Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia Wizara hii ya Afya.

Mheshimiwa Spika, nianze kukupongeza wewe binafsi kwa kazi kubwa unayoifanya ya kuendesha Bunge lako hili. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye suala zima la afya. Kabla sijaongea maeno yote nianze kuongea jambo liliotokea juzi na leo Bungeni tumeliona Mheshimiwa Rais ameweza kutafuta vifaa vya high technology, leo tunatibu sickle cell.

Mheshimiwa Spika, Binafsi sikuwahi kujua kaka sickle cell inapona; yaani sikuwahi kujua kabisa kwenye maisha yangu. Lakini kwa juhudi binafsi za Mheshimiwa Rais ameweza kupambana kuhakikisha leo katika nchi 50 za kiafrika nchi yetu ya Tanzania inatibu sickle cell, ni sifa kubwa sana na juhudu kubwa sana za Mheshimiwa Rais, tunazidi kumpongeza.

Mheshimiwa Spika, lakini nimpongeze Mheshimiwa Waziri Ummy na Naibu wake Mollel kwa kazi kubwa wanayoisimamia kufikia hatua hii tuayoiongelea sasa hivi. Mheshimiwa Rais yuko na juhudi sasa za kujenga kituo mahiri cha utibabu wa kansa hapa Dodoma katika Hospitali ya Benjamini Mkapa ambacho kitakuwa ni kituo kikubwa cha Afrika. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kutujali kwa sababu ni magonjwa ambayo hayana tiba na yanaua vizazi na vizazi.

Mheshimiwa Spika, hakika tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais tangu tumepata uhuru wa nchi hii hatujawahi kuwa na mashine kubwa kama za CT scan kwenye mikoa yetu, ilikuwa ni lazima ufunge safari uende Muhimbili uende Bugando, na hiyo ni kwa familia tu ambazo zina uwezo familia ambazo hazina uwezo hata kujua mgonjwa wao anaumwa nini inakuwa siyo rahisi na hatimaye mnakutwa na vifo.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa juhudi zote za kazi kubwa anayoifanya kusimamia miradi ya kimkakati ambayo inaenda kumalizika, kupeleka pesa kwenye halmashauri, kufanya kila aina ya kazi. Halmashauri sasa hivi kuna fedha zinazoenda asilimia 100 tofauti na ilivyokuwa hapo kale. Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa sana sana sana.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais pia amejitoa kusimamia Demokrasia ya nchi hii ni jambo kubwa sana. Sasa hivi hakuna tena mapigano hekaheka za kisiasa, tuko kimya tunatekeleza maendeleo jinsi Mheshimiwa Rais anavyo yataka.

Mheshimiwa Spika, mimi niungane tu na mzee ma-bi, ma-bi na ma-tri ma-tri, kwamba wale wenzetu wa upande wa pili ambao ni marafiki zetu wa kisiasa kwa heshima kubwa na kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Rais waweze kumuachia apite bila kupingwa, kwa sababu ameleta vitu ambavyo tulikuwa hatuvifikirii kabisa. Ameleta demokrasia, amaeleta maridhiano ambayo nchi yetu imekuwa ina sifa kubwa kwa wenzetu. Sasa, kama za jirani wanaona sifa kubwa kwa nini sisi tusimpongeze Mheshimiwa Rais na kumpa heshima ya kupita bila kupingwa?

Mheshimiwa Spika, lakini vile vile nindelee kuipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa waliyoifanya kwenye Mkoa wetu wa Tabora leo hii Mkoa wa Tabora tumekuwa na jengo la emergency ambalo lina vifaa vyote na inafanya kazi, ni kitu ambacho hakijawahi kutokea, kwa kweli. Nimezaliwa pale na nimekulia hatukuwa na jengo la emergency na niliwahi kuongea humu Bungeni mara kadhaa. Kwa Mheshimiwa Samia Suluhu imewezekana na jengo hili linafanya kazi. Saa hivi tunamalizia jengo la ICU ambapo vifaa vya ICU vyote vimefika, ni bado muda mchache tu tutaanza kulitumia, tunatoa pongezi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, tuna wodi mbili za wazazi za ghorofa, wodi ya kwanza imekwisha bado wodi ya pili ambayo ipo inaendelea, ila fedha zimekwisha. Mheshimiwa Ummy tunakuomba sana utumalizie jengo hili la ghorofa la mama na mtoto ili lianze kutumika. Tunajua unajua umuhimu wa mama na mtoto na tunajua jinsi unavyolisimamia jambo hili tunakuomba sana.

Mheshimiwa Spika, narudia kusema katika mkoa wa tabora tuna CT scan ambayo inafanya kazi iliyonunuliwa kwa bilioni moja na milioni mia nane. Hili ni jambo la kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Leo ndugu zetu wamekuwa wanapata kila kitu pale Tabora wanampongeza sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashukuru sana kwa watumishi 38 mliotupa tumewagawa katika kada mbalimbali; lakini bado tuna upungufu mkubwa wa watumishi hasa madaktari bingwa. Kwenye ikama ya Serikali tunatakiwa tuwe na madaktari bingwa 21 lakini tuna madaktari watano tu, wa akina mama mmoja, wa watoto watatu na wa upasuaji mmoja; katika mkoa mzima wenye wilaya saba. Mkoa huu kwenye Sensa ya mwaka jana imekuwa mkoa wa tatu kwa kuwa na wananchi wengi. Watanzania wengi wanaishi Mkoa wa Tabora kutoka Dar es salaam, Mwanza kisha Tabora, lakini tuna madaktari bingwa watano tu.

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri atuongezee madaktari bingwa. Tofauti na hapo watu wengi sana inabidi waende kwenye hospitali za rufaa wabebwe na ambulance. Hospitali yetu ya Mkoa wa Tabora ina ambulance moja tu, ambulance nyingine zote ziko TAMESA zinaumwa, haziponi wanasema vipuli hakuna. Sasa sijui ni vipuli hakuna au ni bajeti ya Serikali haipo; hapa nashindwa kuelewa. Kwa sababu hizi land cruiser vipuli vyake vipo. Mkitupatia hata milioni 50 tunaweza tukatoa ambulance hata 10 zikafanya kazi kwa sabau mkoa wetu ni mkubwa mahitaji ni makubwa sana. Tunakumba sana Mheshimiwa Waziri tupate ambulance. Mkoa wa Tabora ni mkubwa, wewe unaufahamu, na una wakazi wengi wengi kweli kweli.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu suala la dawa limekuwa ni kero kubwa. Mheshimiwa Waziri nikuombe sana muongeze mtaji MSD ili watu wakiwa na cash sasa wafike walipie na wapate dawa za kwenda kwenye mikoa yao na Watanzania waendelee kuhudumiwa. Tunajua Serikali imetenga pesa nyingi hilo Mheshimiwa Waziri hautalishindwa.

Mheshimiwa Spika, ningee sasa kuhusu Malaria. Mwaka 2017/2018 tulikuwa na wastani wa asilimia 11.7 za wagonjwa wa malaria lakini leo hii mwaka 2022 tuna wastani wa 23.4 na hali ya malaria imekuwa mbaya, tuna wagonjwa wengi kwenye hospitali yetu ya mkoa ambao wanaumwa malaria.

Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri wafanye kila aina ya mikakati kuhakikisha tunapata dawa nyingi za malaria. Pia wafanye mkakati wa kuhakikisha wanazuia ugonjwa huu wa malaria kwenye mkoa wetu, ambao umekuwa ni mwingi sana. Tunakuomba sana Waziri. Ugonjwa huu tunajua unashambulia watoto wadogo pamoja na akina mama wajawazito, tunakuomba sana utusaidie.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri aliwahi kuja Tabora. Tulionge humu Bungeni wakatuambia kwamba hospitali ya kanda inajengwa kwenye Mkoa wa Tabora. Mheshimiwa Ummy alikuja Tabora, tukafanya mkutano tukiwa naye kwenye Hospitali ya Kitete, akasema tafuteni eneo. Tumetafuta eneo ekari 200 kwenye Wilaya ya Uyui. Mheshimiwa Waziri hii Hospitali yetu ya Kanda ya Mkoa wa Tabora vipi? Tunaomba ukija ku-wind up utupe majibu. Wananchi wa Tabora wamenituma wanasema tunataka hospitali yetu ya kanda, Mheshimiwa Waziri alituahidi hapa. Kwa hiyo Mheshimiwa Ummy wanakusikiliza na wanategemea majibu yatoke kwako ili waweze kujua kuhusu hospitali yao.

Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kwa kusema, kuna watu waliongea hapa wakasema wauguzi wengi wana majibu mabaya sana. Lakini mimi niwe upande wa wauguzi kwa leo. Niliwahi kwenda kumuangalia ndugu yangu hospitali amelazwa wodi moja ina vitanda 40 wamelala wagonjwa wawili wawili. Huyu nesi yuko na nesi attendant wake mgonjwa huyu anamaliza drip, mgonjwa huyu anatapika, mgonjwa huyu anatakiwa achomwe sindano. Yaani inafika stage nilikuwa nawasaidia kuwachukua wagonjwa kuwapeleka kwenda kujisaidia. Wanazidiwa Manesi wetu hata ningekuwa mimi wagonjwa 80 walio mahututi unawahudumia wewe peke yako. Nikumuomba Mheshimiwa Waziri mjitahidi sana kutuongezea wauguzi.

Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuwalaumu saa nyingine mtu anachoka anafikia the maximum, yaani anajikuta amejibu tu jibu lile. Na sisi kwa kweli tuone kazi kubwa wanayoifanya wauguzi wetu kazi kubwa wanayoifanya madaktari wetu.

Mheshimiwa Spika, kitaalamu wanatuambia sijui daktari mmoja anatakiwa ahudumie watu wangapi, lakini unakuta ni daktari mmoja tu tangu asubuhi amehudumia watu zaidi ya 150, amechoka, yuko hoi. Tuendelee sana kuwasemea ili waweze kupata madaktari wengi na manesi wengi watu wetu waweze kupata huduma nzuri; lakini pia waendane na posho zao stahiki ambazo pia zitazidi kuwatia moyo manesi wetu na Madaktari wetu na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja.