Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi naungana na Wabunge wenzangu kuchangia kwenye Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri wa Elimu na timu yake nzima kwenye marekebisho makubwa aliyofanya kwenye mitaala ya elimu kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wetu mkubwa ilikuwa ni mtaala mzima wa elimu ambao ulikuwa unaleta shida sana, kwamba mtoto aliyesoma ndiyo anakuwa mgogoro zaidi na taabu ngumu zaidi kwa mzazi kuliko yule ambaye hajasoma. Mzazi anateseka, Serikali inateseka na mpaka mwisho hatupati ufumbuzi, lakini kwa mtaala huu alioleta Mheshimiwa Waziri kama hawakuuchakachua wenzetu wasomi, unaweza ukatusaidia kutufikisha mahali pazuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana sana na Mheshimiwa Shigongo alivyosema. Ni kweli kabisa elimu ya sasa hivi Mheshimiwa Waziri, ilikuwa kama gereza, hauna uhuru nayo wewe mzazi. Sasa hivi kwa mtaala huu tunakuomba sana Mheshimiwa Waziri katutofautishie sisi wa vijijini na wale wa mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijijini Mheshimiwa Waziri, watoto wetu sisi ni rasilimali ya kuzalisha mali ndiyo baadaye anaanza shule. Ninyi huku mjini Watoto wenu ni watoto wenye gharama. Kwa hiyo, lazima tutofautishane hapo. Sisi wa kwetu akiwa na miaka minne anaanza shughuli za kilimo pale nyumbani na kuchunga mbuzi, anang’oa mbegu za mpunga anakusaidia kupanda. Kwa hiyo, msije tena mkaleta hapo mkasema, aah sisi mambo human rights, watoto wanateseka, Hapana! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hawa watoto ndiyo wanaolima huu mchele mnaolia kila siku kwamba umepanda bei. Nani mzee anayeweza kuinama kutwa nzima kwenye tope kama siyo watoto? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunaomba sana kwa kuwa umefungua kwamba mzazi akiwa na shida kesho kwamba ana shida, ana kazi yake nyumbani aje aombe ruhusa shuleni kwamba naomba mwanangu, siku tatu tukafanye naye kazi ili baadaye atakuja shuleni Jumatatu. Itatusaidia sana kwa ukubwa huu ambao umeufungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile elimu hii lazima iwe wazi na iwe nyepesi hasa darasa la kwanza. Afundishwe mtoto kitu chenye faida maana yake unaponiambia mimi nikajitegemee lazima kiwepo kitu kinachonivutia, kwamba unaniambia mimi nilime mahindi lazima unieleze kwamba punje fulani, miche fulani ukimwagilia ndoo moja ya gharama hii utapata shilingi hii, ili huyu mtoto awe na interest ya kwenda kufanya ile kazi akiwa bado mdogo. Itatusaidia tumepiga kelele sana muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi nikifika darasa la nne Mheshimiwa Waziri nikawa mtoro lakini ukanifuata ukanikuta kwenye mahindi nalima mahindi ni kosa? Litakuwa kosa gani? Niruhusu nisome hata jioni kama unaona nashinda kwenye mahindi, nisome jioni nitalipa hiyo gharama kwa sababu hii siyo dini, hata dini ina option, kwamba kama hukusali Saa Saba au hukusali Jumapili sala ya asubuhi unaweza kusali ya Saa Saba ili kusudi maisha yaweze kwenda wakati mtoto anasoma na mzazi yuko na mtoto wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la VETA. VETA Mheshimiwa Waziri waongezee mitaala. Tunapoongea hapa VETA hana mtaala wa simu, hana mtaala hata wa television, hana mtaala wa pikipiki. Leo kuna market kubwa sana ya wafanyakazi wa ndani, VETA hana mtaala wa wafanyakazi wa ndani. Utajiri wa nchi za Asia ni wafanyakazi wa ndani. Ninyi mnasema mnafundisha hotel management, kutenga ugali unahitaji kusoma? Haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfanyakazi wa ndani leo hii wote ni mashahidi ukitafuta mfanyakazi wa ndani unampigia Mheshimiwa Jesca kule Iringa unamwambia nitafutie kijana kule mlimani utafikiri unatafuta mbuzi wa mizimu. Yaani ni kazi kweli ni soko kubwa sana. Tulikuwa wote pamoja kwenye mtaala wa elimu, yule jamaa kutoka Philipines alivyosema kwamba utajiri wa Philipines ni wafanyakazi wa ndani ambao wanakwenda nchi za nje. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri wa Elimu weka wafanyakazi wa ndani kwenye mitaala yetu itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakwenda kwenye suala moja ambalo najua ni gumu sana. Tumeruhusu msichana akipata mimba aendelee na shule lakini wanaopata mimba wanaweza kuwa wamebakwa labda mbili, asilimia 98 walielewana lakini sheria yetu inasema na huyu atatumikia kifungo cha miaka 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu yetu ambayo mliitoa mwaka jana Wizara ya Elimu, waliopata mimba shule ya msingi walikuwa 3,850, sekondari walikuwa elfu nane na kitu na ninafahamu kabisa hiyo takwimu kwa sababu kuna maelewano mengi sana kule kijijini, inawezekana msingi walikuwa zaidi ya 10,000, sekondari walikuwa zaidi ya 20,000. Sasa Mheshimiwa Waziri ina maana hawa 40,000 watapatikana watoto 40,000, baba zao watakuwa gerezani. Mwakani tena watapata mimba wengine 80,000 lakini tutakuwa na wafungwa tena 80,000. Je, magereza yetu inaweza kuwabeba? Je, hawa watoto watakapokua wakute wazazi wao wako gerezani miaka 30 watamlaumu nani na kosa lao kubwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni swali gumu, ni kazi yetu Wabunge maana yake tunaamka asubuhi ukiamka nyumbani watu watatu unakuta wana mtoto, kwamba baba yake alifungwa au alitoroka na mimi mtoto wa shule nimeruhusiwa kwenda shule lakini na nyanyaswa pale nyumbani. Mnafahamu wote makabila yetu au wenzetu mnatoka Uingereza? Makabila yetu mnayafahamu msichana anapozalia nyumbani hapendwi na kaka kwa sababu kaka alitarajia kupata ng’ombe 40 nae aoe, mzee naye alitarajia kukaa high table, naye hampendi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huyu msichana anabaki na mateso, na mume naye ametoroka. Sasa Mheshimiwa Waziri labda tulilete kisheria tuone wale ambao hawakubakwa, huyu mwanaume aozeshwe huyu mtoto, aozeshwe huyu msichana ili huyu msichana aendelee na shule akiwa ameolewa. Maana yake hii shule ni kambi tu wazungu walituletea? Shule ni kambi tu siyo wala kitu chochote. Sisi Waafrika hatukuwa na shule. Hii ni kambi tumeletewa ikatengenezwa vizuri ndiyo ikawa shule. Sasa kweli watu wapoteze maisha yao baada ya miaka mitano tutakuwa na watoto laki tano hawana baba ila tuna wafungwa laki tano, magereza yetu yatatosha ukiunganisha na wafungwa wengine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri sisi ambao tunaya-face hayo matatizo kule kijijini, maana yake mwenye mtoto wa kiume anakuja kukulilia kwamba mwanangu amepata matatizo amefungwa ana kesi. Mtoto wa kike naye anakuja pia anasema nina watoto wawili kweli nimeruhusiwa kwenda shule lakini hawa watoto sina wa kuwatunza, atawatunza nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni swali gumu ambalo ni lazima Waheshimiwa Wabunge tulifikirie kwa mapana sana. Mimi sikatai sheria ya kwenda shule nakubaliana nayo asilimia 100, kwamba huyu aliyejifungua aendelee na shule lakini huyu mwanaume anaenda wapi sasa? Anaenda gerezani miaka 30. Mheshimiwa Waziri hiki ni kitu ambacho kiko nje ya utaratibu lakini ni dunia tunayokutana nayo, tutafanya namna gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, familia zingine wamekwenda watu mpaka wanne wapo gerezani lakini hawa wananchi wanakubali hawa waoane na huyu aendelee na shule. Nafikiri tulifikirie kwa mapana sana ili iweze kutunusuru kwenye hili tatizo. Tunaweza kuliona leo ni janga dogo lakini sisi kule vijijini ukiamka asubuhi ni mgogoro kweli. Unashinda kutwa nzima unampigia huku, unaenda gerezani kumuangalia huyu, unamsaidia huyu, mtoto hana baba na kote unakuwa unaendelea na mgogoro, kwa hiyo nashukuru sana Mheshimiwa Waziri kama utaweza kulifikiria kwa mapana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa Mheshimiwa Waziri niliwahi kuleta hoja hapa kwamba watoto iwe lazima kuwatunza wazazi siyo wajibu, lakini naona sheria hiyo bado. Mheshimiwa Waziri lazima tuifikirie kwa mapana sana. Mimi nimefanya kazi kubwa na mtoto wangu kutoka akiwa nursery school mpaka form six. Wewe Serikali umempenda umemuona ana akili umekuja kumchukua, anakuja kukufanyia kazi wewe, unamkopesha wewe na shule anasoma ya kwako, wewe faida unachukua wewe na anakuja kukufanyia kazi na unamkata. Mimi huyu mzazi wala hunisaidii, yaani hakuna chochote chenye value kwangu wala huna habari. Ni kweli mbona timu za mpira, mtu anapojua mpira anapocheza mpira si unapata na wewe uliyemtunza au timu iliyomtunza? Itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri na ninarudisha pongezi nyingi kwako na shukrani nyingi sana zimuendee Mheshimiwa Rais kwa kuturuhusu kulijadili hili suala la elimu na hadi tulipofikia sasa hivi nashukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)