Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nami awali ya yote nitoe pongezi sana kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa fedha nyingi anazozitoa kwa ajili ya ujenzi wa sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Mama ametoa fedha nyingi sana kwa maana ya kupeleka fedha kwenye sekta ya elimu pamoja na sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutoa pongezi zangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Ndugu yangu Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, kwa kazi kubwa anayofanya, pamoja na Naibu Waziri wake ambaye ni Mheshimiwa QS Kipanga. Vilevile nimpongeze sana Katibu Mkuu wa Wizara hii, Dada yangu Profesa Carolyne Nombo, anafanya kazi vizuri sana na Naibu Makatibu wakuu wake wwili ambao ni Profesa James Mdoe na Dkt. Rwezimula.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pongezi kwa Kamishna wa Elimu ambaye ndiyo Mwalimu Mkuu wa Tanzania pamoja na Wakuu wa Taasisi zote ambazo ziko chini ya Wizara hii ya Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nikueleze, katika Wizara ambazo wanasikiliza ushuri, Wizara ya Elimu wanasikiliza sana ushauri na hasa wa Kamati. Mnafahamu mimi nimekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, nimefanya nao kazi, kwa kweli Wizara ina viongozi wanaosikiliza sana ushauri wa Wabunge. Mwenyezi Mungu awabariki kwenye jambo hili, endeleeni kusikiliza ushauri na kuishinikiza Serikali kutimiza yale ambayo Wabunge wanayashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kupongeza Wizara na hasa katika Jimbo langu la Maswa Mashariki. Wamenipa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi ya Mwabalatulu katika Kata ya Mpindo, lakini vilevile wamenipa fedha kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Mwangala Sekondari, wamenipa fedha kwa ajili ya ujenzi au ukarabati wa shule kongwe ambayo fedha tulipeleka katika Shule ya Msingi Shanwa. Kwa kweli ukarabati umefanyika na kwa kweli wamefanya kazi kubwa na nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado niendelee kushukuru kwa fedha walizozitoa katika programu ya ujenzi wa shule 63 za VETA, Maswa nayo imekuwa mnufaika, tumepata fedha ambayo inakwenda kujenga shule ya VETA na kwa kweli ujenzi huu unaendelea. Niwaombe Wanamaswa wenzangu kwamba tuusimamie vizuri ujenzi huu ili tuweze kupata shule kwa haraka na watoto wetu waweze kujifunza.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kupongeza Wizara hii, kama nilivyosema wanasikiliza ushauri. Niwapongeze sana kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuandaa mitaala na sera ya elimu. Tumeona hapa juzi Tarehe 12 – 14 kongamano kubwa hapa Dodoma. Haijawahi kutokea, watu 1,500, wataalam mbalimbali wadau wa elimu wamekuja katika Mji wa Dodoma kutoa mawazo yao kuhusu namna ya kuboresha sera na mitaala ya elimu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado taarifa kupitia kwa Mheshimiwa Waziri inasema kuna Watanzania 250 nao ni wataalam, wametoa maoni yao na ushauri wao kupitia njia ya mtandao katika kuhakikisha kwamba wanatoa michango yao ili kuboresha suala la elimu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutoa ushauri katika sekta ya elimu ya ufundi. Tumeona ujenzi wa VETA, kila Wilaya VETA zinakwenda kujengwa. Tumeona mikakati ya Wizara ya Elimu katika kutoa elimu ya ufundi, sawa kabisa. Ushauri wangu tuendelee kuwafundisha walimu ambao watakwenda kufundisha elimu ya ufundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru mkakati wa Wizara ya Elimu mmetenga vyuo kumi vya mwanzo kwa ajili ya kutoa elimu ya walimu wanaokwenda kufundisha ufundi. Mahitaji ya walimu wa ufundi yanakwenda kuongezeka, tunaomba sana vyuo hivi ambavyo mnakwenda kuviandaa basi mviandae vizuri na kuhakikisha kwamba mnafanya udahili wa kutosha kuhakikisha kwamba vijana wengi wanakwenda kupata elimu ya ufundi na ufundi wenyewe ni ule wa kisasa kwa teknolojia za kisasa ili hawa waende kuwafundisha wanafunzi katika hivi vyuo ambavyo tunakwenda kuvianzisha katika kila Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema haya kwa sababu tunakwenda kujenga vyuo vya VETA lakini tusipokuwa makini tutaanza tena mgogoro uleule wa kutafuta walimu wa ufundi. Kwa hiyo, ni lazima tujiandae kwa hili. Tunajenga vyuo, basi tuandae na human resources kwa maana ya walimu wanaokwenda kufundisha elimu hii ya ufundi katika vyuo hivyo, hili ni jambo la msingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika vyuo hivi vinavyokwenda kujengwa, baada ya muda kidogo, miaka miwili, mitatu kutakuwa na uzalishaji wa wanafunzi ambao wamepewa elimu katika vyuo hivi. Baada ya kuzalishwa katika vyuo hivi, hao wanafunzi wanakwenda wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ushauri. Kwanza Wizara hii pamoja na Serikali kupitia Hazina, Waziri wa Fedha kama yupo ananisikia, tuanze kutenga fedha kwa ajili ya training factories katika Wilaya zote hapa nchini. Hizi training factories zitaendelea kupokea wanafunzi, watajifunza wanafunzi mbalimbali, lakini hizi factory zitumike kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo zinatokana na mazingira husika katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ambao ninaweza nikautoa katika hili, kuna maeneo ya uchimbaji wa madini, kwa mfano uchimbaji wa dhahabu, kuna mitambo mingi inatumika maeneo yale na kuna vipuli vinaagizwa kutoka maeneo mbalimbali, lakini tukiwa na factory industries, yaani kwa maana ya kwamba viwanda vidogo ambavyo vinaweza vikazalisha vipuli katika maeneo hayo, na wanafunzi wa maeneo yale wakaingia kwa ajili ya uzalishaji wa vipuli katika maeneo hayo hayo, hili litakuwa na tija kwa maana ya kwamba wataendelea kupata mafunzo na pia wataendelea kupata kipato kwa sababu watakuwa wanazalisha. Kwa hiyo, hizi factories ni very very important. Serikali sasa ianze kuangalia kwa sababu tayari tunakwenda kupata output kubwa ya wanafunzi waliojifunza katika vyuo hivi vya VETA.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kushauri tena, tumeambiwa, hata msemaji aliyepita amezungumza kwamba tukitaka kujenga Taifa, tujikite katika kuwekeza kwenye elimu, lakini vile vile tuelewe kabisa kuwekeza kwenye elimu ni njia ya kumkomboa kijana wa Kitanzania. Pia kuna jambo lingine la michezo ambalo Mheshimiwa Waziri amezungumza, kwenda kuanzisha vyuo vya michezo kwa maeneo mbalimbali. Kwa kweli lazima tufundishe vijana wengine ambao wanakwenda kufundisha elimu ya michezo katika vyuo mbalimbali. Tuna vijana wa kitanzania wana uwezo mkubwa, wana vipaji vya mpira, michezo mbalimblia ikiwa ni pamoja na vipaji vya usanii kwa maana ya kuimba na kucheza ngoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tupate walimu wa kufundisha na kuweza kufanya talent identification. Siyo hivyo tu, ni lazima tuweke na mkakati wa kufanya talent development, kwa maana ya kwamba lazima vipaji hivi viendelezwe ikiwa ni pamoja na yale masuala ya uvumbuzi mbalimbali ambao tayari Wizara ya Elimu imeanza kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwenye suala la UNESCO. Niungane na Kamati, imetoa ushauri mzuri, na tumekuwa tukitoa ushauri mara kwa mara. Tume ya UNESCO iko chini ya Wizara ya Elimu. Tume ya UNESCO haifai kukaa chini ya Wizara ya Elimu. Serikali naomba msikie, Tume ya UNESCO inasimamia mambo mbalimbali na mambo mtambuka ikiwemo masuala ya urithi wa dunia. Kwa mfano, yule mjusi mkubwa aliyeko Ujerumani, mtu wa kwanza kwenda kumdai yule mjusi ni Tume ya UNESCO. Sasa lini Wizara ya Maliasili itaongea na Wizara ya Elimu kuhusu UNESCO aibuke aende kule kumdai yule mjusi?

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la UNESCO ni suala mtambuka. Kamati imesema kwamba iende kwenye Wizara mtambuka. Ingesema tu moja kwa moja straight kwamba UNESCO iende chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikafanye kazi yake vizuri. Hilo naomba nitoe ushauri, na kwa kweli bila kufanya hivyo UNESCO itaonekana kama vile ni mtoto ambaye hajaliwi na Wizara ya Elimu, na kwa kweli hana kazi na Wizara ya Elimu. Ana component moja tu. Tunaomba sana, ushauri wa kamati unaposema kwamba UNESCO iondolewe chini ya Wizara ya Elimu, ushauri huo uzingatiwe, iende chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ikafanye kazi yake inavyostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)