Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nachukua nafasi ya kuwasilisha mchango wangu kwa hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Afya. Namshukuru Mungu kwa hatua hii ya kusimama mbele ya chombo chetu muhimu kupaza sauti.

Mheshimiwa Spika, napenda kwa dhati nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitahada zake na umahiri anavyosimamia ustawi wa nchi na wananchi wake kwenye nyanja zote ikiwemo uchumi, mahusiano na mashirikiano.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi anavyosimamia shughuli za Serikali kwa ufanisi mkubwa. Hali kadhalika nafurahia na kujivunia umahiri na usimamizi wa viwango wa Spika wetu katika kusimamia majukumu yake kulipaisha Bunge letu sio ndani ya Tanzania bali kimataifa, nampongeza sana Mheshimiwa Spika, Dkt. Tulia.

Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu naanza pia kuthamini kazi safi inayopimika na inzayokidhi haja inayosimamiwa na Waziri Ummy na watendaji wote wakiongozwa na madaktari, wauguzi na wadau wote katika sekta hiii ya afya.

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunakwenda kupaa katika Bara la Afrika kwa vile huduma zetu za afya zinavyoendelea kuboreka na kuwa za kisasa zaidi tumevunja kioo.

Mheshimiwa Spika, leo Madaktari Bingwa wetu wameweza kufanya operation nzito kama ya kupandikiza Uloto. Operation za kupandikiza figo na operation za moyo na nyingine kwa utaalamu wa hali ya juu bila kupasua sehemu kubwa.

Mheshimiwa Spika, madaktari mabingwa na timu nzima hizi kwa hakika waonwe na watazamwe kimaslahi zaidi. Watu hawa wanafanya kazi sana wanastahili kupata mafungu yaliyoombewa fedha bila kikwazo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono na kupongeza dhamira ya kuifanya Hospitali ya Mirembe kuwa taasisi. Kwa jinsi mahitaji ya huduma yanavyoongezeka na watu wanavyozidi kuwa wengi uwepo wa taasisi unakwenda kuwapunguzia wananchi usumbufu wa kusaka huduma.

Mheshimiwa Spika, tunashaka kwamba matatizo ya afya ya akili yanamea kwa speed na hivyo vitendo vinavyofanywa na kuvunjwa kwa maadili na udhalilishaji na hata ubakaji vinaweza kuhusishwa na mtiburiko wa akili.

Mheshimiwa Spika, nashauri Wizara ikasomesha wataalamu wengi wa fani hii Psychologists Counsellor na kuwapa kazi ya kuwashughulikia waathirika badala ya kuwatumia social workers.

Mheshimiwa Spika, wapo wagonjwa wa afya ya akili ambao wamepona walioletwa hapa Mirembe Hospital kutoka sehemu mbalimbali za nchi yetu. Fungu la kuwarudisha wagonjwa hawa baada kupona halitoshi hivyo wanabaki muda mrefu kabla ya kurudishwa makwao.

Mheshimiwa Spika, sekta hii ya afya imetendewa haki kabisa hospitali za kisasa zimejengwa na zinaendelea kujengwa karibu Wilaya zote na vifaa vya muhimu vipo; Ct- Scan, maabara ya kisasa, theatre na wodi za heshima za wajawazito na wagonjwa wengine. Vifaa tiba na dawa zinawafika wananchi.

Mheshimiwa Spika, wananchi wengi hasa wa vijijini bado wanateseka na maradhi kama haya kansa mbalimbali kama haya ya shingo ya kizazi na mengine. Pia watu wengi hawapati fursa za kupata kuchunguzwa afya zao hivyo hubaki na maradhi kwa muda mrefu na hivyo kuathirika vibaya sana.

Mheshimiwa Spika, wananchi hawa wanashindwa kupata tiba mapema na pia kutomudu gharama. Nataka kushauri Serikali kupitia Wizara ya Afya walazimishe kuchunguza wanawake waliona umri hatarishi wa kupata kansa iwe ni lazima kuchunguzwa hivyo tutaweza kuokoa maisha ya wengi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.