Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na mimi kuniruhusu nichangie hii hoja ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa bajeti yao ya mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitachangia mambo mawili tu, la kwanza, litakuwa lugha ya kufundishia na la pili, elimu ya ufundi. Mambo haya mawili sio mageni humu Bungeni na wala sio mageni Serikali na hasa mimi pia sio mgeni kwenye mambo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nijiunge na watu wote Wabunge waliochangia kuishukuru Serikali yetu. Serikali hii ya Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya mambo makubwa sana katika kukuza elimu na hasa bajeti pia. Pia tunapata elimu bure, ujenzi wa miundombinu, madarasa, maabara, nyumba za walimu lakini mabweni. Hii inatupunguzia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Pofresa Mkenda na Wizara yake kwa kujituma sana na kuonesha haya, kuyatekeleza maoni ya Mheshimiwa Rais, kwa vitendo, wote Wizarani nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la lugha kufundishia elimu yetu, najua liko tatizo la watu kupenda mambo ya kigeni, kupenda mambo ya kizungu. Moja kwa lugha lakini pia hata kwa mavazi na kusema mtoto huyu amesoma sana anaongea kingereza kama maji au anaongea kifaransa kama maji. Kwa hiyo, amesoma sana, wanalinganisha elimu na lugha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi hapa Tanzania, Serikali ilikuwa na mpango mzuri wa kuendelea kutumia kiswahili kama lugha ya kufundishia na ikachukua muda mrefu, Serikali iligharamia gharama kubwa sana kuandaa vitabu vya kufundishia baada ya Elimu ya darasa la saba Kidato cha kwanza na chapili na wataalamu kule TATAKI Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliandaa vitabu hivyo wakiwa tayari sasa baada ya tafiti nyingi kuonyesha kwamba mtoto ili aelewe maarifa lazima afundishwe kwa lugha ya mama yake, na lugha ya mama hapa Tanzania asilimia 85 ni kiswahili kwa hiyo Serikali ilijikita kufanya tafiti na kupata majibu hayo wakaamua sasa watafute vitabu vya kufundishia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iligharamia gharama kubwa sana kuandaa vitabu vya kufundishia baada ya elimu ya darasa la saba Kidato cha kwanza na chapili na wataalamu kule TATAKI Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliandaa vitabu hivyo ikiwa tayari sasa baada ya tafiti nyingi kuonyesha kwamba mtoto ili aelewe maarifa lazima afundishwe kwa lugha ya mama yake, na lugha ya mama hapa Tanzania asilimia 85 ni Kiswahili. Kwa hiyo Serikali ilijikita kufanya tafiti na kupata majibu hayo wakaamua sasa watafute vitabu vya kufundishia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi hapa leo nimesikitika sana matokeo ya Tume ya mapitio ya Sera pamoja na Mitaala kupendekeza kwamba nyuma tutakuwa na lugha mbili za kufundishia kama ilivyokuwa zamani kiingereza na Kiswahili. Hii mimi ninaona kwamba tunarudi hatua kubwa sana nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spoika, mimi hapa nina vitabu. Jiografia kidato cha pili na mwandishi, ni Makunda lakini pia hiostoria kidato cha kwanza na Mwandishi Sago na Jiografia kidata cha kwanza, mwandishisi Makunda huyo. Pia nina kitabu Misingi ya Umeme na Sumaku, mwandishi Almasi Maige. Pia nina kitabu hapa kidato cha kwanza baiolojia mwandishi Isack na mwenzie Mustapha, nina kitabu hapa cha kidato cha kwanza Jifunze Kemia mwandishi Lema na Kimbi, nina kitabu hapa Uraia Kidato cha Kwanza mwandishi Kajigiri lakini nina kitabu hapa Mwandani wa Fundi Umeme mwandishi Almasi Maige, nina kitabu hapa cha Hisabati Kidato cha Kwanza mwandishi Saidi Sima, na nina kitabu hapa cha Fizikia Kidato cha Kwanza mwandishi Thadei na mwenzie Kiiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini kimetokea kupiga gia ya kinyume Serikali bila kutoa sababu. Mimi ningefurahi sana Waziri akisimama hapa atoe sababu kwa nini wameamua kurudi nyuma baada ya gharama kubwa hii iliyofanywa na Serikali ya vitabu vyote kidato cha kwanza na cha pili na kuwa tayari nani amesema turudi nyuma?

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna nchi yoyote iliyoendelea kisayansi kwa kutumia lugha ya watu wengine. Wafaransa Kifaransa, Waingereza Kiingereza, Warusi Kirusi, Wajerumani Kijerumani, Wachina Kachina, na kadhalika. Zipo nchi pia za wenzetu, Misri katika Afrika na nchi nyingine kadhaa sisi nini kinatushinda?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Kiswahili kimekua na kutumiwa kote, lakini kinachoendelea kule wanasoma kama somo. Mapendekezo ya mapitio ya sera pamoja na elimu wanasema na sisi Tanzania tunatumia Kiswahili kama somo. Ndio wenye Kiswahili lakini tunatumia Kiswahili kama somo. Sisi tulitaka, mimi na wenzangu ambao ni wazalendo, wanapenda lugha ya Kiswahili, tuna uthibitisho kwamba mtoto akifundishwa Kiswahili ataelewa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejivua, inasema kwamba wanaotaka sasa kutumia Kiswahili waanzishe shule zao na wanaotaka Kiingereza waanzishe shule zao. Inawezekana, watu hao watakaoanzisha shule zao watapata wapi gharama za kutafsiri vitabu kama hivi vyote viwe vya Kiswahili, watapata wapi walimu hawa wa kufundisha? Hili ni jukumu la Serikali. Serikali inashindwa, Serikali sasa ituambie kwamba sasa jukumu la elimu liwe kwa watu binafsi. Kwa sababu ni nani mtu binafsi ataanzisha shule ya Kiswahili? Haiwezekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kukwepa, wanafanya mchepuko kwa sababu ambazo sisi hatuzijui. Mimi sijaelewa kwa nini Serikali isije na msimamo wa kusema hatutaki elimu hii ifundishwe Kiswahili. Na mimi nimekuwa nasema, kwa nini Serikali isianzishe shule ya mfano watoto wakasoma darasa la kwanza mpaka la sita Kiswahili, wakaendelea mpaka sekondari school Kiswahili? Labda hadi kidato cha pili cha tatu na cha nne tukaona matokeo yake? Kwa sababu watakuwa wanasoma Kiingereza kuanzia darasa la kwanza watakuwa pia wanajua Kiingereza. Kwa hiyo ikionekana elimu haifundishiki Kiswahili huko mbele hii shule watajiunga Kiingereza. Kwanini Serikali haitaki kufanya hivyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wengi wanatushangaa sana Watanzania, sana, nawaambieni. Mimi nasafirisha rangi nchi za nje kule, nikiwaulizia taaluma yetu ifundishweje wanasema kwa nini msitumie Kiswahili kama vile Wachina, Wafaransa, Waingereza na kadhalika? Kwetu ni nini kimetokea? Mimi ninapendekeza Serikali isijivue jukumu la kuendesha shule ya mfano ya Kiingereza, lakini pia nashauri vilevile pamoja na kuanzisha shule hiyo Serikali ianzishe shule hiyo ya mfano na shule hiyo iangaliwe, ichague wanafunzi wazuri kuanzia darasa la kwanza mpaka shule ya sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naiongelea Elimu ya ufundi. Ninaipongeza sana Serikali kwa kuja na mfumo ule na kubainisha kwamba kunatakiwa kuwe na mitaala miwili, mmoja unaitwa huu elimu amali au elimu ya ufundi. Wako watu humu ndani tulisoma elimu hiyo ya ufundi, akina engineer manyanya. Tuliicha baadaye kwa sababu ilionekana kwamba huko mkimaliza wote mna-degree sawa huyo aliyesoma mtaala wa ufundi na aliyesoma mtaala wa kawaida tunapata mishahara tofauti. Mtu aliyesoma kutoka Dar es Salaam Technical College akarudi kuwa mhandisi pale anapata mshahara kima cha chini ya mhandisi aliyesoma chuo kikuu, kwa hiyo Elimu hiyo ikafa. Leo tumeona, ninawapongeza sana. Kwamba mitaala yote miwili itaenda sawa na mtu wa mwisho kule, mhandisi wa mwisho kutoka taaluma hii ya amali na ya kawaida wote watakuwa na thamani sawa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.