Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Afya. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwingi wa Neema kwa kunijalia afya na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Nimpongeze sana Waziri wa Afya, dada yangu Mheshimiwa Ummy, Naibu Wake, watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya. Nawapongeza sana sana.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais mnyenyekevu, msikivu, Rais mwenye huruma na mapenzi makubwa kwa Watanzania. Hii imejidhihirisha wazi katika bajeti hii, tumeona namna ambavyo ameweza kuongeza fedha ili Watanzania waweze kupata huduma bora za afya. Mheshimiwa Rais tunakupongeza sana.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii, kwa niaba ya wananchi na wanawake wa Mkoa wa Singida kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa miradi mingi ambayo ametupatia katika Mkoa wangu wa Singida; miradi ya afya, vituo vya afya vimejengwa, Hospitali za Wilaya ya Mkalama, Ikungi pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Ilongero ninampongeza sana Mheshimiwa Rais, tunamshukuru sana.

Mheshimiwa Spika, ningependa kugusia kuhusu Hospitali yangu ya Rufaa ya Mkoa wa Singida. Hospitali hii ujenzi wake umekuwa ni wa muda mrefu sana. Mheshimiwa Ummy, dada yangu amewahi kuitembelea hospitali hii pamoja na Mheshimiwa Dkt. Mollel na viongozi mbalimbali, lakini hospitali hii ya rufaa hadi sasa haijakamilika. Namwoamba sana Mheshimiwa Ummy hospitali hii ya rufaa sasa hivi ikamilike ili wananchi wa Mkoa wa Singida nao waweze kupata matibabu ya kibingwa katika Hospitali hii ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.

Mheshimiwa Spika, hospitali hii ikikamilika itaweza kuwahudumia hata wananchi wa mkoa Jirani kama Tabora, Simiyu pamoja na Shinyanga. Naomba sana Serikali itenge fedha ili hospitali yetu hii ya rufaa iweze kukamilika.

Mheshimiwa Spika, pia hospitali zangu za Wilaya ya Singida hazina vifaa tiba vya kutosha na wataalamu. Naomba Serikali iweze kuleta wataalam pamoja na vifaa tiba ili sasa matibabu yaweze kutolewa kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, Hospitali yangu ya Wilaya ya Mkalama, Ikungi pamoja na Manyoni zina changamoto kubwa ya watumishi. Naomba mtuletee watumishi. Mkalama ina ukosefu wa watumishi 750, Ikungi ina ukosefu wa watumishi 1,022 na Manyoni kuna ukosefu wa watumishi 350.

Mheshimiwa Spika, kama Wabunge wenzangu walivyotangulia kusema, kwamba uwepo wa majengo mazuri, yanatakiwa pia yawe na vifaa tiba pamoja na watumishi. Pia vipo vituo vya afya, ambavyo ni Sepuka, Mgori, pamoja Msange, havina magari ya kubebea wagonjwa na pia havifanyi upasuaji. Naomba sana vituo hivi vya afya viweze kupata vifaa tiba pamoja na magari ya kubebea wagonjwa ili huduma bora za afya kwa mama na mtoto ziweze kutolewa.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa haya machache, naunga mkono hoja na ninaendelea kuwapongeza sana madaktari wote na wauguzi wote kwa kazi nzuri ambazo wameendelea kuzifanya, ni kazi ya thawabu, Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)