Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi hii leo ya kuchangia Hotuba ya Wizara hii ya Maji. Kwanza kabisa ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima wa kuwa hapa siku ya leo na pili ningependa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya na hasa katika sekta hii ya maji.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais, ana azma kubwa ya kumtua ndoo mama kichwani, katika kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa na miradi mingi ya maji. Lakini Mheshimiwa Rais si kumtua ndoo mama kichwani peke yake hata sisi wababa wanatutua mizigo ya mawazo vichwani kwa sababu wake zetu walikuwa wanatumia muda mwingi sana kwenda kufuatilia maji ambayo shughuli nyingine zenye maendeleo nyumbani zilikuwa zinasinyaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri ndugu yangu Mheshimiwa Jumaa Aweso kwa kazi kubwa anayoifanya. Mheshimiwa Aweso pamoja na Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Viongozi wengine wa wizara hiyo wanaitendea haki wizara yao kwa kuhakikisha kwamba miradi ya maji inafanikiwa katika nchi nchi hii.

Mheshimiwa Spika, waswahili wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni lakini Mheshimiwa Aweso hatonyongwa atapewa haki yake akiwa mzima na bajeti yake leo itapitishwa hapa ili aweze kwenda kutuhudumia watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia napenda niwapongeze wenzangu katika Jimbo la Bagamoyo na hasa viongozi, ma– engineer wanaotoa huduma katika maji ningependa nichukue nafasi hii kumpongeza engineer James Kionaomela ambaye yeye huwa mara nyingi sana anatupatia taarifa au Mbunge wake ananipatia taarifa katika miradi ya maji ambayo inayoendelea katika Jimbo la Bagamoyo. Pia ningependa kumpongeza manager wa DAWASA wa Mapinga ndugu yangu Abrahamu Mwenyemaki ambaye naye pia amekuwa msaada mkubwa kwangu kunipatia taarifa mbalimbali kuhusu masuala ya maji katika Jimbo langu la Bagamoyo.

Mheshimiwa Spika, tarehe 16 Machi, 2023 Mheshimiwa Waziri Mkuu alizindua mradi kubwa kabisa wa uhifadhi wa maji, alizindua tenki la maji la lita milioni tano pale maeneo ya Kibaha. Mradi huo wa maji umesaidia sana au unaendelea kusaidia sana Mikoa ya Dar es salaam na Pwani. Kwa sababu mradi huu utahudumia watu zaidi ya 37,000 katika Miji wa Dar es Salaam na Mji wa Bagamoyo.

Mheshimiwa Spika, ningependa kabisa nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwamba mradi huo wa maji ambao uko pale uliyozinduliwa wa lita milioni tano unasaidia katika kata zangu za Mapinga na hasa katika vitongoji vya Kibosha pamoja na Kimele, na vilevile unasaidia katika Kata ya Kerege katika vitongoji vya Kitanga, pamoja na Nyakahamba kwa kweli juhudi kubwa imefanyika na Serikali katika kuifanya hili zaidi ya dola milioni 86 zimetumika katika mradi huu.

Mheshimiwa Spika, kuna mradi mwingine wa upanuzi wa mradi wa maji wa Kidomole ambao umetumia shilingi milioni 334, zaidi ya milioni 334 mradi huu kwa kwakweli utakuwa mkombozi mkubwa sana kwa wananchi wangu wa kata ya Fukayosi hasa maeneo ya Kidomole katika Vitongoji vya Relini, kitongoji cha Mwanasenga, kitongoji cha Kinyamvuu pamoja na kitongoji cha Vihagata. Huu mradi utakapokamilika wananchi hawa nafikiri wataishukuru sana Serikali kwa kiwango kikubwa sana, kwa sababu miaka mingi sana hawana maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna mradi wa shilingi milioni 583 wa kupeleka maji katika Kijiji cha Kitame. Mradi huu wa maji wa milioni 385 unaendeshwa na mkandarasi mmoja anaitwa Amkami Mheshimiwa Waziri. Naomba nikwambie mradi huu ushafikia asilimia 35 lakini mpaka leo mkandarasi bado hajalipwa, ametumia pesa zake mwenyewe kwa uzalendo wake. Kwa hiyo, tunaomba muongeze juhudi katika kuwalipa wakandarasi ili miradi hii ya maji iweze kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna mradi mwingine wa maji ambao unaitwa Mradi wa SE Kitongoji cha Segwa pamoja na Magofi wa milioni 155. Mradi huu unaendelea vizuri na wananchi muda si mrefu wata-enjoy kupata maji.

Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Makurunge na Kata ya Fukayosi bado tuna changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji. Watu wa Fukayosi na Makurunge wanapata maji kutoka katika Mradi wa Wami, lakini sijui mpaka sasa hivi Mheshimiwa Waziri nini kinaendelea? Watu wa Makurunge, watu wa Fukayosi wanakaa mpaka miezi mitatu bila ya kupata maji.

Mheshimiwa Spika juzijuzi hapa watu walinipia simu ilifikia hatua mpaka walimu wakataka kufunga Shule Msingi pale Mkenge kwa sababu wanafunzi hawana maji ya kutumia. Nikamuomba Meneja wa DAWASA wa Chalinze Fumbuka ilibidi atume doza la kupeleka maji pale shuleni wananchi ili waweze kunusurika. Kwa kweli Waheshimiwa Waziri hali ya pale mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nimeona katika hotuba yako nimeona pesa ambazo umezitenga kwa kipindi cha bajeti ya Mwaka 2023/2024 kuna miradi ambayo nitanufaika nayo. Mradi wa Kifuda Razaba, Mradi wa Wami Fukayosi, Makurunge, Mkenge Fukayosi, Kalimeni yote imeingizwa katika programu ya kupatiwa pesa kwa kipindi hiki kijacho hili miradi hii iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala moja ambalo nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri. Suala la Misamaha ya Kodi kwa Vyombo au Vifaa vya Miradi ya Maji. Mheshimiwa Waziri hakuna kitu kinachokuchelewesha sana katika miradi yako kama jambo hili hebu jaribu kufanya kila njia utakayoiweza. Kaa na mamlaka zinazohusika pale wakandarasi ambapo wameishapata tender kuhakikisha wanapatiwa hii misamaha ya kodi haraka iwezekanavyo ili miradi iweze kuendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu leo hii utakuta mkataba wa mradi unasainiwa lakini bado mradi unaweza ukakaa zaidi ya miezi minne, mitano mpaka sita au mwaka mmoja ukiulizwa mradi huu kwanini hauendelei utaambiwa kwamba bado hatujapata msamaha wa kodi. Kwa hiyo, niombe Wizara yako nikuombe Mheshimiwa Waziri, uwe karibu na viongozi hawa ambao wanatoa hii misamaha ya kodi kwa ajili ya hii miradi ya maji kukufanyia haraka na wepesi zaidi ili…

SPIKA: Mheshimiwa, Kengele imeishagonga.

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: …ili uweze kuhakikisha kwamba Miradi hii inafanyika kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache nashukuru sana, Ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)