Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia katika bajeti hii ya Wizara yetu pendwa ya Afya.

Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza sana Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya madaktari wao, madaktari bingwa katika nchi hii, tumeona jitihada zao za dhati kutoka moyoni, kuanzia Jakaya Kikwete Muhimbili hapa Benjamini Mkapa, Bugando Mbeya na KCMC inaonyesha ni namna gani madaktari wetu katika nchi hii sasa wanaanza kwenda mbele zaidi ya uzio.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi ushauri wangu kwa Wizara, ni kwamba lazima ifikie sasa Wizara iunde timu ya madaktari bingwa labda, kwa sababu tunazo wilaya 139 na hao madaktari bingwa wawepo madaktari bingwa ambao ni mobile unit, wanaotembea.

Mheshimiwa Spika, hawa madaktari bingwa katika nchi hii watapunguza mrundikano kule Muhimbili, kwa sababu sisi tunajua kwa kalenda, kama labda Mkoa wa Mwanza kuna madaktari kumi; wanaingia madaktari bingwa wa macho, viungo, figo na moyo. Wakifika pale tunaambiwa kwamba Sengerema watakuwepo kwa wiki mbili au kwa siku mbili; wale madaktari bingwa watasaidia watu wetu ambao ni maskini ambao hawana uwezo wa kusafiri kuja katika hospitali za rufaa.

Mheshimiwa Spika, katika hili tunamshukuru Mheshimiwa Rais sasa vifaa tiba vimeanza kupelekwa nchi nzima. Tuna kila kitu katika hospitali zetu za wilaya. Mnafeli wapi watu wa Wizara ya Afya katika jambo hili?

Mheshimiwa Spika, Tunaona hospitalli zetu za makanisa Wajerumani wale Waholanzi wana ma-flying doctors wale, wanasafiri wanakuja Itigi, Sengerema na kwingine, na wanafanya jambo kubwa sana. Wanakuja na meli, sisi tumewahi kwenda kutibiwa na Wachina kwenye meli bandarini. Hapa tuna madaktari bingwa wamemaliza elimu zao, kwa nini msitengeneze unit hiyo ya madaktari bingwa ambao bado hawajapata ajira lakini wawekwe katika sehemu hiyo? Wale madaktari watasaidia sana kupunguza magonjwa hayo ambayo wananchi wamekaa nayo kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala jingine ambalo nataka niishauri Wizara hii ni kwamba, tunayo magonjwa haya ya mlipuko ambayo yamezunguka katika ukanda huu wa maziwa makuu haya magonjwa hayajaisha naishukuru sana Wizara kwa kuchukua hatua ya haraka katika hili gonjwa lililojitokeza Bukoba watu wengi waliona kwamba wale Watanzania inakwenda kuangamia lakini jambo hili waliweza kulidhibiti ndani ya siku kumi likaisha tunaipongeza sana Wizara katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule Usukumani wamenituma nije nishukuru wanasema yule Mama wa corona mbona hatumuoni, hali sasa siyo nzuri sasa tunataka huyu Mama wa corona sasa leo aje aseme hapa, je, corona imeisha? Kwenye nchi hii? hawa wanaokufa wanakufa kwa mafua tu? Au wanashindwa kupumua?

Mheshimiwa Spika, sasa haya tunakuomba sana Mheshimiwa Waziri katika majumuisho yako uje utueleze haya magonjwa ya mlipuko ni namna gani mmejipanga nayo; na kama yamekwisha au kama hayajaisha basi tuendelee kuchukua tahadhari. Unayo nafasi kubwa sana kwa mujibu wa sheria kuwaeleza Watanzania nini kinachoendelea.

Mheshimiwa Spika, nakuja kuzungumzia hospitali zetu za wilaya. Hizi hospitali za wilaya sasa hivi zinapelekewa madaktari zimepewa vifaa tiba nchi nzima, lakini tunavyo vituo vya afya na zahanati. Sasa kule kwa sababu kuna madaktari sasa wanahitajika madaktari bingwa. Leo vituo vyetu vya afya vilikuwa havijapata madaktari vinapelekewa madaktari. Sasa, kama mnapeleka madaktari kule kwenye Hospitali zetu na vituo vya afya basi hizi hospitali za wilaya mziweke katika sehemu ya hospitali za rufaa. Kwa sababu, kwa mfano kwenye jimbo langu mimi nina hospitali vituo vya afya ninavyo vinane bado nina zahanati karibu zahanati 30.

Mheshimiwa Spika, sasa unategemea kwamba wagonjwa wale tunawapa rufaa kuwapeleka Bugando au Sekou Toure hospitali inakwenda kuelemewa. Ninachoomba mimi katika sera sasa za Wizara mzitambue kuzichukua hizo hospitali za wilaya ziwe zenu, madaktari bingwa wapelekwe kule ili tupunguze msongamano Muhimbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri hili wazo Mheshimiwa Waziri alichukue. Katika majumuisho yake aje atuambie; kama wanaweza kuhudumia, kupeleka vifaa tiba na kila kitu kwa nini wasilete madaktari bingwa kule? Vifaa vya maabara na wataalamu wamepeleka, isipokuwa hatuna madaktari bingwa naomba sana Wizara wachukue jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, jingine ambalo ni la muhimu sana ni suala la huduma bora kwa hawa wagonjwa wetu. Tunakwenda kutoa huduma bora lakini muangalie na madaktari katika nchi hii sasa nao wapewe huduma. Madaktari wanakiumbia katika nchi hii, wanaondoka. Wauguzi nao muwajali sasa ifikie hatua…

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. TABASAM H. MWANGAO: Mheshimiwa Spika, niache basi Mheshimiwa nimalizie.

SPIKA: Mheshimiwa Tabasamu kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge.

TAARIFA

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nilikuwa naomba kumpa taarifa tu Mheshimiwa tabasamu kwamba, hata vitabu vitakatifu vimeisema vizuri nafasi ya daktari na imeisema; “Innal Muallima Wa Twabiba Kila Humaa, Laa Yanswahan Idhaa Huma Lam Yukramaa Fakna-A Bijahilika In-Jaufata Muallimu, Fasbir Lidaika In Jaufata Twabiba,” kwamba; ridhika na ujinga wako ukimuudhi mwalimu, lakini subiri maradhi yako ukimuudhi daktari. Madaktari ni watu muhimu sana, tusiwaache watoke nje. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Tabasamu unaipokea taarifa hiyo?

MHE. TABASAM H. MWANGAO: Mheshimiwa Spika, ameanza kwa Aya kwa hiyo amenipiga kwa Aya, na mimi kama muumini naunga mkono taarifa yake.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la utoaji wa huduma zetu za afya. Viongozi wetu wa kitaifa wamekuwa wakipita kule katika wilaya zetu, wanapita katika na mikoa, tarafa na kata, wanatoa ahadi kwamba hapa patajengwa hospitali ya wilaya, patajengwa kituo cha afya, patajengwa zahanati.

Mheshimiwa Spika, sasa tunamuomba sana Waziri wa Afya, hizi ahadi za Marais, ahadi za Waziri Mkuu, ahadi za Mawaziri wao wenyewe mnazozitoa kwa wananchi zinakuja kututesa sisi. Sisi Sengerema tunakushukuru ulitoa ahadi ya kujenga Kituo cha Afya Chifufu, kile kituo cha afya Mheshimiwa Waziri wamenituma nije nikushukuru kimeisha, tunakupongeza sana kwa hilo.

Mheshimiwa Spika, alipita Hayati John Pombe Magufuli pale Busisi, na pale Busisi ni kwao, akatoa ahadi kwamba kuna kituo cha afya kinajengwa pale akiwa na Naibu Waziri Mollel; hili jambo mpaka sasa hivi mnataka labda mimi nikashindwe uchaguzi, kuna lawama zingine zitakuwa zinanitafuna mimi kwa sababu Mheshimiwa Mollel ulikuwepo. Sasa, naomba leo kwenye majumuisho hapa mkija mseme lini Kituo cha Afya cha Busisi kinakwenda kukamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jamani tuziheshimu hizi ahadi za Marais. Marais wanapopita kule kwetu sisi wanatuacha na hali mbali. Mnakuja kwenye bajeti hivi viyu havimo, inakuwa ni hatari. Sasa naomba kwenye majumuisho ya Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri waje waseme lini jambo hili litakuwepo.

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho nina Hospitali ya Wilaya. Wewe mwenyewe Mheshimiwa Ummy ulifika pale na umeiona ile hospitali. Mheshimiwa Jafo alipita pale akaona; na leo wote mmo humu. Mheshimiwa Mollel hii Hospitali ya Wilaya imeshakamilika kila kitu. Ni kwa nini hospitali hii haifunguliwi? Naomba majibu katika hayo.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nakupongeza leo umekaa kwa utulivu mkubwa na mimi nakuunga mkono dakika zangu kumi hazijatosha nimeacha dakika mbili kwa wengine.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Mungu akubariki sana, amina. (Makofi)