Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mungu, hatimaye nitoe shukrani na pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya kwa Taifa letu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuwatua akina mama au wanawake ndoo kichwani, dhamira hii inadhihirishwa na bajeti baina ya 2022/2023 na 2023/2024. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2023/2024 ni shilingi bilioni 756.205 wakati bajeti iliyopita ni shilingi bilioni 709.326, na ndiyo maana hii inadhihirisha hilo. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anahitaji dunia iendelee kuwepo. Bila kuwa na maji hakuna viumbe. Kama hakuna viumbe, nani ataishi katika hiyo dunia? Hakuna kitu. Kwa muktadha huo, ndiyo maana ya kutaka Watanzania na ulimwengu kwa ujumla uendelee kuwepo; kuna ile Sheria ambayo tumeipitisha hapa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mita sitini kutoka vyanzo vya maji, wasilime na wasifanye shughuli zozote za kibinadamu sehemu hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya kuyasema hayo, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Aweso pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu na watendaji wote katika Wizara hii. Hapa naungana na Wabunge wote, kila Mbunge aliyesimama, hakuna ambaye hajampongeza Mheshimiwa Rais, hakuna ambaye hajampongeza Mheshimiwa Waziri. Hawa ni viongozi wazuri ambao waliishika; aliyeishika Quran, aliyeishika Biblia, anatekeleza yale ambayo aliyaapa katika kiapo chake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nikushukuru tena, Jimbo langu la Mchinga, limetengewa pesa takribani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili kwenye maeneo yafuatayo: Mputwa, shilingi milioni 492; Mlangala A na B, shilingi milioni 340; Milola, shilingi milioni 496; Matimba, shilingi miloni 250; Nangaru, shilingi 58,322,000,000; Mkwajuni, halikadharika kama nilivyotaja pale Nangaru; na Mipingo shilingi milioni 400. Watu wa Mchinga wanakusubiri, wanasema, huyu kijana; maana wanakuita kijana, mtoto; tunamhitaji aje kwetu, hatuna cha kumpa. Hivi hapa tafuta muda ili twende, wale watakushukuru. Hata mimi Mbunge wao hawajaniambia wanachotaka kukufanyia pamoja na Naibu Waziri wake. Tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na miradi hii mipya ambayo umetupatia, kuna ule mradi ambao unatokea kule Myapa unakuja mpaka Mitaro hatimaye unaenda kwenye Jimbo la Mchinga. Kazi iliyofanyika ni kubwa na kazi iliyofanyika ni nzuri, na Mkandarasi anafanya kazi nzuri. Mimi hapo sitasema, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Ukishamnyonga, haki utampa saa ngapi? Hutaweza kumpa hiyo haki. Tumwombee aendelee kufanya hizi kazi ambazo wana-Mchinga wamemtuma na Watanzania wamemtuma. Kufanikiwa kwa Mchinga ni kufanikiwa kwa Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, tulipewa shilingi bilioni 12. Mpaka sasa tumepokea takribani shilingi bilioni 7.7, bado shilingi bilioni 4.7. Mradi ilibidi uishe mwezi Mei, bado haujaisha. Tunachoshauri, hizi pesa ambazo zimebaki, zipelekwe haraka. Wana-Mchinga wana imani sana na Mheshimiwa Waziri, na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sababu wakati wanachimba ile mitaro kuweka yale mabomba, hakuna aliyeamini, kwa sababu miaka mingi imepita Mchinga bila kuona ile koki ya kufungulia maji. Sasa hapo wameona kumesimama simama, tunaomba Mheshimiwa Waziri ajitahidi kadri inavyowezekana tumalize hizi shilingi bilioni 4.3. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, huu mradi ulikuwa wa awamu mbili. Awamu ya kwanza ni shilingi bilioni 12.4 na awamu ya pili ni shilingi bilioni 22.9. Wakati tunamaliza huu, tuangalie ile awamu ya pili. Kwa nini tunazungumzia awamu ya mbili? Ndani ya awamu ya pili, mradi huu utanufaisha maeneo mengi kama yafuatayo; kuna Kijiweni, Mnang’ole, Mvuleni A na B, Bimba, Kilolambwani, na Maluu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu mradi huu unapita mjini, kwenye mji kutokea Lindi kuelekea Dar es Salaam, njiani mle kuna vijiji navyo vitanufaika na mradi huu. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ni msikivu, Serikali yetu ni sikivu, naomba hili liwekwe kwenye ajenda kwa maana ya kwamba liwekwe kwenye utaratibu, wakati tunamalizia phase ya kwanza, tutaingia phase ya pili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nilikuwa nataka niseme hayo, nimshukuru Mheshimiwa Waziri, nimpongeze, na hizi pongezi anazopewa ni za haki na anastahili kupewa pongezi hizo. Msione vinaelea, mjue vimefanya nini? Vimeundwa, na waumbaji ni nani? Sisi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bila kuyapitisha haya, hayo mengine hayawezi kufanyika. Bila Mheshimiwa Rais kutafuta hizo pesa, mengine hayawezi kufanyika. Yatafanyikaje? Anayesimamia, Mwenyekiti pale ni nani? Ni Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, anafanya kazi kubwa na nzuri. Tunakutakia kila la kheri na Afya njema, Mwenyezi Mungu akubariki sana, akisaidiwa na Msimamizi anayesimamia Bunge, ambaye sio mwingine bali ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)