Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi na nipende kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu wingi wa Rehema, ambae ameweza kutufanikisha kuweza kujadiliana na kutimiza majukumu yetu kwa siku mbili.

Mheshimiwa Spika, pia nipende kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa wema wake na hekima alizojaliwa na Mwenyezi Mungu na akaona kwamba aweze kututumikia watanzania, aweze kuokoa jamii ya watanzania kwa kuwa na dhamira safi ya kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dhamira hii ililenga kumtua mama ndoo kichwani lakini kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wameweza kuongea. Pia, si tu kumtua ndoo mama kichwani bali kuokoa familia kwa sababu ndoa zinakwenda kuimarika. Wakinamama wanaacha kwenda kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kutafuta maji, sasa wanakwenda kufanya majukumu yao kama mama kama Mke ndani ya familia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais, dhamira yake hii ameweza kuitekeleza na mara kadhaa akiwa katika misafara anapotembelea miradi na kuzindua, amewahi kuongea “anachukizwa anapokutana na wakinamama huko kwenye vijiji wamebeba ndoo kichwani” na dhamira hii imeendelea kuonekana. Vilevile, alishasema yeye mwenyewe ni Mama maji, atahakikisha Tanzania inakwenda kupata maji safi na salama. Hili ameweza kulithibitisha kwa mwaka huu wa fedha tunaokwenda kuumaliza 2022/2023, kupata fedha asilimia 96. Hii inaonesha mama amekuwa akisema na kutenda na tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, naomba nimshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango, nae hajawa nyuma katika hili wakati akiyatetea mazingira. Tunafahamu vyanzo vya maji vinahitaji mazingira lakini tunamshukuru pia Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa na yeye pia vita hii ya kuhakikisha tunamtua ndoo mama kichwani hajawa nyuma. Hata katika hotuba yake tumeweza kumsikiliza na tumeona kabisa commitment ya Serikali katika kuhakikisha tunapata fedha zitakazohakikisha miradi inabuniwa lakini vilevile inatekelezwa na kukamilishwa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nikupongeze wewe mwenyewe, wewe ni Spika wa viwango kama walivyosema wengine, umekuwa ukitupa ushauri mara kadhaa sisi Serikali na ushauri wako mara zote umekuwa na tija kubwa sana kwa sisi kuweza kutimiza majukumu yetu. Ninakuombea kwa Mwenyezi Mungu, wananchi wa Mbeya Mjini waendelee kukuelewa kama wanavyokuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawapongeza wananchi wa Mbeya Mjini kwa kuweza kuongozwa na wewe kwani hata kwenye jimbo lako tunajifunza kwa matendo. Kazi nyingi unazozifanya na sisi tunakuiga kwa sababu wewe ni kiongozi wa mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze pia Naibu Spika kwa kazi nzuri pia anayoifanya na ushirikiano mkubwa ambao ametupatia sisi Wizara ya Maji, ushauri wake tutaendelea kuzingatia na kuhakikisha tunatimiza majukumu yetu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze na kuishukuru Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira. Mheshimiwa Mwenyekiti, Jackson Kiswaga, pamoja na Makamu wake Mheshimiwa Anna Lupembe pamoja na Kamati nzima, mmekuwa washauri wazuri katika kuona tunatimiza wajibu wetu na tunahakikisha tunamtua ndoo mama kichwani kwa umoja wetu. Tunawashukuruni sana Kamati tuko tayari kuendelea kushauriwa ili tuweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Wabunge wote, mmeongea vizuri sana tunawashukuru kwa pongezi, tunawashukuru kwa ushirikiano. Pale mnapoweza kuwasemea watendaji wetu kama ya mameneja wa wilaya waweze kuthibitishwa inaonesha dhahiri mna mashirikiano nao mazuri. Kwenye hilo tunawashukuruni sana na hayo ni maelekezo ya Mheshimiwa Waziri, Jumaa Hamidu Aweso, nyakati zote za vikao kwamba, watendaji wawe na mahusiano mazuri na Serikali, wabunge, pamoja na Chama Tawala ambacho ilani yake tunaitekeleza. Ahsanteni sana Waheshimiwa Wabunge, hoja zote, ushauri ambao mmetupatia, sisi kama wasaidizi wa Mheshimiwa Waziri, tumesikia, tumepokea tutatekeleza kwa msaada wa Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wameweza kuziongea humu ndani, naomba nitaziongea chache na nyingi ataziongea Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la uvunaji wa maji ya mvua. Sisi kama Wizara tumejipanga vizuri na kuhakikisha suala la uvunaji wa maji ya mvua tunakwenda kulifanyia kazi kwa umakini mkubwa. Pamoja na kutumia majengo makubwa ya Serikali, pamoja na kutumia majengo ambayo pia tunashauri wananchi waweze kuvuna kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge mmeweza kushauri, tutazingatia na kufanya hayo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, kumshukuru Mheshimiwa Samia Samia Suluhu Hassan, ni pamoja na kutendea kazi vifaa alivyotupatia. Mvua kwetu kama Wizara huwa tunahesabu ni baraka na mvua hii ambayo Tanzania tunaipata kwa wingi hatutaki iendelee kuonekana ni laana. Tuna vifaa vya kuchimbia mabwawa, tutavitumia vifaa hivi ambavyo Mheshimiwa Rais, alitoa fedha nyingi tumeweza kuvinunua na tayari tumeshavipokea hapa nchini na tayari vimekwishaanza kazi. Maeneo mbalimbali ambayo yanakuwa na mafuriko tutahalkikisha tunakwenda kuchimba mabwawa madogo, makubwa na ya kati ili tuweze kuvuna maji haya yaweze kutumika kwa mifugo, kilimo vilevile kwa mahitaji ya majumbani na viwandani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tutaendelea kuhakikisha miradi mikubwa ambayo tunaijenga nchi nzima, tunakwenda kutumia vizuri rasilimali fedha ambayo Mheshimiwa Rais anakesha kuitafuta na kutupatia sisi Wizara kwa uaminifu mkubwa, kuona maeneo ya vijijini ambayo miradi hii mikubwa inapita basi na wao wakabaki kuwa wanufaika. Hatutapitisha mabomba makubwa na kuwacha vijiji hivi ambavyo vinapitiwa na miradi mikubwa bila kupewa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, tuna Chuo chetu cha Maji. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, ameendelea kutoa fedha nyingi kwenye Chuo cha Maji, sasa hivi Chuo cha Maji kina sura nzuri, tunaamini elimu nzuri inapatikana kwenye mazingira mazuri. Mazingira ya Chuo cha Maji yameboreshwa kwa sehemu kubwa na yanaendelea kuboreshwa. Tutahakikisha wale wahitimu tunaendelea kuwatumia kwenye miradi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, anapenda kusema tunajenga hospitali anapelekwa daktari na nurse. Sasa Wizara ya Maji tumesema si tu kukabidhi zile jumuiya za watumia maji, tutatumia wataalam wetu ambao tunawazalisha kwenye chuo chetu ili waeze kusimamia hii miradi vizuri kwa weledi mkubwa ili kuongeza tija zaidi. Tayari tumekwisha anza kuwatumia wataalamu hawa na tutaendelea kuwatumia zaidi na zaidi.

Mheshimiwa Spika, suala la vifaa vya kazi, sisi kama Wizara tayari tumelifanyia kazi. kwa mwaka huu wa fedha tunaomaliza 2022/2023 tumeweza kuagiza magari 21 kupitia RUWASA, vilevile kwa mwaka ujao wa fedha 2023/2024 tuna magari 25 ambayo tumeagiza na wizara kama wizara imeagiza magari matatu, jumla magari 49. Vifaa hivi vya kazi tutahakikisha vinapatikana na kuongeza kila wakati kadri tunavyoendelea kupata fedha.

Mheshimiwa Spika, suala la kuwathibitisha watendaji wa RUWASA. Wabunge wengi wamewasemea mameneja wa wilaya. Tayari sisi kama wizara tumelichukulia hatua na tayari tumelifanyia kazi mpaka sasa watumishi 44 wameshathibitishwa na tayari watumishi 117 wapo kwenye vetting wanafanyiwa kazi ili na wao waweze kuthibitishwa. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, tumepokea ushauri na tutahakikisha hawa wote ambao watakidhi vigezo wataweza kupatiwa nafasi ambazo wanazifanyia kazi sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi na niseme tena Waheshimiwa Wabunge tunawashukuru kwa ushirikiano mkubwa tuendelee kushirikiana. Baada ya Bunge kama kawaida tutaendelea kufika kwenye majimbo kuhakikisha kazi zinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)