Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha siku ya leo lakini kipekee nimshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya. Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wote ni mashahidi Bajeti ya Wizara ya Afya mwaka jana Fungu 52 ilikuwa shilingi trilioni 1.1 mwaka huu tunaomba mtupitishie shilingi trilioni 1.2 kuna ongezeko la shilingi bilioni 100.

Mheshimiwa Spika, bajeti ya Sekta ya Afya, ukiangalia fedha zilizotengwa kwenye Wizara ya Afya na fedha za TAMISEMI, bajeti ya Sekta ya Afya imeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.1 mwaka jana hadi shilingi trilioni 2.4. Hii inaonyesha dhamira ya dhati kabisa ya Rais Samia ya kuboresha huduma za afya nchini.

Mheshimiwa Spika, natambua kamati imezungumzia maazimio ya viongozi wakuu wa nchi waliyokutana Abuja ya kwamba nchi zinapaswa kutenga asilimia 15 ya fedha zao za bajeti kwa ajili ya afya. Lakini Wabunge naomba tushukuru angalau tunaona ongezeko la fedha za afya kila mwaka. Kwenye hili tutaendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia. Amezungumza Naibu Waziri wangu mafanikio ambayo tumeyapata, majengo yapo kila sehemu, zahanati, vituo vya afya, hospitali za halmashauri tunazungumzia vifaa tiba vya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka miwili iliyopita tulikuwa na CT– Scan 13 tu. Leo tuna CT–Scan 45 ndani ya Rais Samia Suluhu Hassan. Ndugu zangu wa Kigoma leo wana huduma ya CT- Scan, Katavi wana huduma ya CT–Scan, Manyara, Simanjiro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwako Mbeya ninahaidi itakapofika tarehe 30, Juni tutakuwa tumekamilisha MRI na CT–Scan lakini kwenye suala la MRI hajapata tokea. Tulikuwa tuna MRI moja tu Hospitali ya Taifa Muhimbili leo chini ya Rais Dkt. Samia miaka miwili tumefunga MRI Chato, tumefunga MRI Mtwara na tutakamilisha ufungaji wa MRI Mbeya, huyu ndiyo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, maneno machache vitendo vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu hii miaka miwili iliyopita tukipata wagonjwa mahututi tutawalaza wagonjwa 258 tu. Leo watokee wagonjwa mahututi tuna uwezo wa kulaza wagonjwa 1000 kwa wakati mmoja, huyu ndiye Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumetambua huduma za magonjwa ya dharula (Emergency Medical Department). Mwaka jana 2022 tulikuwa na majengo nane, miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan tuna majengo ya EMD 118, tena yameshuka mpaka katika ngazi za halmashauri. Zamani EMD unaiona Muhimbili, unaiona KCMC unaiona Bugando leo mpaka kijijini kule hospitali ya halmashauri unakuta huduma ya EMD. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa huduma za kina mama wajawazito tumeweza kuboresha huduma sasa hivi asilimia 98 ya kinamama wajawazito wana imani na huduma zinazotolewa na wanaudhuria kliniki. Hii imetuwezesha kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya mwaka mmoja kutoka vifo 43 hadi vifo 33 katika kila vizazi hai 100. Lakini vifo vya watoto watano chini ya miaka mitano tumevipunguza kutoka vifo 67 hadi vifo 43. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali ya sekta ya afya duniani inapimwa kwa viashiria hivi. Ikiwemo vifo vya watoto lakini kubwa Tanzania na Dunia ya Kimataifa tulijiwekea malengo, inapofika 2025 watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wajue hali zao. Leo Tanzania tumefikia asilimia 94.4 kabla ya 2025.

Mheshimiwa Spika, tulipaswa kuweka asilimia 95 ya wenye UKIMWI wanaotumia dawa, wawe wapo kwenye dawa tumeishafika asilimia 95 kabla ya 2025. Lakini habari njema, wanaotumia dawa za kufubaza virusi za UKIMWI asilimia 96 maambukizi ya UKIMWI yamegandamizwa au virusi vya UKIMWI vimepunguzwa nguvu, haya ni mafanikio makubwa chini ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nikushukuru sana kwa jinsi unavyoongoza Bunge letu Tukufu pamoja na kusimamia mijadala ndani ya Bunge. Wewe ni icon, wewe ni inspiration kwa wasichana na vijana Tanzania kwamba tunaweza kuwa na wanawake wakafanya kazi kubwa na nzuri kama Dkt. Tulia Ackson hongera sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee niwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hoja yetu pamoja na kamati. Kamati yetu madhubuti inayoongozwa na Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo Mbunge wa Maswa Mashariki ambaye imesomwa na Mheshimiwa Cecil Mwambe, tumepokea maoni na ushauri wa kamati. Tunawaponeza sana kamati kwa ushauri wenu mzuri lakini kipekee tunawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na ushauri kubwa. Kubwa, tutatekeleza maoni naushauri ambao mmetupatia kwa sababu una lengo la kuboresha huduma za afya kwa watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tumefarijika sana kupokea pongezi kutoka kwenu Waheshimiwa Wabunge, pongezi hizi tunazichukulia kama deni letu na watendaji wangu kwenu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wa kufanya kazi zaidi usiku na mchana ili tuweze kuimarisha na kuboresha huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge, napenda nitambue Waheshimiwa Wabunge waliyochangia hoja yangu. Wapo Wabunge 47 akiwemo na Naibu Waziri, Wabunge 44 wamechangia kwa kuongea na Wabunge watatu wamechangia kwa maandishi. Kwa sababu ya muda naomba nisiwataje.

Mheshimiwa Spika, hoja kubwa ambazo zimetolewa ziko kama hoja tisa nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutoa ufafanuzi. Nitajikita katika hoja nane na kama muda utatosha nitazungumzia hoja ndogo ndogo, moja moja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge hoja kubwa ambayo wameileta pamoja na kamati ni Serikali kuwekeza nguvu zaidi katika huduma za kinga badala ya huduma za tiba. Waheshimiwa Wabunge hoja hii tumeipokea na ndiyo maana katika bajeti yangu kipaumbele cha kwanza maana ya huduma za kinga, huduma ya kwanza ya kinga ni chanjo za watoto zinazoweza kuzuia magonjwa. Tumetenga bilioni 114.3 kwa ajii ya kuhakikisha tunatoa chanjo zote za Watoto. Tutanunua pia ma–fridge, majokofu kama 1,600 na tutatumiwa magari ya chanjo 102 na kuyasambaza katika halmashauri zenu ili yaweze kuhudumia suala la chanjo.

Mheshimiwa Spika, chanjo ya pili ambayo tutaipa kipaumbele ni chanjo ya kuwakinga wasichana dhidi ya saratini ya mlango wa kizazi. Waheshimiwa Wabunge, naomba mkawe mabalozi, chanjo hii ni salama, chanjo hii haimzuii msichana kuja kupata mtoto, kuja kupata ujauzito sana sana inamzuia kutokuja kupata maambukizi ya ugonjwa wa saratani.

Mheshimiwa Spika, turuhusu tuje tufanye semina Bunge lako tuonyeshe aina za saratani zinazoongoza kwa watanzania ya kwanza ni sarati ya mlango wa kizazi. Kwa teknolojia hii haikubaliki kuendelea kuwa na kizazi cha wasichana wenye saratani ya mlango wa kikazi. Niwaombe sana wazazi na walezi wenzangu wenye watoto wa umri wa chini ya miaka 14 tuwapatie chanjo ya saratani ya mlango wa kikazi chanjo hii inatolewa bure bila malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia eneo la pili la kinga ni suala la lishe, tutaendelea kuwasaidia wazalishaji wadogo wa chakula, tutawapatia vinu 300 vya kuongeza virutubisho na kutoa matone ya vitamini A kwa watoto wenye umri ya chini ya miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, tumeona pia kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, viwanda vinavyozalisha unga wa ngano, viwanda vinavyozalisha unga wa mahindi, viwanda vinavyotengeneza mafuta ya kula wanapaswa kuongeza virutubisho katika product zao. Kwa hiyo, tutashirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha viwanda vyote Tanzania vinafanya food fortifications ili tuweze kuimarisha kiwango cha lishe kwa watanzania.

Mheshimiwa Spika, eneo jipya ambalo tunakuja nalo katika suala hili la kinga ni kuimarisha kada ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii (Community Healthy Workers). Wamekuwepo hawa watu, mradi wa UKIMWI ana–train wahudumu wa afya ngazi ya jamii siku mbili, watu wa malaria ana–train wahudumu wake wa afya siku tatu, mtu wa kifua kikuu kila mtu anawahudumu wa afya ngazi ya jamii.

Mheshimiwa Spika, tumeona ipo haja ya kuja na mfumo mmoja wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii integrated and coordinated community health workers program hawa wahudumu wa afya ngazi ya jamii tutaanza nao elfu tano na Waheshimiwa Wabunge watachaguliwa katika vijiji vyenu na mitaa yenu. Tutazielekeza Serikali za vijiji ndiyo wawachague, tutawapa mafunzo ya miezi sita na tumeamua tujikite katika maeneo makubwa sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ya kwanza ni afya ya uzazi mama na mtoto, eneo la pili litakuwa lishe, eneo la tatu afya na usafi wa mazingira, eneo la nne magonjwa ya kuambukiza hususani malaria, kifua kikuu na ukimwi na eneo la tano magonjwa yasiyo ya kuambukiza hususani ni kisukari, shinikizo la juu la damu na magonjwa ya moyo na eneo la sita ni magonjwa haya ya mlipuko kama Ebola na Marburg.

Mheshimiwa Spika, tunaamini kabisa ameongea Mheshimiwa Oliver pale, tulipata mlipuko wa Marburg kule Goziba kuna watumishi wa afya wawili tu. Ukiweka wahudumu wa afya kila kijiji wawili, watatu wale ndiyo watakuwa jeshi la kwanza la afya la kuwafikia wananchi kutoa huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, nimepokea concern kuna wahudumu wa afya ngazi ya jamii waliyopo, waliosoma siku mbili, wiki moja, wiki tatu hatutawaondoa tutawa–phase out kidogo kidogo. Kwa hiyo, hii niwatoe wasiwasi kwa hawa tuna–train, tutawalipia lakini hawa wataendelea lakini baada ya muda tutawaondoa kidogo kidogo.

Mheshimiwa Spika, eneo la nne kwa upande wa kinga ni suala ya afya mazingira. Tutaanzisha kampeni ya usafi wangu mita tano, mita tano usafi wangu lakini pia tunafikisha miaka 50 ya kampeni ya mtu ni afya iliyoanzishwa na Rais wetu Julius Kambarge Nyerere. Katika kufanikisha huduma za afya, mazingira tutawabana sana Serikali za mitaa watekeleze sheria ndogo zinazosimamia usafi na afya mazingira.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni ubora wa huduma, Wabunge wengi hapa wamesema mmejenga majengo, mmeleta vifaa tiba lakini huduma siyo nzuri. Tunakubaliana na Waheshimiwa Wabunge, kwamba uwekezaji mkubwa uliyofanywa na Serikali katika eneo la miundombinu, vifaa vya uchunguzi na vifaa tiba pamoja na kuajiri watumishi lakini bado kuna baadhi ya hospitali zetu hazitoi huduma bora.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge tumebaini kuwa changamoto kubwa ni uongozi. Jana nilitoa mfano wa Hospitali ya Muhimbili chini ya Profesa Janabi, ni uongozi. Kwa hiyo tunakuja na programu ya mabadiliko ya kiutendaji kwa wasimamizi wa utoaji wa huduma za afya (Leadership for Health Transaformation Program) ili kuwaongezea uwajibikaji, ufanisi na tija katika utoaji wa huduma za afya. Lakini tutaimarisha utawala bora, uongozi na menejimenti za usimamizi za hospitali, kwa kushirikisha kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mikoa. Lakini tutafanya kaguzi za mara kwa mara na za kushtukiza ili kuimarisha usimamizi shirikishi katika vituo vya kutoa huduma za afya. Vile vile tutaendelea kushirikiana na mabaraza ya kitaaluma kuhakikisha wanataaluma wao wanatoa huduma bora za afya.

Mheshimiwa Spika, tumeanzisha pia kwenye mitaala ya vyuo vya afya somo la customer care. Kwa hiyo shule na vyuo vyetu vya afya pia vitafundisha masuala ya good customer care, matumizi ya lugha ya staha na faraja kwa magonjwa, ili wanaomaliza pia wasiwe tu wanatibu lakini pia wafanye huduma kwa kutumia lugha nzuri.

Mheshimiwa Spika, suala la rasilimali watu katika sekta ya afya, uhaba wa watumishi limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge zaidi ya kumi. Sisi tumeendelea kuajiri watumishi takribani 100,000. Sekta ya afya inahitaji watumishi takribani 219,000 na waliopo ni kama 109,616. Sambamba na kuomba vibali utumishi sisi wenyewe kama sekta ya afya tumejiongeza kwa hospitali zetu kupitia mapato yao ya ndani kuajiri wataalamu wa afya takribani 4,189 ambao wameajiriwa kwa mikataba. Lakini pia kuanzia mwaka jana nimewataka wadau wote wa maendeleo wanaotekeleza miradi ya afya nchini, kutumia angalau asilimia 10 ya fedha zao kuajiri watumishi wa afya. Badala ya mradi malaria sijui malaria kila baada ya dakika moja kwenye redio na Tv, tunakata asilimia 10 ya fedha za miradi zinakwenda kuajiri watumishi wa afya na tutawapeleka katika maeneo ambayo yana uhaba. Lakini pia tutatoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ya wataalamu wa afya, hususani madaktari bingwa na bobezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumetangaza juzi ajira za madaktari bingwa 30. Mpaka tunafunga muda tumepokea maombi ya madaktari bingwa 12 tu. Kwa hiyo madaktari bingwa wengi wanapenda kufanya kazi katika sekta binafsi. Tulichokiona, sera inataka tusomeshe madaktari bingwa walioajiriwa na Serikali, inatutaka tusomeshe watumishi walioajiriwa na Serikali; lakini tumeangalia katika hospitali zetu kuna watumishi wanaojitolea zaidi ya miaka miwili hadi miaka mitatu. Kwa hiyo hao tutawapeleka kusomea udaktari bingwa na tutawapa mikataba ya kufanya kazi katika hospitali husika angalau kwa muda wa miaka minne ndipo wanaweza Kwenda kwenye hospitali binafsi. Suala hili pia nadhani uliligusia wakati wa maswali na majibu.

Mheshimiwa Spika, eneo jingine ni kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Tutaendelea kutoa elimu kwa jamiii kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza, tutafanya utafiti. Mwaka huu tunafanya utafiti wa kitaifa; na kwa upande wa elimu ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge naomba niwahamasishe, mambo manne tu ukiyazingatia. Ya kwanza, mazoezi angalau zisipungue dakika 30 kwa siku, moyo uende mbio na utoke jasho. Pili, punguzeni matumizi ya chumvi kupita kiasi. Tatu, punguzeni matumizi ya sukari na unaweza kuishi bila kula sukari; kama ulikuwa unatumia vijiko vitatu tumia kijiko kimoja. Vilevile eneo la nne ni kupunguza mafuta na sisi Wizara ya afya tumepeleka maombi kwa Wizara ya fedha kuangalia jinsi gani wanaweza kuongeza ushuru kwenye bidhaa hizi ili tupunguze matumizi ya bidhaa zinazosababisha magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza. Tutajikita kwenye magonjwa matatu; kisukari, shinikizo la damu pamoja na magonjwa ya moyo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza pia tumeshusha huduma hizi tumeanzisha kliniki katika ngazi za msingi, lakini pia tutaanzisha vituo 100 vya uchunguzi wa saratani katika ngazi ya msingi.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la huduma za utengamao (rehabilitative services). Asubuhi hapa nimemtambulisha mwanangu Lukiza. Lukiza sijui kama unanisikia Lukiza. Nadhani mnamuona ndivyo yuko hivyo. Lukiza amezaliwa na tatizo la autism, usonji. Lukiza alikuwa hawezi kuvaa nguo, hawezi kula, hawezi kupiga mswaki, hawezi kufanya chochote. Mama yake Hilda amehangaika na mtoto. Lakini kwa sababau ya huduma za utengamao ikiwemo huduma za mazoezi tiba, huduma za kazi (occupational therapy), huduma za speech, Lukiza anaweza kujivalisha nguo zake mwenyewe leo, Lukiza anaweza kula leo, Lukiza ametulia pale ameingia saa kumi, Lukiza hajafanya fujo yoyote kwa sababu amefundishwa jinsi ya kufanya utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala hili limenigusa kama mama. Ukienda kwenye vituo vya watoto wenye ulemavu asilimia 99.5 wanapelekwa na akina mama wenzangu. Sisi kama Serikali tumeamua kuimarisha huduma za utengamao kwa watoto lakini pia tunaboresha huduma hizi kwa sababu umri wa kuishi pia unaongezeka wazee nao wanakua. Lakini pia ajali zimeongezeka, Profesa Ndakidemi umesema hapa mtu amekatwa mguu, amekatwa mkono, huduma za utengamao ndio zinamsaidia mtu tuishi maisha bora (quality life). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile pia tutaangalia watoto wenye autism, tutaangalia watoto wenye mtindio wa ubongo, watoto wenye udumavu wa akili, watoto wenye mongolia, watoto wenye ukosefu wa utulivu. Waheshimiwa wabunge anaweza akazaliwa mtoto ana ukosefu wa utulivu akapewa masaa mawili atunge ushanga, miaka miwili mtoto yule anabadilika anakuwa na utulivu. Kwa hiyo eneo hili ni eneo ambalo tutalipa kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, na kipekee nimpongeze sana Hilda Nkabe kama mama, akaanzisha taasisi ya Lukiza Autism Foundation ili kuongeza elimu na hamasa ya watoto wenye usonji. Lengo la Hilda ametaka wanawake wenzake wasiwafiche watoto wenye usonji na watoto wenye ulemavu. Ndiyo maana kila mwaka tunafanya mbio (Run for Autism) ili kuongeza hamasa kuwaonesha kwamba watoto hawa wanawezekana.

Mheshimiwa Spika, nipongeze wataalamu wetu. Tunaye Doctor ambaye amekuja hapa mtaalamu wa Physiotherapy, Godfrey Kibati, ambaye anafanya masuala la Occupational Therapy. Tutashirikiana naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona mpaka twende Muhimbili hawa madaktari wakasome miaka mitano hatutafika. Kwa hiyo tutaanzisha kozi za miezi sita mpaka tisa za muda mfupi. Tuchukue wauguzi labda wawili kutoka kila hospitali au kila halmashauri, madaktari wawili kutoka kila hospitali kila halmashauri tuwapeleke wasome angalau kozi hizi tatu za masuala la tiba utengamao.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tumesema, kwamba lazima tufanye assessment. Tiba hizi za utengamao zinapatikana wapi? Kwa hiyo tutafanya assessment kujua vituo vyote ambavyo vinafanya huduma hii, ikiwemo kuimarisha huduma za matibabu. Lakini pia kuna suala la afya ya akili na namna ya kukabiliana nalo. Tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kuona umuhimu wa Serikali kuwekeza kwa kuibeba ajenda hii ya afya ya akili. Afya ya akili ndio msingi wa afya ya binadamu. Hakuna afya bila afya ya akili, na ndio uchumi wa mtu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwenye hili, kama ilivyo kwenye huduma za utengamao, hatuna wataalamu wa kutosha. Tunafurahi wenzetu wa Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS) mwaka huu wataanzisha kozi ya Clinical Psychology, angalau, na mimi nimewaambia, sisi Serikali tuko tayari kugharamia wanafunzi 10 watakaofanya degree ya kwanza ya Clinical Psychology ili tuweze kuwapata na kuwasajili katika maeneo mbalimbali. Lakini tunatoa elimu kwa umma kuhusu vihatarishi vya afya ya akili na namna ya kukabiliana nayo. Tutahakikisha pia kwamba tunakuwa na wataalamu wa muda mfupi, maana tukisubiri wamalize miaka mitano tutakuwa tumechelewa sana. Kwa hiyo hii pia tutaifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tumeamua kuipandisha hadhi Hospitali ya Taifa ya Akili Mirembe, itakuwa ni Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili. Tunawataka Mirembe wafanye promotional activities, wafanye tiba, wafanye mafunzo na wafanye tafiti. Kwa hiyo tutawapa maeneo makuu manne. Vilevile pia tumesema tutaanza na huduma za afya ya akili katika hospitali kumi za rufaa za mikoa na hospitali za halmashauri.

Mheshimiwa Spika, kuhusu umuhimu wa kuanzisha huduma ya kisaikolojia Balozi dada yangu Jesca Msambatavangu ameiongea vizuri. Tunawaaalika sekta binafsi; Ulaya, Marekani, India hii ni biashara kubwa. Yoga masuala ya rehabilitation, masuala ya breathing technique, kama kuna mtu kuna msitu mzuri akaanzishe watu waende siku mbili wakaondoe ma-stress ya Bungeni, muondoe ma- stress ya familia nyumbani, baba amekuchukiza, jamani Watanzania tengeni muda wa ku-refresh, otherwise mtapata changamoto nyingi. Kwa hiyo suala hili tutaendelea kuliboresha.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, kwa kweli tunakwenda vizuri. Lakini jambo moja ambalo limezungumzwa na Wabunge wenzangu wananwake, wameniuliza, Mheshimiwa Waziri, hebu tuambieni sasa sera ya huduma hizi ni bure au siyo bure? Nimefanya uchambuzi na timu yangu, tukaangalia, Mheshimiwa Waziri wa fedha yupo. Tukaangalia mama anatakiwa kwenda kliniki angalau mara tano wakati wa ujauzito. Hudhurio la kwanza ni shilingi 2,397. Hudhurio la pili shilingi 15,187. Hudhurio la tatu 2,397. Hudhurio la nne 1,727. Hudhurio la tano ni 2,397. Kwa hiyo kwa mahudhurio matano mwanamke mjamzito gharama ni shilingi 24,103. Tumeondoa umeme, tumeondoa mzani, tumeondoa dawa ambazo zinanuliwa na Serikali, hizi ni zile re-agent kufanya nini kwa mfano, Hb, kupima wingi wa damu, protini, kupima mkojo pamoja na kupima blood glucose. Tuna wanawake takribani milioni mbili kila mwaka, kwa hiyo ni 48,000,000,000.

Mheshimiwa Spika, tukienda kwenye huduma za kujifungua kawaida, tumefuta vitu vidogo vidogo vingine vyote, tumepata ni 32,952. Wanawake 1,600,000 ndio wanajifungua kawaida, kwa hiyo inakuwa kama 52,000,000. Wanaojifungua kwa upasuaji gharama ni 63,000; kwa hiyo hapa inakuja bilioni 119. Hivyo, kama tunataka kutoa huduma bora kwa wanawake wajawazito Waheshimiwa Wabunge ni bilioni 119, hatujaweka umeme, hatujaweka maji, hatujaweka vifaa, hatujaweka CT-scan, hatujaweka X- Ray mashine, hatujaweka ultrasound. Kwa hiyo tunaongea na wenzetu wa Wizara ya fedha, kwamba hebu watuangalie huko mbeleni kama kuna elimu bure basi na hili sasa liende badala likabaki kwenye makaratasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hiyo ndiyo gharama ambayo tumeipata. Lakini niendelee kusisitiza kwa watoa huduma za afya. Kuna dawa tunazinunua bure, nataka wajawazito wapewe bure. Kuna vitu tunavinunulia bure, tunataka wajawazito wapewe bure.

Mheshimiwa Spika kuna suala la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Kabla sijazungumza hili niende kwenye kuimarisha huduma za ubingwa bobezi. Kwenye hili kwa kweli tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kutambua mchango wa wataalamu wetu. Lakini kipekee tunamshukuru Rais Samia, tumetenga safari hii bilioni 23, amesema Naibu Waziri. Kupeleka mgonjwa wa figo nje ya nchi ilikuwa milioni 120 lakini ndani ya nchi milioni 30. Uroto nje ya nchi milioni 250 na ndani ya nchi ni milioni 58 mpaka 70. Kwa hio ilikuwa ni kukosea niliposema bilioni kwa hiyo ni milioni 58.

Mheshimiwa Spika, tulikaa na wenzetu wa Wizara ya Fedha, tukampelea Mheshimiwa Rais maombi yetu. Kama mgonjwa huyu mtoto wa sickle cell anaweza kupona kwa milioni 58 kama tulikuwa tunapeleka wagonjwa hawa nje ya nchi kwa nini tiusitenge fedha ya ndani ya kuwasaidia wasio na uwezo kupata huduma hizo. Tunamshukuru Rais Samia, na ndiyo maana bajeti yetu ina addendum. Tumepata bilioni tano za kugharamia kupandikiza uroto kwa watoto wenye sickle cell, lakini pia tutapandikiza figo kwa watu wenye matatizo ya figo, na eneo la tatu tutapandikiza watoto vifaa vya kusaidia kusikia cochlear implants. Tutaweka vigezo, tangu jana tulivyosema nimepata maombi mengi, kwa hiyo tutaweka vigezo yupi atastahili, yupi hatastahili. Lakini kubwa Waheshimiwa Wabunge wataalamu wetu wanafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa tiba utalii, hapa ninaposema wataalamu wetu saba wameitwa Malawi ili kutoa huduma za uchunguzi wa moyo kutoka Jakaya Kikwete na wameshawachunguza wagonjwa 720, na kati yao 537 wamegundulika kuwa na matatizo ya moyo, wanakuja Tanzania kupata huduma hii. Kwa hiyo tiba utalii itakuwa inawezekana chini ya Rais Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalize hili la bima ya afya. Bima ya afya ndiyo roho ya huduma za afya nchini. Asilimia 70 ya fedha za hospitali zetu za umma na binafsi zinategemea bima ya afya. Tumefanya actuarial studies na kuona kwamba baadhi ya vifurushi vinahatarisha uhai na uendelevu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Ndugu yangu Hawa ameliongea. Hawa Toto Afya Card anachangia 50,400. Katika kila shilingi 100 wanatumia shilingi 667. Lakini la pili tumefanya uchambuzi zaidi, katika mwaka 2021 watoto waliosajiliwa Toto Afya Card walikuwa 157,920 wakachangia bilioni 5.9 wakatumia bilioni 40.5; jamani kuna bima ya afya hapo? Unachangia bilioni tano unatumia bilioni 40.

Mheshimiwa Spika, fedha zinaenda wapi? Asilimia 53 kumuona daktari. Watanzania tuna utamaduni fulani hivi. Nikishakuwa na bima ya afya kitu cha kwanza naenda kwenye polyclinic ya kumuona specialist; tukaangalia magonjwa gani haya. Ugonjwa wa kwanza ni malaria, malaria unatibiwa katika zahanati. Ugonjwa wa pili mfumo wa hewa, unatibiwa katika ngazi ya zahanati, ugonjwa wa tatu UTI. UTI inatibiwa katika ngazi ya chini. Kwa hiyo tumeangalia hela asilimia 58 za hela ya Toto Afya Card zimeenda kwenye vituo binafsi vya kutoa huduma za afya, asilimia 20 imekwenda hospitali za Serikali, asilimia 22 imekwenda katika vituo vya taasisi za dini. Kwa hiyo mtaona wenyewe hakuna uendelevu wa bima ya afya ya Toto Afya Card.

Mhesimiwa Spika, sasa, the way forward mtu-challenge, the way forward, ndiyo maana tunasema kuna vifurushi, kwamba watoto wasajiliwe Pamoja na wazazi wao. Lakini la pili watoto wasajiliwe wakiwa shuleni. Kama kuna watoto 100, kwa sababu kama shule ina watoto 100 watakaoumwa watakuwa labda 10 watasaidia 90 watalipia wenzao 10 watakaoumwa, lakini hili suala the way forward yake ni bima ya afya kwa wote. Bima ya afya ndiyo itakayotutoa.

Mheshimiwa Spika, tumefanya uwekezaji mkubwa katika huduma za afya, tumejenga ili wananchi wapate huduma bora za afya, inabidi waweze kulipia kabla ya kugua. Suala hili tunaendelea na majadiliano ndani ya Kamati, tunaamini tutaweza kufikia muafaka.

Mheshimiwa Spika, maswali mengine mojamoja ambayo ni suala la dada yangu Mheshimiwa Fatma Toufiq kuhusu Health Basket Fund ipelekwe kwenye dawa. Asilimia 33 ya hela ya Health Basket Fund inapaswa kutumika kwa ajili ya dawa, lakini tunazungumza kuijengea mtaji MSD. Hapa tunalalamika MSD haipeleki dawa, tutabadilisha watu kama hatutaipa mtaji MSD ikawa ni duka, ukishakuwa na vifaa vyako una-order unapewa. MSD sasa hivi anasubiri hela za vituo zije ndio akanunue dawa.

Mheshimiwa Spika, la pili, suala la dada yangu Mheshimiwa Munde, tumewanyang’a, kwa nini Hospitali ya Kanda imetoka Tabora imepelekwa kwingine. Hatujawanyang’anya tuliangalia vipaumbele. Tuliona Kigoma tutavutia DRC, wagonjwa wa Burundi na wagonjwa wa Rwanda, ndio maana tukaenda Kigoma, lakini nataka kuwapoza, tutajenga Hospitali ya Taifa ya Huduma za Watu Wenye Ulemavu Tabora kwa sababu, walishatenga eneo. Hilo jambo tunataka kuwaahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalize kuhusu majengo yote ambayo hayajakamilika. Tumetenga fedha na tumekubaliana ndani ya Wizara, badala ya kuanza ujenzi mpya ni vizuri tukakamilisha ujenzi wa majengo ambayo tumeyaanza.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni huduma kwa wazee. Huduma kwa wazee tumelipokea na tumeanza. Dawa za kisukari aina mbili za wazee sasahivi zitapatikana katika ngazi ya zahanati. Dawa aina tano za kisukari kwa ajili ya wazee na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, tumezishusha kutoka Hospitali ya Wilaya, sasa zitapatikana katika kituo cha afya, lakini pia tutaendelea kuimarisha.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema kwamba, tumepokea hoja za Wabunge zote na nyingine tutazijibu kwa maandishi ikiwemo upatikanaji wa ambulance, amesema vizuri Naibu Waziri wangu. Tulipokwenda Toyota basic ambulance walitupa bei ya milioni 144, tukaenda UNICEF tukapata kwa milioni 83.9, advanced ambulance, Toyota, sijui kama naharibu biashara ya mtu sijui lakini, tukapewa bei ya shilingi milioni 162, tukatumia UNICEF tumepata kwa shilingi milioni 93. Kwa hiyo, tume-save bilioni 17.8, amesema hapa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kila halmashari itapata ambulance mbili na sisi Wizara ya Afya tutaongeza ambulance moja kwa baadhi ya majimbo ambayo yana idadi kubwa ya vifo vya akinamama wajawazito na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalize tu kwa kusema, hospitali zetu hizi…

SPIKA: Dakika moja, malizia Mheshimiwa.

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kusema, niwaombe sana tuilinde NHIF. Muhimbili JKCI ya Jakaya Kikwete, hela anazokusanya cash ni bilioni 5.0, NHIF analipa bilioni 22 kwa mwaka. Muhimbili, hela anayokusanya cash bilioni 12, NHIF bilioni 50; hela hizi ndivyo wanavyotupa maombi, nina mgonjwa amekwama Muhimbili, nina mgonjwa amekwama JKCI, nadaiwa maiti, ndio zinatumika kulipia wagonjwa wetu.

Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kukushukuru wewe, lakini pia kwa kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ushirikiano mkubwa anaonipatia. Katibu Mkuu Dkt. Seif Shekalaghe, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Grace Magembe, Wakurugenzi wote wa hospitali, lakini kipekee nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini kuwa Waziri wa Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, hii ni bajeti yangu ya saba kusoma kama Waziri wa Afya. Mwaka huu tutaleta mabadiliko makubwa zaidi ili tuweze kuboresha huduma za afya. Sio kwamba, najua sana au nina akili sana, lakini naamini ni kwa sababu ya kudura na kadari za Mwenyezi Mungu. Ndio maana nasimama hapa kwa mara ya saba kusoma bajeti ya Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru familia yangu, ndugu zangu na watu wangu wa Tanga Mjini, nawapenda sana. Watu wa Tanga waangalie kazi zangu za Tanga Mjini, tumejenga barabara, tumejenga shule, tumeboresha Bandari ya Tanga, tumefanya mikopo. Naamini 2025 Tanga Mjini wanarudi na Odo Ummy Mwalimu na sio mtu mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naafiki.