Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote na mimi nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi leo tuweze kuchangia hoja iliyoko mezani. Nianze kwa kutoa shukrani zangu kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo amei-support vizuri sekta ya elimu hususani katika jimbo langu la Kilolo lakini na nchi nzima kwa ujumla. Tunayo mengi ya kusema lakini tushukuru sana kwanza kwa ahadi yake ya kujenga vyuo vya ufundi VETA ambavyo pia Wilaya ya Kilolo ni wanufaika na ujenzi unaendelea hivi tunavyozungumza; tunaona kazi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nishukuru kwa ujenzi wa shule za wasichana za mikoa ambapo kwa Mkoa wa Iringa itajengwa katika Wilaya ya Kilolo. Ninafahamu kwamba maandalizi yanaendelea na sisi tunaisubiri kwa hamu, tumejiandaa tumejipanga na eneo lipo tayari. Ni kazi tu ya kuanza ujenzi ndiyo inayosubiriwa. Kwa hiyo tunashukuru sana kwa kazi zinazofanywa na Mheshimiwa Rais na sisi tuko tayari kushirikiana naye na kuendelea kumuunga mkono.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nipongeze juhudi zinazofanywa na wizara katika kuboresha mitaala ambayo imekuwa ni kilio chetu muda mrefu humu ndani. Mimi ninaamini majadiliano yanayoendelea yatatupa mtaala bora ambao utaendana na mazingira na hali ilivyo kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninao ushauri katika masuala machache ambayo yanaenda kwenye Sera ya Elimu na taratibu mbalimbali, na nianze kwanza na suala la udhibiti ubora. Lakini nizungumzie kidogo kipengele cha mitihani na nizungumze jinsi wasimamizi wa mitihani wanavyopatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, walimu wanaofundisha shule mbalimbali za sekondari huchukulia kwamba ule usimamiziwa mitihani ni fursa kwao kwa namna mbalimbali kama vile kukua na kujifunza, kusimamia pamoja na kusahihisha. Kukua na kujifunza kuelewa zaidi lakini pia ni fursa kwao kwa sababu ina kipato pia zaidi. Sasa, namna wanavyopatikana hakuna uwazi wa kutosha wa kuwafanya wale ambao hawakuchaguliwa waridhike kwamba na wao hawakuchaguliwa kihalali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependekeza kwamba kuwe na utaratibu mzuri wa uchaguzi wa walimu wanaosimamia mitihani na vigezo. Yaani kuwe na mwongozo mzuri unaosema vigezo vya walimu wanaosimamia mitihani namna wanavyopatikana, wale wanaosahihisha mitihani na namna wanavyopatikana, ili kuondoa malalamiko au kuondoa mtu mmoja kuhodhi maamuzi ambayo inawezekana inaweza kupelekea mianya ya rushwa kwa walimu wetu ambao pia vipato vyao si vikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo ni la kwanza, ningependekeza hata tunavyotengeneza sera pia iangalie hicho kipengele, kwamba ni namna gani usimamizi na usahihishaji wa mitihani unafanyika na hao wanaofanya hiyo kazi wanapatikanaje. Ikiwa wazi kwa namna yoyote ile inapunguza malalamiko kwa hiyo linakuwa ni jambo ambalo linauwazi wa kutosha, hilo ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo kisera halijakaa vizuri; wote tunajua kwamba watoto katika shule zote, chekechea, msingi, na sekondari, sasa hivi hizi shule nyingi ni shule za kutwa, liko jambo la chakula cha mchana, sasa jambo la chakula cha mchana limetiwa nguvu sana na umuhimu wa lishe bora kwa watoto wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo jema na wazazi wamelipokea vizuri. Katika mazingira ya elimu bila malipo wanafunzi wengi wanachangia. Lakini nataka nikupe scenario moja, unakuta kwenye kata kuna shule mzazi anatakiwa kuleta mahindi debe moja kila mwezi lakini kuna shule mzazi anatakiwa kuleta debe tatu kila mwezi na mwingine anatakiwa kuleta kilo tano kila mwezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kawaida sisi wote tuna utaalamu wa kutosha wa kujua ratio za chakula kwa sababu tunazo shule za bweni tunajua Watoto wanatakiwa kula nini mchana. Utaratibu ambao ungeweza kuwa mzuri ni mwongozo wa uchangiaji wa chakula kwenye hizi shule ili kusiwe na mtu anaamua tu. Ndiyo maana wazazi wakati mwingine wanakuwa wagumu kuchangia kwa sababu hakuna kigezo kinachotumika kujua ratio ya mwanafunzi ya chakula lakini yule anayeamua mengi anaweza akawa na nia ovu, inatoa fursa au mwanya kwa mtu ambaye yeye ana mipango yake ya kuchangisha chakula zaidi kwa jambo la kwake yeye aweze kufanya hivyo kama Wizara haikutoa muongozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba Wizara ya Elimu fanyeni utafiti njooni na ratio ya chakula mtoto anachotakiwa kula ili mzazi aambiwe kwa mujibu wa taratibu unatakiwa kuchangia hiki ili mtoto wako ala chakula cha mchana, na hiyo itapunguza kabisa malalamiko yale yanayojitokeza. Na itapunguza, wakati mwingine unakuta wamekusanya mahindi yamebaki shuleni kwa sababu walichangisha zaidi au wakati mwingine ni majaribu sasa kwa walimu wale kupata majaribu sasa ya kuuza au kufanya jambo lingine ambayo inapelekea mwakani uchangishaji unakuwa mgumu. Suala hili ni la miongozo. Kwa hiyo mshirikiane na TAMISEMI kutoa muongozo mzuri ili hili nalo liweze kwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kuhusu mikopo ya vyuo vikuu. Kuna changamoto ndogo ambapo mtu ameomba mkopo hakupata. Kimsingi huwa mtoa tu majina hamuwezi kumwambia kwa nini hukupata, na kwa sababu hajui anakata rufaa akikata rufaa majina yanatoka tena hayasemi tena kwa nini rufaa yake haikukubaliwa; mwakani anakata tena rufaa hivyohivyo mpaka akiendelea kujaribisha mpaka atakapopata. Nafikiri mifumo ya rufaa huwa inamrejesho. Kwa sababu ni vibaya kuendelea kumtumainisha huyu mtu kwamba akikata rufaa mwakani atapata. Kwa hiyo kama bodi imeona kuwa huyu mtu hakopesheki imjulishe kwamba wewe hautakopeshwa mpaka utakapomaliza miaka yako mitatu ili asiendelee kupata shida ya kukata rufaa kukata rufaa wakati kiukweli bodi imesharidhika kwamba huyu mtu hakopesheki na impe majibu kwamba kwa nini hakopesheki.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili tumelizungumza muda mrefu hapa bungeni; kwa sababu wakati mwingine unakuta huyu ni mtoto kweli wa maskini labda au alisoma shule za kanisa na kwa hiyo pengine au shule hizi za binafsi kwa kulipiwa na mfadhiri na vigezo vingine vingi. Sasa kadiri ambavyo anazidi kukata rufaa anategemea; ni kama bahati nasibu. Mimi nisingependa bodi ya mikopo ifanye kukata rufaa kama bahati nasibu. Kwamba sijui nitapata au sijui sitapata tena; anakata rufaa wakati mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwe na mfumo wa taarifa, yaani wa mrejeshi. Kwamba sababu ambazo zimekufanya usikate ni hizi na kwa hiyo kama hazitarekebishika hautapata, au wewe usiombe tena kwa sababu umekataliwa, au wanaoruhusiwa kukata rufaa watolewe orodha kwamba ninyi mnaweza kukata rufaa. Kwa hiyo hao watu wataona pale kwenye orodha; kwamba hawa ndio mnaoweza kukata rufaa na hawa hawawezi kukata rufaa ili shughuli ziendelee na wale ambao hawastahili kukata rufaa wa sikate rufaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine la mwisho ambalo ningependa kuzungumza ni namna elimu inavyosimamiwa, na hasa kwenye Vyuo Vikuu. Tunavyo sasa vyuo vikuu ambavyo vinasimamiwa na Wizara moja kwa moja lakini kuna vyuo mbalimbali vinavyosimamiwa na Wizara nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninafikiri hili ni suala la Elimu kwa sababu watoto wote wanaosoma wanatarajia kuingia kwenye soko la ajira kwenye sekta zote. Yaani kama ni kwenye Serikali za mitaa wanatakiwa kuingia kwenye sekta zote. Kama ni kwenye sekta ya fedha wataingia kwenye sekta zote. Kama ni kwenye sekta ya michezo wataingia kwenye sekta zote kama kila Wizara itaanzisha chuo kwa ajili ya watu wa taaluma yake vile vyuo vikuu vingine vinakosa relevance.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningefikiria kwamba kuwe na mfumo tu mmoja wa vyuo vikuu vyote na viwe vinasimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kwa hiyo watoto wanapomaliza wote wanakwenda kwenye utaratibu wa kutafuta ajira, kunaweza kukawa na vyuo vyenye msisitizo wa jambo fulani. Kwa hiyo kunaweza kukawa na vyuo vya madaktari ambavyo havisimamiwi na Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kunaweza kukawa na vyuo vya watumishi wa Serikali za mitaa ambazo hazisimamiwi na TAMISEMI, au vyuo vya michezo ambavyo havisimamiwi na Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kwa sababu mwisho wote wanomaliza wanaingia kwenye soko la ajira moja na kwa hiyo hakuna sababu ya kwamba vyuo hivi visimamiwe na watu wengine. Lakini pia Serikali ni moja; kwa hiyo sualala uratibu wa elimu likiratibiwa na sehemu moja, hasa kwenye hii mitaala tunayoendelea litakuwa jambo zuri kwa sababu uratibu ule utafanyika kwa uzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa niwakumbushe tu kwamba kwenye upungufu wa walimu kwa kweli baadhi ya wilaya zilizoko pembezoni zina shida sana, hasa kwa mfano Wilaya ya Kilolo, kuna maeneo kwa kweli ni changamoto, tunaona walimu wawili watatu. Kwa hiyo changamoto ya walimu pia kwa kushirikiana na TAMISEMI inapofika wakati wa kuitatua basi tuangalie pia maeneo ambayo yana changamoto kubwa ili yaweze kuapta kipaumbele katika kupangiwa walimu zaidi na ili hiyo changamoto iweze kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)