Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika hoja hii muhimu ya hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa natoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoleta mageuzi makubwa katika Sekta hii ya Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu katika Bajeti ya Wizara hii ya Elimu, nitajikita katika eneo la lishe na hapa naomba nitambue kwamba eneo la lishe ni moja ya maeneo ya vipaumbele ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tokea akiwa Makamu wa Rais. Vilevile eneo hili la lishe ni moja ya vipaumbele ambavyo vimeainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, chama changu pendwa ya mwaka 2020 - 2025 ukienda kwenye ukurasa wa saba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo, naomba nirejee katika Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 ambayo hivi sasa inafanyiwa mapitio. Katika sera hii imeainisha bayana kwamba Serikali itahakikisha inatoa huduma muhimu ikiwemo chakula shuleni. Naamini Serikali ilifanya vile kwa kutambua umuhimu wa chakula na lishe shuleni, lakini kwa bahati mbaya sana utekelezaji wa suala hili umekuwa na changamoto kubwa na hautekelezeki ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kelele nyingi za wazazi pamoja na wadau, niipongeze Wizara ya Elimu ilifanya tafiti na baadaye ikaleta mwongozo. Mwongozo huu hapa ambao ulizinduliwa mwaka 2021 ambao ni Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma wa Chakula na Lishe kwa Wanafunzi wa Elimu ya Msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwongozo huu na kutokana na tafiti iliyofanywa na Wizara ya Elimu, ilibaini kwamba katika shule za kutwa asilimia 70 hazitoi huduma ya chakula na lishe shuleni. Kwa msingi huo nifanye rejea ndogo tu, kwamba kwa takwimu za mwaka 2021 za Serikali shule za msingi ambazo tunazo hapa Tanzania ni takribani 18,546 na jumla ya wanafunzi ambao wako kwenye shule hizi za msingi ni takribani milioni 11.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijirejea kwenye ile asilimia 70 ya shule zetu hazitoi chakula na lishe shuleni. Kwa muktadha huo inamaanisha kwa mwaka 2021 jumla ya watoto takribani milioni 7.9 walikuwa wanaenda shule wana shinda na njaa na dunia imeshatambua ikiwemo WHO, World Bank na Mataifa ya nje na hata hapa ndani, hapa nchini kwamba chakula na lishe vina mchango mkubwa moja kwa moja katika makuzi ya mtoto pamoja na ufaulu wa darasani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata na wenyewe Wizara ya Elimu wametambua na wameiweka humo kwenye mwongozo ambao wameutoa. Sasa nimejaribu kufanya ulinganifu ambao Wizara ya Elimu inaweza ikafanya tafiti nzuri zaidi na kukokotoa kwa kina zaidi. Matokeo ya mwaka 2022 mwaka jana ya mtihani wa kidato cha nne, asilimia 51 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana walipata division four. Asilimia 12 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani kwa mwaka 2022 walipata divison zero, ukijumlisha hizi asilimia 51 na asilimia 12, unapata asilimia 63, ambayo haipishani sana na ile asilimia 70 ya shule ambazo hazitoi chakula na lishe shuleni. Kwa hiyo kwa muktadha huo unaweza ukaona kwa tafiti na ulinganifu wa haraka haraka kwamba ni dhahiri pamoja na sababu zingine ukosefu wa chakula na lishe shuleni una mchango mkubwa katika ufaulu wa wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo linalonisikitisha ni kwamba japokuwa kule kwenye Sera ya Mwaka 2014, Serikali imetambua na kusema kwamba Serikali itahakikisha inatoa huduma muhimu katika shule ikiwemo chakula shuleni. Sasa cha kushangaza katika mwongozo huu wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe shuleni, Serikali imejivua jukumu hilo na badala yake imeelekeza kwamba utekelezaji wa mwongozo wa chakula na lishe shuleni ni jukumu la jamii na wazazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo linasikitisha kwa sababu, ni Serikali hii hii kwa kutambua uwezo na uchumi hafifu wa wananchi na wazazi uliamua kuja na elimu bure ili kumwondolea mzazi mzigo wa kulipa ada na michango mbalimbali lakini Serikali hii hii kwa kutambua wazazi wale wale, sasa imeamua kuwavika wao jukumu la huduma ya chakula na lishe shuleni na yenyewe ikajiondolea jukumu hilo wakati katika Sera ya Elimu ya 2014, inatambua kwamba hilo ni jukumu la msingi la Serikali. Kwa hiyo jambo hili linahitaji liangaliwe kwa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu kuna kitu kinaitwa human capital development, rasilimali watu, kwa Taifa kama la Tanzania kama ambavyo linakua kwa kasi inayokua, kwa uwekezaji mkubwa ambao unafanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan tusipowekeza vya kutosha kwenye hii rasilimali watu yetu tutajikuta huko mbeleni tuko kwenye shida. Kwa hiyo, niombe sana Wizara ya Elimu wanapofanya mapitio ya mitaala pamoja na mipango mingine, tutafute namna ya kuhakikisha ya kwamba suala la chakula na lishe shuleni liwe ni suala la msingi kwa sababu si suala la anasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mapendekezo mawili yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo la kwanza, ninaiomba sana Wizara ya Elimu ichakate namna ambavyo chakula na lishe shuleni kinatakiwa kitolewe, kwa sababu hivi sasa hakuna mwongozo. Huu mwongozo uliotolewa ni mzuri lakini mwongozo katika maneno, hakuna mwongozo ambao unasema hicho chakula na lishe ni cha aina gani? Hicho chakula na lishe wastani wa gharama kwa kila mwanafunzi ni kiasi gani kwa mwezi ili wazazi wajue kwanza ni kiwango gani. Maana yake hivi sasa kila shule inajipangia yenyewe kiwango chake lakini pia lazima kuwe kuna uhakika hicho chakula kinachotolewa kweli kina lishe au ni chakula ili mradi tu kushibisha tumbo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa pili. Serikali kupitia Wizara ya Elimu itafute namna ya kutokwepa jukumu lake la msingi la kuchangia na kuhakikisha katika shule zetu kuna huduma ya chakula na lishe, hivyo ichangie katika gharama. Serikali inatoa ruzuku kwenye maeneo mengine kupitia capitation. Kwa hiyo, ninaiomba Wizara ione namna gani ambavyo na yenyewe kulingana na ule mwongozo utakaokuwa umenyambulisha gharama za kila mtoto kupata chakula na lishe shuleni, Serikali ichangie walau asilimia 60 na wazazi wachangie asilimia 40 lakini hiyo ionekane wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa niipongeze sana Serikali kupitia Wizara ya Elimu. Mwaka jana mwezi wa Tisa, Serikali kupitia Wizara ya Elimu wamejiunga na kitu kinaitwa School Meals Coalition. Huu ni mpango wa dunia ambao nchi zinajiunga na moja ya ahadi ambazo wanaweka ni kwamba ifikapo mwaka 2030 kila mtoto katika kila shule atapata walau mlo mmoja wa chakula na lishe kwenye shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa 2030 siyo mbali, hatutaweza kufika kama Wizara ya Elimu itaendelea kutolitilia maanani suala hili na kuanza kuwa na mipango nalo. Kwa hiyo, hapa jambo kubwa ambalo lipo niombe sana Wizara itafute namna ambavyo itapata fedha kwa ajili ya kufanikisha jambo hili na fedha zipo duniani. Yako mashirika ya kimataifa na iko mipango ya kimataifa ambayo tayari inasaidia nchi zingine Barani Afrika kutekeleza ajenda ya chakula na lishe shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo niliwahi kusema katika moja ya michango yangu hapa kwenye bajeti hii hii ni GPE (Global Partnership for Education). Tunayo bahati kubwa kwamba Mwenyekiti wa GPE ni Rais Mstaafu wa Tanzania, Mheshimiwa Dokta Jakaya Kikwete. Sasa tunashindwa nini kutumia fursa hiyo ikiwa wanachangia GPE wanasaidia nchi zingine Barani Afrika na sisi pia Tanzania tunaweza tukapata fursa hiyo, lakini hata Benki ya Dunia hata IMF, AFDB zote zinajikita katika kutekeleza katika eneo hili pamoja na UNICEF. Kwa hiyo mimi naamini kwamba fursa hizi zipo, ikiwa tu tutaamua kulibeba jambo hili kwa uzito unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuhitimisha kwa kuiomba sana Serikali kwa kumuomba sana Profesa Adolf Mkenda, kwa sababu natambua anajua umuhimu wa chakula na lishe kwa Watoto, umuhimu wa chakula na lishe katika ufaulu. Tutafanya yote na yote yanaweza yakawa yasiwe na tija inayotakiwa au tija inayotarajiwa endapo tutaendelea kuruhusu watoto wetu asilimia 70 waendelee kuwa wanaenda shule na wanakaa na njaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)