndiyo umemtoa kwenye ujinga? Kwa hiyo, lazima tuangalie hii mifumo yetu inatupeleka wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wameandaliwa kupambana na magonjwa? Jana Waziri wa Afya alikuwa anahitimisha hapo akasema kupambana na magonjwa ni kubadilisha lifestyle. Achana na mafuta, sukari, chumvi na pamoja na mazoezi. Sasa ni Watanzania wangapi wanaelewa ni namna gani kwa kuelimika kwao watapambana na magonjwa ili siku moja Tanzania Malaria iwe historia kama ilivyo ukoma ni historia, kipindupindu ni historia. Tunahitaji silaha ambayo ni elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ndoto ya kwenda kwenye uchumi wa kati. Tunawategemea hawa vijana watupeleke katika uchumi wa kati. Tunajua demografia nchi yetu asilimia 70 ya vijana ni wana umri kati ya mwaka mmoja mpaka miaka 30. Hao ndiyo tunaowategemea, elimu yetu ni kwa kiasi gani imewaandaa hawa kwenda kujiajiri na kwenda kufanya shughuli ili walipeleke Taifa letu katika uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mama yetu amekumbuka akaliona hili akasema sasa tuangalie upya mitaala pamoja na sera ya elimu ambayo sasa itatupeleka kupambana na hali hiyo ili kijana wa Tanzania sasa aweze kujitegemea, aweze kujiajiri na aweze sasa kuiletea nchi yetu uchumi na tuweze kuvuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napongeza mtaala huu unaonekana utakuwa mtaala mzuri tu, kwa sababu unaonyesha sasa kuanzia form one kutakuwa na mikondo miwili. Kuna mkondo mmoja ambao ni elimu ya jumla hii ambayo wanafunzi wanasoma form one mpaka form four, pia kuna huo mkondo mwingine wa elimu ya awali ambayo ni elimu ya ufundi, itamsaidia kijana kujifunza ufundi wa namna yoyote ili atakavyofika form four aweze kujiajiri na aweze kujitegemea, kwa sababu atakuwa amepata ujuzi na elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji maandalizi makubwa. Kwanza wananchi wa Tanzania wenyewe wajiandae kwamba tunavyoenda kwenye mfumo huu ni vitu gani hasa vinatakiwa lakini na vijana tunaowapeleka shuleni wanapaswa kupata elimu. Serikali sasa ndiyo ifikirie tu kwamba tunavyoenda kwenye mfumo huu ambao Mheshimiwa Waziri amesema, ataanza pilot area mwakani, mwaka 2024, ni kwa kiasi gani kwa sababu tunahitaji bajeti ya miundombinu, tunahitaji walimu waliobobea. Isije ikawa tena ni elimu ya nadharia, unamtoa mtoto pale form four, unamtoa mtoto pale form six au hiyo technical school bado ni nadharia akawa hajajifunza kitu. Kwa hiyo, ninawaomba Serikali ifikirie kama tunaanza tentatively mwakani, japokuwa ni pilot area na hili ndiyo tulilokubaliana na ndiyo tunataka sasa tutoke kwenye maadui hawa watatu, basi Serikali itenge pesa za kutosha ili Wizara iweze kujiandaa kwa jambo hili geni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninaloliona la kurudisha elimu yetu nyuma isiwe bora sana ni suala la miundombinu. Tulikuwa tunaona zamani tukishindanisha shule zetu, shule za private, shule za seminari zilikuwa zikiongoza kwa ufaulu lakini ukiangalia siri ni nini ndani? Mwalimu wa seminari ana wanafunzi 45 tu darasani ukilinganisha na shule za Kata wakati huo mwalimu ana wanafunzi hadi 100 anaowafundisha. Je, anao uwezo wa ku-monitor na kufuatilia mtoto huyu anafanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi Taifa limefanya kwa nia njema, kwa mfano suala la elimu bure. Elimu bure imeongeza ufaulu kwa shule ya msingi na kuongeza ufaulu katika shule ya msingi ina maana pia imeongeza udahili wa form one. Imeongeza udahili kwa asilimia 88. Kwa mfano, tukiona mwaka wa 2021, watoto wa form one walikuwa wamedahiliwa 780,376 lakini mwaka jana 2023 wamedahiliwa wanafunzi wa form one 1,073,000. Sasa implication ya hii ina maana kwa sababu wengi wamedahiliwa bado tunahitaji vyumba vya madarasa, bado tunahitaji matundu ya vyoo, bado tunahitaji vitabu, tunahitaji walimu. Sasa Serikali inavyofanya vitu kwa nia njema, tunasema safari moja inaanzisha nyingine, imejipangaje sasa kuendana na hayo matokeo ambayo tuliyatarajia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kazi kubwa sana kuiweka hii katika historia kama tutakubaliana kama upungufu wa madarasa ambao unaenda kwenye 102,000 na hata ripoti ya CAG tumeiona ya mwaka 2021 imeonesha katika Halmashauri 45 imeonesha kuna upungufu wa madawati 158,000, matundu ya vyoo 56,000, nyumba za walimu 35,000, madarasa 27,000 katika Halmashauri hizo 45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tu kwamba ni afadhali kuachana na hii kwa sababu kwanza tukiingia kwenye huu mfumo ambao utakuwa na madarasa ya kawaida ya elimu na itakuwa na madarasa ya amali bado tutahitaji madarasa zaidi. (Makofi)

Sasa tungeachana na huu upungufu. Kwa vile tunafahamu kwamba darasa moja linajengwa kwa shilingi milioni 20, Serikali ingeongeza bajeti basi katika Wizara hii ili tujenge madarasa at least 25 kwa mwaka ambapo itaenda kwenye shilingi bilioni 500 kwa mwaka ili katika historia tutakuwa tumekamilisha upungufu wa madarasa, tukapambana na jambo lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu kuangalia Bajeti ya Wizara ya Elimu, naipongeza Wizara kwa sababu bajeti imefika shilingi trilioni 1.6, lakini ninaangalia bajeti iliyoenda kwenye maendeleo ambayo ni shilingi trilioni 1.1, lakini asilimia 67 ya bajeti hii ambayo ni sawasawa na shilingi bilioni 738.7 inaenda kwa mkopo wa elimu ya juu na asilimia 33 ambayo ni sawasawa na shilingi bilioni 363.1, ndiyo inayoenda kwenye investment. Sasa najaribu kuangalia, watu wanaweza wakaona kwamba bajeti kubwa ya elimu ya maendeleo imefika Shilingi trilioni moja, lakini fedha za investment hapo bado ni kidogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuone kama kweli tuna nia njema ya kuboresha elimu, tuangalie kwamba bajeti inayoenda perse kwenye investment. Kwa sababu ukiangalia fedha inayoenda kwenye mkopo ambayo pengine wanafunzi watakuja kudaiwa, mimi binafsi najaribu kuona labda iwe revolving fund kama siyo hivyo, iwe capacity building. Ingefaa zaidi hata iitwe capacity building, lakini tukiweka kama ndiyo fedha za maendeleo, kama ndiyo investment, kwa vyovyote vile tutakuwa sijui tunajidanganya au tunaiumiza Wizara, kwa sababu uwezo wa kufanya kazi ni mdogo, fedha zinazobaki kwenye investment ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inahitaji kufanya mambo mengi, ikiwa ni pamoja na utafiti, kujenga miundombinu. Naona mara nyingi Waheshimiwa Wabunge mkiuliza kujengewa VETA kwenye majimbo, mkoani, lakini pesa za Wizara ndiyo hizi, kidogo, pamoja na kuwafundisha walimu na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee pia ruzuku ambayo Serikali inatoa kwa shule ya msingi zaidi, inatoa ruzuku ya shilingi 10,000 kwa mwaka. Katika fedha hiyo, shilingi 4,000 inaenda kwenye vitabu, na shilingi 6,000 ndiyo inaenda shuleni. Ukigawanya hiyo shilingi 6,000 kwa mwaka ina maana kwa mwezi ni shilingi 500 kwa mwanafunzi. Hivi mwalimu anaweza kufanyaje kwa shilingi 500 kwa mwezi kwa mwanafunzi mmoja? Ruzuku hii ni kidogo. Kuna walimu wanajiongeza. Kuna clip moja ilikuwa inatembea, mwalimu anafundisha mambo ya kemikali, ameleta maziwa ya mgando, limao, na kadhalika; hivi mwalimu akitaka ku- demonstrate, anataka kufundisha kwa vitendo, ukamwachia shilingi 500 kwa mwezi, anaweza kufanya kitu gani? Kwa hiyo, ruzuku hii ni ndogo, Serikali ifikirie tu kuongeza basi angalau ifike hata shilingi 20,000 au shilingi 25,000 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naona linarudisha nyuma ubora wa elimu ni uhaba na ubora wa walimu. Tumeona uhaba wa walimu ni mkubwa. Kwa shule ya msingi tunaenda kwenye 100,958 na shule ya msingi tunaenda kwenye 74,000, ukijumlisha unapata 175,000. Naipongeza Wizara ya TAMISEMI na Mheshimiwa Rais kwa kutoa kibali hicho cha kuajiri walimu 13,000, lakini kiukweli speed hii ni ndogo, mpaka kuja ku-overcome hiyo gap ya 175,000.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Yustina, muda wako umekwisha.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)