Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Afya kwa Mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge wote kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu, pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Afya na Taasisi zake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo naomba pia na mimi nichukue fursa hii kumshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri sana anayoifanya katika suala zima la kuleta maendeleo. Pia kuhakikisha kwamba anaiangalia sekta hii ya Afya kwa jicho la kipekee, nampongeza sana Mheshimiwa Rais. Tunajua kabisa azma yake ni kuhakikisha kwamba afya ya watanzania ina imarika ili kusudi waweze kufanya maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa Saba wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ambapo ameeleza kwamba azma ya Serikali ni kuboresha utoaji huduma pamoja na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya katika hospitali za rufaa, hospitali za mikoa, hospitali za kanda, maalum na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili naomba nitoe ushauri, natambua kazi nzuri sana ambayo inafanywa na Serikali. Lakini pia napenda kuishauri Serikali hasa kwa Mkoa wangu wa Dodoma, katika Mkoa wa Dodoma, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, hospitali hii ni tegemeo kubwa sana kwa wananchi wa Dodoma na maeneo mengine ya Jirani.

Mheshimiwa Spika, wananchi wengi wanategemea kupata matibabu katika eneo hili. Naipongeza sana Serikali imejitahidi sana kuwekeza miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa jengo la wagonjwa la ICU lakini pia usimikaji wa mashine ya CT – Scan ambayo iko katika hospitali ile na inatumika vizuri.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hayo ni kwamba hospitali ile ina majengo mengi sana ambayo ni chakavu na ambayo yalikuwepo tangu enzi za mkoloni. Pamoja na kwamba kuna majengo ambayo yamekuwa yakijengwa lakini bado eneo lile ni dogo. Kwa hiyo, nilikuwa naomba nitoe ushauri kwamba, hebu Serikali ione umuhimu basi katika eneo lile dogo iweze kujenga majengo ya ghorofa ili kusudi kuweza kupata majengo zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na mpango wa Serikali wa kujenga ghorofa ambalo lingeweza kuhudumia magonjwa ya mifupa. Ushauri ni kwamba Serikali ione uharaka sasa wa kujenga jengo hili la mifupa ili kusudi wananchi waweze kupata tiba vizuri na jengo liwe la kisasa. Naamini kabisa kama likijengwa jengo hili basi huduma zitapatikana kwa uzuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwamba hospitali hii ya mkoa ambayo ni maarufu kwa jina la General Hospital inapakana na eneo la jeshi ambalo liko Jeshi la polisi pale. Kwa hiyo, kuna eneo liko pale, Serikali iome umuhimu wa kulitoa lile eneo la Polisi kwa hospitali ili kusudi waweze kujenga miundombinu zaidi katika kuendeleza majengo mapya kwa ajili ya utoaji wa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri mwingine ni kuhusiana na manunuzi ya dawa katika vituo vya kutolea huduma. Kuna fedha kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa za dawa moja kwa moja kutoka bohari, hili ni jambo jema sana. Lakini kuna nyakati bidhaa hizi yaani dawa zinakuwa hazipatikani katika bohari ya dawa. Ushauri wangu, je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na asilimia fulani ya fedha zipelekwe kwenye akaunti za vituo husika ili bidhaa zinunuliwe kutumia wazabuni wengine? Hii itachangia upatikanaji wa dawa pale ambapo bohari kuu inakuwa imeishiwa dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niliona kwamba nishauri hili kwa sababu tumekuwa tukipata malalamiko ya mara kwa mara kuhusiana na upungufu wa dawa katika vituo pamoja na hospitali. Kwa hiyo basi, ushauri wangu kama Serikali itaona hii inafaa basi hebu ichukue ushauri huo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilitamani kuzungumzia nilitaka kuzungumzia kuhusiana na suala zima la mwitikio wa UKIMWI. Natambua juhudi kubwa sana ambazo Serikali imekuwa ikizifanya kwa ajili ya kupambana na UKIMWI, naipongeza sana Serikali. Hata hivyo, pamoja na pongezi hizo bado maambukizi mapya yanaendelea na takwimu za hivi karibuni zinaonesha kwamba walau karibu wananchi 54000 wamepata maambukizi mapya. Hii taarifa nzuri. Basi nilikuwa naomba Serikali iendelee na juhudi za kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI.

Mheshimiwa Spika, lakini katika ukurasa wa 40 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, watoto 58760 wapo katika dawa za ARV. Hii sio taarifa nzuri kwani inaonekana kwamba watoto hawa walipata maambukizi kutoka kwa mama zao. Kwa hiyo basi, natambua juhudi za Serikali kwa kuona Kwamba maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yanakuwa yanazuiwa. Kikubwa ni kwamba inabidi elimu itolewe ili kusidi hawa wakina mama waweze kufika katika vituo vya clinic mapema waweze kupata huduma mapema ili kusudi wasiweze kuwaambukiza watoto wao.

Mheshimiwa Spika, Tanzania bila maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto inawezekana. Kwa hiyo, nilikuwa naishauri Serikali iendelee kutoa elimu hasa katika maeneo ya pembezoni. Kwa sababu tunaamini kabia mijini wanapata elimu lakini pia maeneo ya pembezoni wanapata elimu lakini wanahitaji elimu zaidi ili kusudi waweze kupata huduma mapema na mwisho wa siku maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto yanaweza kuzuiwa.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, ambalo nilitaka kuzungumzia kuhusiana na hili suala la UKIMWI ni kuhusu huduma ya early infant diagnosis ambapo watoto wachanga waliozaliowa na wakinamama wenye VVU hupimwa kwa kutumia vinasaba. Taarifa imebainishwa ya kwamba vituo viko 130 na vinaendelea kutoa huduma lakini ili kuweza kufikia malengo Serikali inatamani kuwa na vituo 340 na hii itasaidia kupunguza maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto hasa maeneo ya pembezoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, Serikali basi iweze ku– speed up kuhakikisha kwamba vituo hivi vinajengwa kwa wakati ili kusudi wakinamama wale ambao wana maambukizi waweze kupimwa na hatimae wakishajua hali zao waweze kupata zile huduma ili kusudi mwisho wa siku watoto wao wasiweze kupata maambukizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba niseme kwamba naunga mkono hoja ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia. (Makofi)