Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri wa Afya, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Wakurugenzi kwa kazi nzuri inayoendelea kufanywa katika kuboresha afya za Watanzania, mnafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi alivyoziwezesha hospitali zetu kupata ICU, Emergency, Ct- Scan, MRI, Angio Suite, Pet Scan na vifaa tiba vingine vingi. Nchi yetu sasa imeanza kupokea wagonjwa kutoka nchi nyingine sababu huduma za afya nchini kwetu zimeboreshwa sana. Ahsante sana Rais wetu na mama yetu mpendwa.

Mheshimiwa Spika, kilio kikubwa kilichopo kwenye vituo vya afya na zahanati ni upungufu wa watumishi na ukosefu wa dawa. Wananchi watafurahia uwepo wa majengo mazuri katika vituo vya kutolea huduma za afya kama wakienda kutibiwa watapata huduma nzuri ikiwemo kupata madawa stahiki. Kwa sasa upatikanaji wa dawa ni shida. Ili kuimarisha upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma ya afya, inabidi MSD ipewe nguvu na mtaji wake.

Mheshimiwa Spika, MSD inahusika na kununua, kuhifadhi na kusambaza dawa. Lakini MSD haina mtaji wa kwake wa kiwezesha kuagiza dawa mapema. Inategemea ipate bajeti ya hospitali na vituo vingine vya kutolea huduma ya afya, ndipo waanze kuagiza data. Utaratibu huu unafanya upatikanaji wa dawa unachelewa, sababu taratibu za manunuzi zinachukua miezi mitatu hadi sita. Kuna marekebisho makubwa yamefanyika ndani ya MSD, ikiwemo hata kurekebisha muundo. Ili kuisaidia MSD iweze kuzifikisha dawa mapema kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na ili MSD iweze kujiendesha kibiashara, napendekeza MSD ipewe mtaji wake yenyewe. Wakiwa na mtaji wataweza kuagiza madawa mapema na hivyo vituo ikiwemo hospitali, vituo vya afya na zahanati wakiagiza dawa, zitakuwa tayari ziko kwenye maghala ya MSD na hivyo dawa zitafikia vituo haraka. Mfumo wa sasa mkipeleke maoteo MSD ndipo inaanza mchakato wa kuagiza dawa na hivyo kuchelewa kuzipata. MSD wapewe mtaji wao.

Mheshimiwa Spika, pia Tanzania iliteuliwa kuweza kusambaza dawa katika nchi za SADC. Hii ni fursa, nchi yetu inabidi ijitahidi kutoikosa hii fursa. Ni hapo MSD itakapopewa mtaji wao wa kutosha wataweza kununua na kusambaza dawa Tanzania na katika nchi nyingine SADC.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kagera unapakana na nchi nyingine nne, ni rahisi kupata magonjwa ya kuambukiza na ya mlipuko kutoka nchi jirani kama UKIMWI, Ebola, Marbag na kadhalika. Pamoja na hayo Mkoa wa Kagera hakuna isolation centres. Napendekeza zijengwe isolation centres katika maeneo ya Bukoba - Muleba, Ngara, Kyerwa na Mutukura ambapo kuna mipaka inayopitisha na kuingiza watu wengi na hivyo kuongeza uwezekano wa kuletwa kwa hayo magonjwa ya kuambukiza na ya mlipuko.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kagera pamoja na kuwa pembezoni na kupakana na nchi nyingine kadhaa, bado hakuna hospitali yenye hadhi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Hili nimekwishaliongelea sana na nimeahidiwa mara kadhaa lakini fedha za kujenga hospitali yenye hadhi ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera haipelekwi. Tunaomba tujengewe hospitali hiyo. Ni lini hii ahadi itatekelezwa?

Mheshimiwa Spika, bima ya afya ndiyo itakayokuwa mkombozi wa Watanzania walio wengi. Gharama za afya ni ghali, Watanzania wengi hawawezi kumudu gharama za matibabu. Ni lini sasa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote utarudishwa Bungeni ili wananchi waweze kupata bima ya afya na waweze kutibiwa bila kikwazo cha kukosa fedha?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.