Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi ya kutoa mchango wangu katika Wizara hii muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Nianze kwa pongezi, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na kubwa ambayo anaifanya hasa katika eneo la kuboresha miundombinu ya elimu; elimu msingi, elimu secondary, lakini pia na katika ngazi ya vyuo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameelekeza pesa zile za UVIKO takribani shilingi bilioni 300 kwa mkupuo mmoja kwenda katika Sekta ya Elimu ambazo zimekwenda kujenga madarasa takribani 13,000 nchi nzima na sasa tumeweza kuona tija kubwa ya elimu, hasa katika eneo la miundombinu. Hii ni historia, ni lazima tuiseme bila kificho, kwa sababu, katika uhai wa Taifa letu hakuna uwekezaji mkubwa kwa wakati mmoja katika Sekta ya Elimu ambao umefanyika kuliko kipindi hiki cha miaka miwili ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nimpongeze pia, Waziri mwenye dhamana hii ya Sekta ya Elimu, kaka yangu, mtani wangu, Mheshimiwa Profesa Mkenda pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Kipanga, lakini na watumishi wote wa Wizara hii ya Elimu kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya. Kipekee niwapongeze kwa rasimu ile ya Sera ya Elimu, ni rasimu ambayo imekuja wakati muafaka na wakati sahihi. Niwaombe sana sasa waendelee kuchukua na kupata maboresho kutoka kwa wadau mbalimbali ili tuboreshe jambo letu hili liweze kuwa na tija ambayo tunaikusudia, lakini ambayo itakuwa ya muda mrefu zaidi katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niwapongeze Kamati, wamefanya kazi nzuri, wasilisho zuri. Kwa hiyo, kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuchangia katika eneo ambalo Kamati imelitaja kama changamoto. Eneo ambalo kuna mgongano wa wazi kati ya taasisi mbili za Serikali, Wizara mbili; Wizara ya Elimu ambayo kimsingi inasimamia sera, lakini kuna Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambayo yenyewe inasimamia utekelezaji wa elimu katika Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hawa wawili kuna wakati wanatoa maelekezo ambayo yanawachanganya, hasa sekta binafsi. Kwa bahati mbaya sana sekta binafsi haina chombo ambacho inakisimamia, hakuna Wizara mahususi ambayo inaisimamia sekta binafsi ya utoaji wa elimu. Hawa kama Wizara wanasimamia eneo la sera peke yake, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wanasimamia shule, lakini wanasimamia shule zinazomilikiwa na umma, maana yake ni kwamba, shule za sekta binafsi hazina msimamizi. Ndio maana kuna nyakati yanatoka matamko ambayo moja kwa moja yanaenda kuathiri utendaji kazi wa shule hizi za binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe kwamba, kama ambavyo pia Kamati imeshauri, ni vizuri Serikali ikatengeneza chombo ambacho kitakuwa kinasimamia Sekta ya Elimu msingi na sekondari, kwa maana kama Tanzania Education Sector Authority, ili iweze kuchukua wajibu kama wa TCU katika ngazi ya vyuo vikuu kwa sababu TCU wanasimamia vyuo vikuu vyote vya binafsi na vile vya umma, lakini ukija katika vyuo vya kati kwa maana ya vinavyotoa certificate na diploma ambapo kuna NECTA VETA pale, nayo inasimamia eneo la vyuo binafsi, lakini na vyuo vya umma. Kwa hiyo, hii itasaidia sana katika kuondoa huu mgongamo ambao upo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo ambalo linafanyika, si jema sana kwenye sekta ya binafsi. Kuna tozo karibu 17 ambazo zinatozwa katika sekta binafsi. Kwa kweli, tunawanyanyasa kwa sababu, hawa ni watoa huduma, lakini sisi tunawachukulia zaidi kama wafanyabiashara. Kwa nini nasema ni watoa huduma? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ukiangalia wanafunzi walioko katika shule za binafsi kuanzia awali mpaka sekondari ni takribani wanafunzi 860,000. Maana yake ni kwamba, shule hizi zisingekuwepo Serikali ilikuwa ina wajibu wa kuhakikisha kwamba, watoto hawa wanakuwa na miundombinu, wanakuwa na Walimu, wanakuwa na capitation, wanakuwa na kila kitu ili waweze kupata elimu, lakini watoto hawa wakimaliza elimu huko wanakosoma, wanakuja kuajiriwa katika Taifa hili ambalo pia, watatoa mchango wao. Sasa ni kwa nini sisi bado tunaichukulia sekta ya binafsi ya elimu kama biashara, badala ya kuichukulia kama wasaidizi na watoa huduma? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo napenda kushauri kwamba tozo hizi 17 kama ambavyo tumeweza kupunguza tozo kwenye kilimo, tumepunguza tozo kwenye mazao mbalimbali na sasa tutazame tozo hizi katika sekta ya elimu, tukianza na service levy ambayo kwanza inakinzana hata na Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa. Hili ni jambo la muhimu sana la kulitazama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ukilitazama hapa utaona kwamba sekta binafsi ina mchango mkubwa katika eneo hili ni idadi ya walimu ambao wameajiriwa na sekta binafsi. Takribani walimu 55,000 hii ni idadi kubwa sana. Na hawa huko walipo wanalipa kodi za Serikali na wanasaidia sasa eneo zima hili la kutoa elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba zisingekuwepo hizi hawa nao ilikuwa ni tatizo ambalo Serikali ilibidi iwatafutie ajira. Kwa hiyo, hili ni jambo muhimu sana, kuwatazama sekta binafsi kama watoa huduma na tusiwatazame kama wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ninataka kulisema ni hili la udhibiti ubora ambalo limezungumzwa, ni jambo ambalo kwa kweli inabidi tutafute chombo ambacho ni huru zaidi kama CAG fulani hivi wa upande wa elimu, ili atoke katika ofisi ambayo haina hata mgongano wa kimaslahi na hawa anaokwenda kuwasimamia. Hii itaongeza tija kubwa sana katika elimu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ni kikwazo, naliona sasa limekuwa kama ni fashion, kuna wakati tunazungumza suala la elimu bila malipo ama elimu bure ambapo Serikali inaweka ruzuku pale. Lakini sasa kuna utitiri wa mitihani ambayo inafanyika, kuna mtihani wa Kijiji, mtihani wa Kata, mtihani wa ujirani mwema, wa Jimbo, yote hii inakwenda kwa mzazi. Kwa hiyo, mzazi huyuhuyu aliyeondolewa mzigo wa michango huku anajikuta sasa anachangia mitihani ambayo imekuwa mingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatukatai, mitihani ni kipimo, lakini hawa walimu nao ambao kila siku wako katika hatua mbalimbali za kuandaa mitihani, mitihani yenyewe inatakiwa ichapwe, inatakiwa isimamiwe, inatakiwa isahihishwe, wanapoteza muda mrefu wa kufundisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wote tumesoma katika hizi shule. Huko zamani hakukuwa na utitiri huu wa kupima mitihani ambayo ni mingi kiasi hiki. Kwa hiyo, ninadhani kwamba ni busara sana tuangalie eneo hili vizuri kuona kama kuna tija ya huu utitiri wa mitihani. Kwa sababu pia unachukua muda mrefu sana kuanzia kuandaa, kusimamia, kusahihisha na mambo mengine. Kwa hiyo kwa maoni yangu, nadhani inapunguza muda wa kufundisha na ndiyo maana sasa watoto wetu wakati mwingine labda wanakuwa ni wa matokeo zaidi kuliko wa hali halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ninalotaka kulichangia ni suala la sekta binafsi kama ambavyo nimetangulia kusema na usimamizi mzima wa sekta hiyo, na hasa yale maeneo ambayo bado tunayaona kwamba hayana chombo kinachosimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni ilitokea sintofahamu ya mabasi yanayosafirisha watoto, hasa katika shule binafsi kwa sababu ndiyo zenye utaratibu huo, lakini yakatoka matamko kutoka kwa Kamishna wa Elimu na kwingineko, kitu ambacho kwa kweli siyo sawa, ni lazima hawa wadau wakae kwa pamoja waweze kutafuta suluhisho la pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yangu ni nini, maana yangu ni kwamba sasa hivi tukitazama, kwa mfano watoto wanaokuwa bweni wameambiwa waanzie angalau darasa la tano ni jambo jema, lakini lazima watu wakae kwa pamoja tutazame hizi changamoto vizuri ili tupate suluhisho la pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mabasi tusitake kuaminishwa kwamba wanaume ndiyo watu ambao hawafai katika jamii, kwamba akifanya kosa mwanaume mmoja basi wanaadhibiwa wanaume wote, kwamba sasa kwenye basi awepo mhudumu wa kike na wa kiume, lakini tunajua kabisa mmomonyoko wa maadili umeigusa jamii yote, wake kwa waume.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)