Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Esther Edwin Maleko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika sekta hii muhimu kabisa ya elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Rais wetu mpendwa, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya. Tumeona bajeti ya sekta ya elimu imeongezwa kwa wastani wa asilimia 18, imetoka bilioni 4.7 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia bilioni 5.7 kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nisiache pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Kaka yangu, Mheshimiwa Profesa Mkenda, pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Kipanga, kwa kazi nzuri wanayoifanya. Nitakuwa ni mchoyo wa fadhila pia nisipowapongeza Watendaji wote wa Wizara hii kwa sabbau tunaona kazi nzuri sana inayofanyika ya kuendeleza elimu katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Wizara ya Elimu kwa kazi kubwa wanayoifanya. Tumeona wigo wa elimu bila ada umeongezwa kwa Kidato cha Nne, Kidato cha Tano na Kidato cha Sita. Serikali inatenga takribani shilingi bilioni 10.3 kila mwaka kwa ajili ya fidia za kulipia ada wanafunzi hawa, tunaipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu imeongezwa sana na sasa imefika asilimia 14.7. Ilitoka bilioni 570 na sasa imefika bilioni 654. Jamani hilo ni jambo kubwa sana la kuipongeza Serikali yetu. Fedha za kujikimu wanafunzi wa elimu ya juu zimetoka kuanzia shilingi 8,500 hadi kufikia 10,000 hii ni hatua kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Serikali, lakini bado sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto na mahitaji mengi. Niende kwenye changamoto chache. Leo kutokana na ongezeko kubwa la udahili wa wanafunzi wanaoendelea katika ngazi zote, mfano kidato cha kwanza, udahili umeongezeka kutoka wanafunzi 780,376 kwa mwaka 2021 hadi kufikia wanafunzi 173,941 kwa mwaka 2023. Hili ni ongezeko la asilimia 38. Kwa ongezeko hili tunakuwa tunahitaji miundombinu ya madarasa na walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto hii ya miundombinu na walimu, nianze na changamoto ya miundombinu. Miongozo inaelekeza kwamba darasa moja liwe na wanafunzi 45, lakini kwa sasa darasa moja lina wanafunzi 74 kwa shule za msingi. Kwa shule za awali mwongozo unasema darasa moja liwe na wanafunzi 40, lakini kwa sasa darasa moja lina wanafunzi 75.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kutokana na takwimu za BEST, kitabu hiki cha takwimu za elimu ambacho kinatolewa na Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI. Tunaona kwa uwiano huu tukisema mwalimu amfikie kila mwanafunzi mmoja mmoja, anawezaje kumfikia mwanafunzi mmoja mmoja katika msongamano mkubwa kama huu? Kwa hiyo tunaona ni namna gani elimu yetu haitafikia kile kiwango tunachohitaji kwa sababu huku kwenye msingi ndiko tunakoenda kukuza elimu ya wanafunzi ili waweze kufanya vizuri katika ngazi za juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali hiyo inafanya shule za msingi kuwa na uhaba mkubwa sana wa madarasa. Na kwa sasa tuna uhaba wa madarasa takribani vyumba 102,485, ni uhaba mkubwa sana. Changamoto hii inasumbua sana katika ufundishaji na kwa utafiti uliofanyika inaonekana kuna vyumba ambavyo wanafunzi wanakaa hata zaidi ya 100 kwenye chumba kimoja. Kwa hiyo tuangalie namna ya kuweza kurekebisha changamoto hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye changamoto ya pili ambayo ni walimu; kwa mujibu wa Hotuba ya Bajeti ya TAMISEMI ya mwaka huu, shule za msingi zina uhaba wa walimu 100,958 na shule za sekondari zina uhaba wa walimu 74,743. Pamoja na TAMISEMI kupata kibali cha kuajiri walimu 13,130, bado uhaba wa walimu utaendelea kubaki kwa sasa tutakuwa na uhaba wa walimu wa takribani 162,551.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiendelea kuajiri kwa utaratibu huu itatuchukua miaka 10 mpaka 15 kuweza kutatua changamoto hii ya walimu. Nasema hivyo kwa sababu wakati Serikali inaajiri kuna walimu wanastaafu na kuna walimu wanaofariki, lakini pamoja na hao wanafunzi bado wanaendelea kudahiliwa kwa hiyo ongezeko la wanafunzi linaendelea kuwa kubwa na wakati changamoto ya walimu ikiendelea kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sensa yetu ya 2012, Watanzania walikuwa milioni 44 na sasa ni milioni 61. Inaonekana hapo katika hiyo miaka kumi hao watu waliozaliwa ni watoto na wanahitaji elimu, sasa tusipotengeneza miundombinu mapema ukifika wakati huo tutapata changamoto, wanasema ukitaka kuliua Taifa uue elimu, kwa hiyo sisi tunataka kuboresha kwenye elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwenye jambo hili, ninaishauri Serikali iweze kuongeza bajeti ya elimu kwa asilimia 20. Kuna Azimio la Incheon la Mwaka 2015 ambalo lilizitaka nchi zote zilizo Ukanda wa Kusini mwa Jangawa na Sahara ziweze kutenga asilimia 20 ya bajeti yote ya Taifa kwenda kwenye sekta ya elimu ili kuweza kukabiliana na changamoto kama hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali itaweza kutoka hapa kwenye asilimia 18 tunayotenga sasa tukaenda kwenye asilimia 20, tunaweza kutatua changamoto hizi ambazo ni za miundombinu na walimu tukaweza kuajiri walimu wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninaishauri Serikali iangalie itakuja na mpango gani mahsusi wa kuweza kuajiri walimu kuendana na ongezeko. Tumeona ongezeko la watoto na upungufu wa walimu. Kwa hiyo, ninashauri Serikali ije na mpango wa miaka mitano, mitano wa kuona katika kipindi cha miaka tunaangalia uhaba wa walimu tulionao tunaugawanya kwa hiyo miaka mitano, tunaona ni namna gani tunaweza kuajiri walimu, hata tukiajiri kila mwaka walimu 25,000 tutakuwa tumepunguza sana tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongeze pale alipokuwa amechangia Mheshimiwa Shangazi. Leo sekta ya elimu inasaidiana sana na wadau hawa wenye shule binafsi, kwa sababu nia yetu ni moja kuweza kuendeleza wanafunzi au Watanzania kupata elimu bora. Sasa inapoonekana upande huu wa wadau wa elimu na Serikali wanakinzana inaonekana kama kuna namna fulani ambayo hawaendi pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo ambayo yanafanyika ambayo siyo mazuri, wawekwe pamoja wazungumze, watatue hizo changamoto.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Malleko kwa mchango mzuri.

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba dakika moja tu nimalizie.

NAIBU SPIKA: Sekunde mbili.

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kuna mbunifu anaitwa Mataka, ameweza kubuni namna gani ya kufanya ufundishaji wa Hisabati, Kiswahili pamoja na Kiingereza…

NAIBU SPIKA: Ahsante, mengine andika.