Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Ghati Zephania Chomete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana katika maisha yetu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika nchi yetu. Pia nampongeza Waziri wa Afya, dada yangu Ummy Mwalimu, Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Godwin Mollel na wafanyakazi wote wa wizara hii kwa jinsi wanavyoendelea kupambana kumsaidia Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kumpongeza sana Mama Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa alizozifanya katika Mkoa wetu wa Mara. Mheshimiwa Rais alikuja mwaka 2022 katika Mkoa wa Mara, tulimwomba CT-Scan, akaahidi atatekeleza. Sasa ametekeleza, ametuletea CT-Scan Machine. Tunamshukuru sana, sana, sana kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Mara na Watanzania wote wanaoishi Mara. Kwa sababu ile mashine ni muda mrefu haikuwa kuwa katika mkoa wetu na wananchi wa Mkoa wa Mara walikuwa wanatoka Mara kwa gharama kubwa kwenda kutafuta huduma hiyo katika Mkoa wa Mwanza katika Hospitali ya Bugando. Hivyo tunamshukuru sana sana Mheshimiwa Rais kwa juhudi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto iliyoko tu pale, kuna miundombinu ambayo haijamalizika, tunamwomba Mheshimiwa Waziri, ile miundombinu imalizike ili kusudi ile mashine iweze kufungwa na wananchi wale waweze kupata huduma hiyo inavyostahili.

Mheshimiwa Spika, niendelee kumpongeza Rais wetu kwa jinsi alivyoendelea kutujengea vituo vya afya, hospitali, zahanati na hospitali za mkoa. Mkoa wetu wa Mara, vituo vya kutolea huduma ambavyo vimejengwa, tuna vituo 335. Hivyo ni kwa ujumla wa hospitali na vituo vya afya na zahanati. Katika vituo 335 tuna vituo 35 tu ambavyo ndiyo vinakidhi mahitaji ya Wana-Mara ambavyo vinalaza wagonjwa, vinatoa huduma ya damu na upasuaji.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia uwiano, ni mdogo sana. Huo uwiano kwa Mkoa wa Mara, kwa mwaka mzima wanajifungua akina mama 93,339. Unapojifungua, lazima upate huduma inayostahiki. Vile vituo ambavyo vimejengwa, havina sifa, kwa maana ya kwamba havina vifaa tiba, havina madaktari na havina madawa.

Mheshimiwa Spika, nitatolea mfano, Kituo cha Afya cha Mliba, ambacho kilijengwa mwaka 1985, lakini kinahudumia kata saba; Kata ya Nyanungu, Kata ya Golong’a, Kata ya Kwihancha, Kata ya Nyarukoba, na kata nyingine. Siyo kwamba zile kata ziko karibu, umbali ni mrefu. Mgonjwa anatembea kutoka kilometa 50 kuja tu pale kwenye kituo, na kurudi pia ni kilometa 50.

Mheshimiwa Spika, kwa uwiano, ukilinganisha ni kilometa kama 100 mgonjwa anatembea, lakini anapofika pale kwenye kituo anakosa huduma stahiki. Kituo hakina x-ray, hakina ultra-sound, hakina maji, hakina Daktari hata wa Kituo pale hayupo. Mheshimiwa Ummy mimi naamini kazi yako ni nzuri sana, hebu tembelea Mkoa wa Mara ujionee adha wanayoipata pale akina mama wale wa Mkoa wa Mara. Ni mbali sana. Siyo hicho tu, ukienda Wilaya ya Bunda, Kituo cha Bunda Mjini pale hakina uzio, hakina generator, hakina ultra-sound, wala x-ray haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alisimama hapa Mbunge wa Mwibara, akasema kuna fedha zimeletwa shilingi milioni 300 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Kasuguti kule Mwibara, lakini zile shilingi milioni 300 hazijafanya ile kazi iliyopelekewa kujenga jengo la mama na mtoto. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri aje kutueleza kwamba zile shilingi milioni 300 mama alizozitoa zijenge jengo la mama na mtoto, lakini hazikufanya hivyo, sasa sijui atatuletea nyingine au atafuatilia zile ili tujue hasa nini hatma ya wale akina mama wa Mwibara? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamwomba sana, sana, sana Mheshimiwa Waziri atuletee madaktari, hasa madaktari bingwa, hatuna. Pia tunaomba sana tuletewe vifaa tiba katika vituo vyetu vya afya na hospitali. Tunakuomba pia tuletewe magari kule kwenye Mkoa wetu wa Mara. Wana- Mara wanampenda sana mama, wanapenda sana nchi yao, kwa hiyo, tunaomba huduma zile ambazo zinaweza kupatikana kwa wengine zipatikane pia na Mkoa wa Mara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee jambo lingine ambalo ninaliona kama ni gumu sana. Kwenye wizara hii kuna Sera ya Afya inayosema, matibabu bure kwa watoto chini ya miaka mitano, wazee na wamama wajawazito. Hili jambo halifanyiki hivyo. Mama zetu, watoto wetu na baba zetu wale wazee ambao ni kuanzia miaka 65 na kuendelea wanapoenda kwenye vituo vile vya afya au hospitali hawapewi matibabu bure wanalipa. Sasa naomba hii sera tujue inatekelezwa vipi?

Mheshimiwa Spika, naomba kuishia hapo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)