Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Dr. Paulina Daniel Nahato

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi nami nichangie katika Wizara hii ya Afya. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mungu kwa kunijalia afya na kusimama leo na kuweza kuchangia katika Wizara.

Mheshimiwa Spika, pia naomba kumshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kujali afya ya wananchi wote na hivyo kuipatia Serikali fedha nyingi sana ili huduma ya afya iweze kuboreshwa kuanzia katika ngazi ya vijiji mpaka ngazi ya juu. Napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Waziri na kumshukuru sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kazi nzuri anayoifanya. Kwa kweli ni mchapakazi, pamoja na Naibu wake, timu yote na Madaktari wote Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya. Nawapongezeni sana, kwani hii kazi ni nzuri, ni kazi ambayo ni ya muhimu kwa sababu bila afya kwa wananchi, maendeleo hayawezi kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeipitia hii bajeti na kwa kweli inatia moyo sana, na kwa kweli tumepiga hatua na tunaenda sehemu nzuri. Naomba nichangie kwanza kwa kuipongeza sana Wizara ya Afya kwa mambo matatu ambayo wameyaleta na wanakwenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, nawapongeza kwa kuja na mpango wa uzalishaji, uratibu na kuwatumia wahudumu wa afya katika ngazi ya jamii (Integrated and Coordinated Community Health Workers Programme). Hii ni muhimu sana, na kwa kweli italeta mafanikio makubwa sana katika Wizara ya Afya na afya kwa ujumla. Kwa sababu katika ngazi ya familia ndipo walipo watu wengi, hawajulikani na hawaendi kupata matibabu wanapoumwa. Kwa hiyo, hii programu italeta mafanikio makubwa kwa sababu hao watakaokuwa trained watakuwa kule katika ngazi ya chini katika vijiji, na watakuwa wanawafahamu watu na tamaduni na hata lugha mbalimbali za watu, na hivyo hii programu itasaidia sana kupunguza gharama au mzigo mkubwa kwa Serikali katika kuleta tiba katika hospitali zetu kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa pika, kwa hiyo, kwa hilo naipongeza sana Wizara ya Afya kwa kuja na mpango huu. Nina hakika, hata nchi ya Rwanda ambayo Bunge liliwahi kunituma kuwakilisha, waliona hilo kwamba lilikuwa ni jambo lililokuwa na mafanikio. Naipongeza sana Wizara kwa kuliona hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, naipongeza sana Wizara kwa kuanzisha programu ya kuwa na Bachelor of Science Psychology katika Vyuo Vikuu nchini, kwa kuanzia na Chuo Kikuu cha MUHAS. Tatizo la afya ya akili limeongelewa mno na hata Mheshimiwa Ummy Mwalimu inaonekana sasa hivi anaijua vizuri hii changamoto ya afya ya akili. Afya ya akili ni chanzo cha matatizo ya magonjwa mengi. Hivyo basi, programu hii inapoanza itaenda kutoa suluhisho la matatizo mengi ya magonjwa ambayo yanaambatana na magonjwa ya akili. Kwa hiyo, naipongeza Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, naipongeza Serikali kwa kuipandisha hadhi Hospitali ya Mirembe kutoka katika jina hili na kuifanya kuwa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili. Hili jina “Mirembe” kwa kweli lilikuwa linaleta unyanyapaa (stigma). Neno “Mirembe” hata mtu wa kawaida akiambiwa, anaonekana kama ni kichaa. Kwa hiyo, sasa hivi Wizara kwa kuliona hilo, na kubadilisha hospitali hii na kuipa hadhi, itaonekana ni seheme ya kawaida kabisa kama hospitali nyingine zozote nchini. Kwa hili nawapongeza sana, sana, sana Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie mambo manne kwa Wizara yetu ya Afya. Jambo la kwanza, niwaombe kama nilivyowahi kuchangia, kuwekeza zaidi kwenye kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza (Non-Communicable Diseases). Naomba sana hili suala tuliangalie. Magonjwa mengi ambayo siyo ya kuambukiza, yanaleta changamoto. Gharama za kutibu magonjwa haya ni ghali na kwa kweli yana-consume fedha nyingi sana. Kwa hiyo, kama tutawekeza uzito katika kuzuia magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza, hakika mambo yatakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, suala la pili, ninaishauri Serikali au Wizara kupanua wigo wa huduma ya vipimo (Diagnostic Services) katika jamii zetu. Kwa sababu kuna magonjwa mengi ambapo yanapogunduliwa mapema, kwa mfano kansa, inatibika, lakini mara nyingi wagonjwa wanakuja hospitali wakiwa tayari wako katika stage nyingine. Kwa hiyo, tuboreshe pia hizi huduma za kugundua magonjwa yanapokuwa katika stage ya awali kabisa.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, naomba kuishauri Serikali, kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya teknolojia ya afya, Wizara itenge fedha kwa ajili ya elimu endelevu kwa watumishi wa Wizara ya Afya. Mambo yanabadilika kila siku, kwa hiyo, in service training, workshop pamoja na kozi fupi fupi kwa wafanyakazi wa afya au watoa huduma wa afya itawasaidia kuwafanya watoe huduma iliyo bora zaidi, inayoendana na teknolojia na mabadiliko yanayotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la nne, naendelea kuishauri Serikali kwa kutoa motisha kwa wafanyakazi wanaofanya kazi vijijini. Watoa huduma wa afya wanapopelekwa vijijini wanaanza kufikiria maisha ya kijijini, kwa hiyo, wanakata tamaa, wanatamani kupangwa mijini. Naiomba Serikali tu iweze kutoa motisha; itoe incentives ili daktari au mtoa huduma anapopelekwa kijijini afurahie, ajue kwamba mimi kumbe kule kijijini nitakuwa aidha tofauti na wa mjini au nitakuwa bora. Kwa hiyo, atafurahia kwenda kufanya kazi vijijini, kuliko hivi sasa ambapo anayekwenda kijijini akifikiria kupata nyumba, akifikiria hali ya kijijini, anaanza kujifikiria mara mbili mbili, anatamani kufanya kila mbinu ili abaki mjini. Watakapopata motisha, labda wao na familia zao, na uhakika pengine wa kupata malipo ya ziada kwa kazi wanayofanya vijijini, kwa sababu tunajua vijijini changamoto ni nyingi. Kwa kweli wafanyakazi wengi watatamani kwenda vijijini hata kuliko kubaki mijini kwa sababu wanajua wataangaliwa kwa jicho tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya muda, naomba kuipongeza tena Serikali kwa kazi nzuri. Naomba kuwashukuru sana Wizara kwa kuiangalia hili.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)